Adha ya ‘Double allocation’

Jamani, mambo haya ya kiwanja kimoja kugawiwa watu zaidi ya mmoja, wenyewe kule Ardhi wanaita “double allocation” myasikiege tu, yakikufika ndipo utakapo jua hasa adha yake ni nini! 

Mimi ninayaandika yaliyonipata katika hiyo inayojulikana kama “double allocation”. Kuna wananchi wengi hapa nchini wanasulubiwa na dhuluma namna hii. 

Kuna methali ya Kiswahili inayosema hivi “Adha ya kaburi, aijuaye maiti”, na kuna usemi kuwa “Siri ya mtungi aijuaye kata”. Suala hili la “double allocation” siyo la ajabu. Limewapata wengi na limewasononesha wengi hapa nchini kwenye masuala ya kiwanja kimoja kugawiwa kwa wahitaji zaidi ya mmoja. Hili linawezekana na linatokea sana katika miji yetu. Hili linatokea kwa sababu ya utaratibu mbovu au niwe wazi uchu wa fedha kwa maafisa Ardhi wa nchi hii na upindishaji wa sheria zilizopo kwa manufaa yao binafsi. Basi mimi ni mmoja niliyewahi kukumbwa na hilo sakata la “double allocation” hapa jijini Dar es Salaam. Nimeonja joto ya jiwe ndiyo hiyo adha ya ‘double allocation’ kwenye viwanja. 

Kwa manufaa ya wasomaji wa makala zangu, nitaelezea kifupi sana nilivyokirihika kwa muda wa miaka 18 mpaka kufikia tamati ya sakala lote la “double allocation” na nikapata HAKI yangu. Wanasheria wana usemi maarufu kuwa “Justice delayed is justice denied”. Sijui kabisa kama usemi huu mahakimu na mawakili wanafuata (practice) kikamilifu. Kama kweli usemi ule ungetekelezeka (adhered to) kesi zisingechukua miaka mingi namna hii). 

Huko mahakamani wao wanao ule utaratibu wao wa hatua mbili; nazo ni “mention” au kesi kutajwa mara kadhaa na “hearing” yaani kesi hiyo kusikilizwa. Mlolongo mrefu unaofuatwa hapa nchini unasababisha kwanza kesi kuchukua muda mrefu kumalizika na pili haki ya mwombaji inacheleweshwa na ndipo kisheria inakuwa haki ya mtu imenyimwa! 

Je, Tume ya Haki za Binadamu wanajua na kufuatilia hili katika Mahakama za Ardhi Wilayani (District Land Tribunals)? Labda muda wa kusota waombaji ungelipunguka, sijui lakini. 

Lakini la tatu, ucheleweshwaji wa kesi namna hizi kunajenga mazingira ya rushwa. Mtu akiona anazungushwa sana basi anaamua atoe chochote ilimradi kesi isikilizwe mapema. 

Hebu soma kesi hii iliyotokea Morogoro tangu mwaka 1994 na Baraza la Ardhi na Nyumba mkoani Morogoro (Land Tribunal) hatimaye wakahitimisha mwaka 2012. Imenukuliwa kutoka gazeti la Tanzania Daima, Jumamosi Mei 12 2012 uk. 5 kichwa cha habari ‘Afisa ardhi ahukumiwa kulipa mil. 25/-‘. Kesi ile ilihusu kiwanja No. 24, kitalu ‘G’ eneo la viwanda Manispaa ya Morogoro. Kesi ilikuja mbele ya Mwenyekiti, Bi. Alycia Mtunga. Mlalamikaji alikuwa Allen Msengo na mlalamikiwa alikuwa Afisa Ardhi Mkoa, Violet Kimeme. Kesi ililetwa tangu 1994 na imeendelea kusikilizwa mpaka kufikia kutolewa uamuzi mwaka ule 2012 takribani miaka 20. Hapo haki ya mwombaji iko wapi? Je, kama angekufa si ndiyo basi? 

ile Afisa Ardhi Mkoa mhusika alitumia madaraka ya ofisi yake vibaya pale alipojimilikisha kiwanja kile huku akijua kilishatolewa “offer” kwa mtu mwingine tangu 1993. Kibaya zaidi akajenga kabisa na nyumba na kujitafutia hatimiliki isivyo kihalali. Huko ni kutumia madaraka ya ofisi vibaya. 

Basi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu si Athumani,  Baraza lilifikia uamuzi wa kumpa haki yule aliyepata offer mwaka 1993. Hatimaye Baraza la Ardhi na Nyumba liliona ulikuwapo ukiukwaji wa sheria pale, na ndipo Baraza kwa haki kabisa likamhukumu Afisa Ardhi yule kubomoa majengo yake katika kiwanja kile na zaidi ya hivyo Afisa yule alipe fedha taslimu sh. milioni 25 kwa mwenye kiwanja kile kwa kosa la kuvamia, kumilikisha na kumcheweshea mwenye kiwanja kukiendeleza, tangu alipomilikishwa mwaka 1993. Juu ya hapo, aliamriwa kulipa gharama zote za kesi ile. 

Sasa tuje kwangu. Mimi nilipewa “Offer” za viwanja vile No. 350 na 351 Jangwani Beach na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi tangu tarehe 3/10/1988 kwa offer toleo la Wizara LD/136219/1/CCC na LD/136218/1/CCC ya tarehe 3/10/1988 kwa viwanja No. 350 na 351 Jangwani Beach Kinondoni, Dar es Salaam. Nikavijengea uwigo wa nguzo za simenti. (Fencing Poles) kuzunguka viwanja vyote 2. Wakati ule huko Jangwani Beach kulionekana kama pori tu. Jirani zangu walikuwa Afisa Mkuu wa Magereza mstaafu,Josephat Mwingira, na Dr. Longinus Dismas Nyoni kwa jina la mitaani Dk. Zamngoni. Upande wa mashariki kulikuwa na plot kubwa mali ya Art Gallary – pori la kutisha. 

Wapima viwanja wa Wizara wakashauri nisianze ujenzi mpaka Mkurugenzi wa upimaji atakapotoa kibali (Director of Survey approval). Baada ya upimaji kukamilika 1996 (ulifanywa na mpima akiitwa Stephen Nyabusani) viwanja vile vilipatiwa nambari mpya vikawa No. 387 na No. 388. Niliitwa wizarani na kubadilishiwa zile nambari za viwanja vyangu katika offer sasa nikapatiwa No. 387 na No. 388 kwa mhuri wa Wizara tarehe 3/4/1998. Mpima viwanja Stephen Nyabusani  akaniambia viwanja vyako mzee viko “intact”, unaweza kwenda kuviendeleza. Huo ulikuwa mwaka 1998. 

Wakati mimi naelezwa na Wizara kuwa sasa unaweza kuanza kuendeleza viwanja vyako, kumbe Jiji limeshagawa viwanja vile kwa watu wengine kwa offer za Jiji No. DCC/LD/57925/4/5M kwa kiwanja No. 387 na No. DCC/LD/57926/2/TMM kwa kiwanja No. 388 za tarehe 16 Mei 1997.

Hapo ndipo ile “double allocation” ilivyotokea. Mamlaka mbili tofauti zimetoa viwanja vile kwa wahitaji tofauti na kwa nyakati tofauti. Mzee Josephat Mwingira akaja kunitaarifu kuwa viwanja vyako vimevamiwa na watu wameshaanza ujenzi – tafadhali njoo uone. Nilifika saiti na kukuta kazi ya kuchimba msingi inaendelea. Nilipokuja kwa Dk. Zamngoni naye akanieleza eti alifikiri nimewauzia.

Hapo ndipo nilikwenda Ardhi kumuona Kamishna anieleweshe uvamizi umetokeaje. Wakati huo mama Longway ndiye aliyekuwa Kamishna wa Ardhi. Baada ya kuona “offer” zangu akatuma maafisa Ardhi wake saiti kupata ukweli wa hali halisi. Bwana Jamal Jaff, Afisa Ardhi, akifuatana na wapima viwanja tulikwenda saiti Jangwani Beach, walikutana na majirani zangu, Mzee Josephat Mwingira (mstaafu Magereza) na Dk. Zamngoni, Longinus Nyoni. Mafiasa Ardhi wale wakatoa ripoti yao kwa Kamishna wa Ardhi Jaji Longway. 

Uamuzi wa Wizara ulitolewa kwa barua ya Wizara No. LD/136218/20 ya tarehe 23/02/1998 iliyojieleza wazi wazi. Jiji kwa kutekeleza uamuzi ule, lilitoa barua kwa wavamizi Kumb. No. DCM/LD/35988/18 ya tarehe 12/3/1998 yenye maelekezo kwa wavamizi.

Kama hayo maagizo hayakutosha, Wizara iliwaandkia barua wavamizi Kumb. No. LD/169327/17 na LD/136218/22 tarehe 07/05/1998 warejeshe hatimiliki zao kwa kuwaelewesha kuwa zilitolewa kwa makosa, hivyo siyo halali. Walitakiwa wazirejeshe (surrender)kwa Msajili wa Hati Wizarani zikafutwe, walipewa siku 14 wazirejeshe hati zile. 

Kilichofuata baada ya pale sasa ndicho ninachokiita adha ya “double allocation”. Kwanza wavamizi hawakurejesha zile hati. Pili kwa vile wana uwezo kifedha walikwenda Mahakama Kuu Dar es Salaam kupinga uamuzi ule wa Wizara. Huko wakafungua kesi No. 266/1998 iliyojulikana kama Civil Case No. 266 of 1998 Salvatory P. Mushumbushi Versus Commisioner for Land and others. 

Hapo ndipo nikajikuta naingizwa katika lile kundi la others. Tulioshtakiwa tulikuwa wanne nao ni:-

1. The Commissioner for Lands 2. The Attorney General 3. The Dar es Salaam City Commissioner na 4. Brigadier General FX Mbenna wakatumbukizwa na watoto wangu 5 John Stephen Mbenna 6 Joseph Frederick Kambona.

Kesi ilianza kutajwa hapo Mahakama Kuu tokea tarehe 26/06/1998 mbele ya Jaji Msumi, ikaendelea kutajwa (mention) mbele ya Jaji Kyando (mpaka alipofariki) ikapelekwa mbele ya Jaji Mwaikugile. Huyu alishaisikiliza na ikabakia kutoa hukumu tu. Ghafla Jaji yule akateuliwa kuwa Zonal Judge Ukanda wa Kaskazini – akahamia kwenye kazi yake mpya bila ya kutoa hukumu ya kesi hii. 

Ndipo akateuliwa Jaji Mihayo kuisikiliza. Huyu naye alianza kuisikiliza upya. Kesi imenguruma kwa Jaji Mihayo kuanzia tarehe 01/12/2006, ikaendelea tarehe 13/04/2007, 26/06/2007, 10/07/2007, 02/11/2007. Kutokana na maombi ya wavamizi kwa Jaji Mihayo barua Kumb. Na. Mushy/A58/LND ya tarehe 03 Julai 2007, Jaji Mihayo alitoa muda yafanyike makubaliano nje ya Mahakama, tukiwa tayari turudi mahakamani kwa uamuzi wa kumalizika kwa kesi hii 266/94.

Tarehe 21/05/2008 mawakili walikubaliana kwenda Ardhi kupata suluhu ya suala hili.Tarehe 15/07/2008 mawakili wa pande zote nikiwamo na mimi tulikwenda kumuona Kamishna wa Ardhi Bwana Msangi.  Ujumbe ule ulijumlisha – Wakili Mbwambo upande wa Mashtaka, Wakili S A Mwaikambo kuwakilisha Attorney General, Kamishna wa Ardhi na Wakili Mujaya kuwakilisha City Director, Wakili Harun Mahundi (Inspector General mstaafu) akiniwakilisha mimi na watoto wangu (5th, 6th and 7th defendants). 

Tulimuona Kamishna na baada ya mimi kujieleza na kutoa ombi la kumaliza kesi kwa maelewano iwapo Kamishna angeridhia kutoa viwanja mbadala kwa washitaki.

 

>>ITAENDELEA 

1498 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons