WAKILI Jeremiah Mtobesya aliyekuwa akiwawakilisha Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake nane wa chama hicho, amejitoa kwenye kesi hiyo leo Agosti 23 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Mtobesya amejitoa katika kesi hiyo baada ya Mahakama ya Hakimu Kisutu kutupilia mbali maombi yao ya kutaka kesi hiyo ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 iahirishwe katika Mahakama ya Kisutu ili kusubiri maombi yao na rufaa yaliyowasilishwa kwenye Mahakama ya Rufani yasikilizwe kwanza na kutolewa maamuzi.

Kwa upande wake, hakimu Mashauri alitupilia mbali maombi hayo kwa maelezo kwamba, kifungu cha sheria walichotumia cha 225 (1) (2) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 hakiipi mamlaka hayo.

Ikumbukwe kwamba, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwamo kuhamasisha maandamano Februari 16 mwaka huu siku moja ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni yaliyosababisha mwanafuzni Akwilina kuuawa kwa risasi.

By Jamhuri