2016: Mwaka wa machungu kwa ‘mapedejee’

Zikiwa zimesalia siku 18 tu kumaliza kwa mwaka huu, baadhi ya Watanzania wameuona mchungu katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli.

Mwaka huu umekuwa mchungu kwa wale waliozoea kuishi kwa mipango, wasiokuwa na kazi maalumu zaidi ya kuishi maisha ya ujanjaujanja, huku wakiwa na matumizi makubwa ya pesa.

Ni mwaka ambao kila mmoja alikuwa na mipango. Kuna waliofanikiwa na kuna walioangukia pua, kwa maana ya kutofikia malengo. Hayo yote ni matokeo katika maisha ya kila siku.

Mwaka mmoja tangu Rais Magufuli aingie madarakani, moja ya mambo yanayotiliwa mkazo na Serikali ya sasa ni pamoja na dhana ya uwajibikaji.

Awali, dhana hii ilionekana kuwa ngumu kidogo kwa wale wasiopenda kuwajibika kwa wakati. Ilikuwa ngumu pia kwa baadhi ya wasanii wa muziki na tasnia nyingine za sanaa.

Asilimia kubwa ya wasanii hapa nchini wanatumia vipaji zaidi ya kuwa na taaluma ya sanaa husika. Huenda ndiyo maana baadhi yao wamegeuka ombaomba kwa kutumia nafasi yao ya umaarufu.

Ni jambo la kawaida sana kumuona msanii mwenye jina kubwa, akikatiza huku na kule akiomba msaada, nauli au wakati mwingine hata hela ya kutumia. Kuna wengine kama ana gari ataomba hela ya mafuta. Katika hatua hii, wengine wamefikia kuomba walipiwe hata kodi za nyumba kutoka kwa mashabiki wao waliojenga urafiki wa karibu.

Kuna waliopenda hali hiyo ya kuombwa hela na baadhi ya wasanii. Kundi la watu wa namna hii mara nyingi huitwa ‘mapedejee’.

Mapedejee si matajiri kihiivyo, bali ni kundi fulani la watu wanaopenda sifa. Hali hiyo imewasababishia kuwa marafiki wa karibu wa wanamuziki ili majina yao yatajwe mara kwa mara kwenye bendi ili kujiongezea umaarufu. 

Hii inaweza kuwa wakati bendi ikifanya onesho mubashara au wakati wa kurekodi nyimbo studio, ndipo majina ya mapedejee hao hutajwa kila ubeti. Wakati mwingine ubeti mmoja unaweza usiwe na maneneo mengine zaidi ya kutaja majina ya mapedejee. 

Kuna wakati fulani, baadhi ya bendi za muziki wa dansi zilikuwa haziwezi kupiga kumbi tofauti, kutokana na hali ya kujenga mazingira ya kuwa na ukumbi wa nyumbani.

Limekuwa jambo la kawaida kusikia kuwa ukumbi fulani ni wa bendi fulani. Kwa hiyo, inapotokea bendi nyingine ikatumia ukumbi ule inakuwa taabu sana kupata watu kama wanaohudhuria inapopiga bendi iliyozoeleka ukumbi husika.

Mwaka 2016 umekuwa mwaka mbaya kwa mapedejee kutokana na ukata uliowakumba. Mapedejee wanalia njaa baada ya mirija yao ya kujipatia pesa bila kutokwa na jasho kukatwa. Tulizoea kuona mbwembwe za mapedejee wakimwaga pesa kila wanapotajwa majina yao. Waliishi kama malaika lakini sasa sijui wanaishi kama nini!

Mapedejee wamekuwa kimya kama vile hawajawahi kuwapo. ‘Hapa kazi tu’  imewanyamazisha na kuwapoteza katika anga ya matanuzi na matumizi yasiyo ya lazima.

Wanamuziki wanalia kutengwa na mapedejee waliozoea kuwamwagia pesa kila uchao. Wanalia ukata uliosababishwa na falsafa za mkuu wa nchi anayetaka asiyefanya kazi na asile.

Maisha ya wanamuziki na wasanii kwa ujumla yamekuwa magumu. Waliozoea kuishi kwa kutegemea mifuko ya mapedejee wanalalama na kuilaumu Serikali.

‘Hapa kazi tu’ imekuwa chungu kwa baadhi ya ndugu zetu waliokuwa wakiamini kuwa ni haki yao kupewa pesa za bure na mapedejee.

Waliozoea kuishi kwa ujanjaujanja bila kutokwa na jasho sasa wanaishi kwa majuto. Mwaka 2016 unaisha huku Watanzania wakijivunia mabadiliko yaliyoanza kuomba usawa na kuondoa kiburi kwa baadhi yetu.

1255 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons