Adha ya ‘Double allocation’ (2)

Ndipo akateuliwa Jaji Mihayo kuisikiliza. Huyu naye alianza kuisikiliza upya. Kesi imenguruma kwa Jaji Mihayo kuanzia tarehe 01/12/2006, ikaendelea tarehe 13/04/2007, 26/06/2007, 10/07/2007, 02/11/2007. Kutokana na maombi ya wavamizi kwa Jaji Mihayo barua Kumb. Na. Mushy/A58/LND ya tarehe 03 Julai 2007, Jaji Mihayo alitoa muda yafanyike makubaliano nje ya Mahakama, tukiwa tayari turudi mahakamani kwa uamuzi wa kumalizika kwa kesi hii 266/94.

Tarehe 21/05/2008 mawakili walikubaliana kwenda Ardhi kupata suluhu ya suala hili.Tarehe 15/07/2008 mawakili wa pande zote nikiwamo na mimi tulikwenda kumuona Kamishna wa Ardhi Bwana Msangi.  Ujumbe ule ulijumlisha – Wakili Mbwambo upande wa Mashtaka, Wakili S A Mwaikambo kuwakilisha Attorney General, Kamishna wa Ardhi na Wakili Mujaya kuwakilisha City Director, Wakili Harun Mahundi (Inspector General mstaafu) akiniwakilisha mimi na watoto wangu (5th, 6th and 7th defendants). 

Tulimuona Kamishna na baada ya mimi kujieleza na kutoa ombi la kumaliza kesi kwa maelewano iwapo Kamishna angeridhia kutoa viwanja mbadala kwa washitaki.

Nafurahi kusema Kamishna Msangi alikuwa mwelewa na mtekelezaji mambo kijeshi kama alivyopevushwa katika kambi za JKT, akatoa kiwanja No. 176 Block 8 kule Mwongozo Kigamboni gharama zake kimalipo ni 1,490,000/-. Wakili wa mashtaka akakikubali na kuahidi mteja wake atakilipia. Tarehe 16/7/2008 tukakutana mbele ya Jaji Mihayo kutoa mrejesho wa makubaliano nje ya Mahakama. Kwa maelewano yale pale Mahakama Kuu, tulipangiwa tarehe 11/8/2008 kufika kusikiliza hukumu ya kesi No. 266/98.

Tarehe 11/8/2008 saa 3 tukafika mahakamani. Mimi nilitegemea Jaji atatoa maelezo marefu ya kesi ilivyokwenda hadi pale ilipofikia tamati ndipo nisikie hukumu. Haikuwa hivyo, kilichotokea ni utaalamu wa kisheria (legal technicality). Nilisikia tu Wakili wa mshtaki, Bwana Mbwambo, akisema nanukuu, “My Client agreed to pay the fees requested. The matter has now been settled and let it be marked so”. Ndipo nikamuona Jaji Mihayo akisimama na kusema, namnukuu, “Order:The matter be and is hereby marked as settled out of Court. No order as to costs”.

Huo ni uamuzi mfupi sana. Kesi iliyoanza tarehe 26/6/1998 hatimaye imemalizika kwa maneno machache namna hiyo! Nilipigwa na butwaa lakini sikuwa na la kufanya. Wakili wangu, Harun Mahundi, akanituliza kwa kuniambia, ‘Mzee, sasa ungojee nipate mwenendo mzima wa kesi na hayo maelewano ya nje ya Mahakama ndipo uende wizarani kuomba hati za viwanja vyako uviendeleze’.

Hiyo ninaita ni hatua ya kwanza (phase I) katika kutafuta haki yangu. Imenichukua miaka 10, wamesikiliza majaji wane (ilianzia na Jaji Msumi, Jaji Kyando, Jaji Mwaikugile na hatimaye Jaji Mihayo). Ninajiuliza, kweli kesi namna hii haingeweza kumalizika katika miezi michache tu hata mwaka mmoja tu? Ni ukiritimba wa sheria za kikoloni wa Uingereza. 

Katika himaya ya Mwingereza (in the British Empire) wote walifuata sheria za Uingereza. Utaratibu wao unasema hivi “every person is innocent until proved guilty” yaani kila mtu ni maasumu, yaani asiye na hatia mpaka pale Mahakama itakapomuona ana hatia. Kwa maneno mengine mtu anaweza kutuhumiwa tu (be a mere suspect) hivyo hana kosa lolote. Katika kesi za “double allocation” mtazamo huo unafuatwa sana. 

Kule Ufaransa wale jamaa sheria zao ziko tofauti. Kule bwana kila mtuhumiwa katika uhalifu basi ni mkosaji mpaka pale atakapojithibitishia uzuri wake yaani kwa Wafaransa. “Every suspect is a criminal until he proves his innocence”.

Hiyo ni mitazamo miwili tofauti namna ya kutoa haki kwa raia. Sisi ndiyo tumeiga kutoka waliotutawala – Waingereza. Matokeo yake kuna huo mlolongo wa hatua lukuki mpaka kufikia kumalizika kwa kesi ndiyo maana kesi zinachukua miaka kukamilika. 

Baada ya kupatiwa “Court Proceedings” pamoja na hukumu ndipo nikaenda wizarani kwa Kamishna wa Ardhi kuomba hatimiliki kwa viwanja vyangu No. 387 & 388 Jangwani Beach. 

Loo! Nako nikajikuta naanza upya kuitafuta hiyo haki yangu. Wizara walinipa barua No. LD/138492/26/LK ya tarehe 16/12/2008 nikaipeleka kwa Mkurugenzi wa Kinondoni (wakati ule alikuwa H. Katanga). Huko nikapata mshtuko wa mwaka. Nikaulizwa umepita ‘site’ ukaona hali ilivyo? Nikajibu bila kusita sijapita. Wakanishauri niende nikaone kwanza kisha nirudi pale Kinondoni kwa Afisa Ardhi (akiitwa mama Kessy). Nikaenda ‘site’ huko ndiko nilikoishiwa na nguvu. Kiwanja No. 387 nilikuta kuna tawi la wakereketwa wa CCM Kilongowima, na bendera inapepea. Kiwanja No. 388 kuna ukuta umezungushwa, kuna geti kubwa na ndani kuna kibanda cha mtu eti anafyatua matofali na kuyauza. Kimekuwa kiwanda cha matofali!

Basi kama usemi wa kale enzi za Wayahudi usemao ‘ukishangaa ya Mussa utastaajabu ya Firauni’, nikaenda kwa Mkurugenzi kuripoti hali niliyoiona na kumwelezea mbona Mahakama Kuu tuliambiwa viwanja vile visiendelezwe na yeyote mpaka kwanza huu mgogoro wa “double allocation” umalizike? Imekuwaje leo Kinondoni mmemilikisha watu bila ya mimi kuhusishwa? Afisa Ardhi Kinondoni akajieleza eti Jiji lilikuwa ni mamlaka (authority) tofauti kabisa na Wizara. 

Nikashauriwa niende Mahakama ya Nyumba na Ardhi kuomba “Eviction order” vinginevyo, mimi kama mimi sina uwezo wa kumtoa mtu pale. Nilifanya kama nilivyoshauriwa. 

Tarehe 6/2/2009 nilifika Mahakama ya Nyumba Kinondoni nikaomba hiyo amri ya kuwaondoa wavamizi katika maeneo yangu. Nikajikuta naanza upya kudai haki yangu. Makarani waliniuliza, ‘Mzee, una wakili?’ Nikajibu sina. ‘Utaweza kulisemea mahakamani kweli?’ Nikajibu kwani kuna ugumu gani hapa? Wakasema kwa shingo upande haya. Wakanipa fomu No. 1 In the District Land and Housing Tribunal’ kwa mujibu wa The Land Disputes Courts Regulations (GN. 174/2003). Nikajaza moja kwa kiwanja 388 ikawa ombi No. 39/9 na fomu ya pili kwa kiwanja No. 387 ikawa ombi No. 40/9 chini ya  Mwenyekiti wa Baraza lile la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kinondoni, Mhesh. Davis. 

Huko nako mambo hayakuniwia mteremko au laini bali yalinichanganya zaidi kupita hata kule Mahakama Kuu. Nikiwa na fikra kwamba Baraza la Ardhi na Nyumba watakachofanya ni kusikiliza na kuona vielelezo kutoka pande zote mbili (kutoka kwangu na kutoka kwa wavamizi) kisha watatafuta ofa zipi ni “genuine” na zipi ni “fake” basi watatoa uamuzi katika muda mfupi tu. 

Lo!, nilikuwa nimedanganyika. Hapa ni Bongo! Hakuna busara wala hekima kama zile za Mfalme Suleiman katika Biblia. Labda niwakumbushe uamuzi wa Mfalme Suleimani hapo kale ulikuwaje, katika Biblia. Imeandikwa “Hukumu ya Suleimani”. Kufupisha stori ya hukumu ile nashauri wasomaji wa makala hii wakasome kitabu cha Wafalme sura ile ya 3 aya za 16-28. 

Kwa kifupi ilikuwa hivi: akina mama makahaba wawili waliokiishi katika nyumba moja na chumba kimoja walizaa watoto kila mmoja na siku yake. Ikitokea siku moja wakiwa usingizini mama mmoja alimlalia mtoto wake na hivyo kusababisha kifo cha mtoto yule. Mama kushtuka, mtoto wake kafa akaamka taratibu na kupeleka maiti yule kwa yule mama mwingine, akabadilisha na akamchukua yule mtoto mzima wa mwenzake, akenda kulala naye akimkumbatia. Yule mama mwingine alipoamka na kuona ana kitoto kilichokufa, hakuridhika ndipo asubuhi akina mama wote wawili wakaenda kwa Mfalme Suleiman kuomba haki ya kuwa na mtoto hai yule. 

Baada ya Mfalme Suleiman kuwasikiliza maneno yao kila mmoja wa akina mama wale akaja na uamuzi huu: “Nileteeni upanga”. Wakaleta upanga mbele ya Mfalme. Mfalme akasema mkate mtoto aliyehai vipande viwili, kampe huyu nusu na huyu nusu.” Ndipo mwanamke yule ambaye mtoto aliyehai ni wake akamwambia mfalme – kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma akasema, “Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai wala usimuue kamwe.” 

Lakini yule mwingine akasema “asiwe wangu wala wako, na akatwe” ndipo mfalme akajibu akasema “Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake”: (Kasome I Fal. 24-28).

 

>>ITAENDELEA 

1369 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons