Je, unajua kwamba Tanzania sasa kuna teknolojia ya kubadilisha majitaka na kuwa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu? Pengine utabaki umeduwaa, ila jambo hilo sasa linawezekana kutokana na mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandera, kilichoko jijini Arusha, Dk Askwar Hilonga, kuvumbua teknolojia mpya.

Dk. Hilonga ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu kutoka Korea Kusini, ameliambia JAMHURI kuwa alianza kufanya utafiti huo akiwa bado anasoma shahada hiyo.

“Nilianza utafiti huu wakati nasoma shahada ya uzamivu nchini Korea ya Kusini. Nilibobea kwenye materials yanayoitwa NANOMATERIALS. Materials haya yanafaa kwa kazi mbalimbali; mimi nikayabuni yanayoweza kuondoa kemikali kwenye maji.

“Baada ya kurudi Tanzania nikaajiriwa chuo cha Nelson Mandela mahali ambapo nikabuni mtambo wa kuchuja maji, ambao sasa tumeupa jina la NANOFILTER,” amesema Dk. Hilonga.

Mtaalamu huyo amesema kilichomsukuma kufanya utafiti huo na kuja na suluhisho kwa matatizo ya maji chini kutokana umuhimu wa kuwa na jamii yenye afya kama nguzo ya maendeleo binafsi na kwa taifa.

Amesema bila kuwa na afya njema, shughuli za uzalishaji haziwezi kufanyika sawa sawa kwa kuwa muda mwingi hutumika katika kujiuguza huku kiasi kikubwa cha fedha kikipotea.

“Kwa miaka mingi jamii hasa ya watu wanaoishi kwenye mazingira ya vijijini, na hata mijini wamekuwa wakinywa na kutumia maji machafu yasiyo salama kwa afya zao,” amesema Dk. Hilonga.

Juhudi zake hatimaye zimezaa matunda, baada ya uvumbuzi wa chujio la kusafishia maji maarufu kama Nano filter, lenye uwezo wa kusafisha maji na kuondoa taka zote na vimelea vya magonjwa bila kutumia kemikali wala nishati ya aina yoyote, huku maji yakibakia kuwa na ladha yake halisi kufanikiwa na kuanza kufanya kazi rasmi hapa nchini.

Teknolojia hii ya kusafisha maji kwa kutumia viasili, inayofahamika kitaalamu kama Nano technology, ni uvumbuzi wa Mtanzania Dk. Hilonga aliyebobea katika masuala ya kemia na kufikia kiwango cha juu cha elimu hiyo ya kemia na hatimaye kugundua chujio hilo.

Dk. Hilonga ameliambia JAMHURI, kuwa chujio hilo maarufu kama nanofilter linaloweza kusafisha maji kutoka kwenye madimbwi, mito, na mabwawa, ambayo kiuhalisia yanakuwa na vimelea vya magonjwa kama vile amiba, bakteria, floraidi, na aina nyinginezo za madini ambazo si salama kwa afya ya binadamu, na kuyafanya safi kwa ajili ya kunywa bila madhara yoyote.

Muundo wa chujio la Nano ukoje?

Dk. Hilonga amesema chujio hilo  linajumuisha muunganiko wa uchujaji wa maji taratibu kwa kutumia mchanga, pamoja na muunganiko wa ‘matirio’ za nano ambazo zimeumbwa kutokana na sodium silicate na silver kuweza kuondoa kemikali nzito ambazo haziwezi kuondolewa na chujio la kawaida.

Mtalaamu huyo ameliambia JAMHURI kuwa chujio linatumia mchanga kwa ajili ya kuchujia maji. Amesema matumizi kama hayo yamekuwepo kwa muda mrefu huku aina hiyo ya chujio imekuwa ikiondoa aina nyingine za vimelea kwenye maji, bila kuondoa kemikali.

“Maji huanza kuchujwa kwa kupita kwenye mchanga kwanza, kisha hupita kwenye mashine za nano zilizowekwa kwenye chujio na kuingia katika sehemu ya mwisho ya chombo cha kukingia maji. Maji yanapofika katika sehemu yenye muunganiko wa nano, husafishwa na kuondolewa sumu zote kulingana na geografia ya eneo husika.

“Kwa kawaida kila ukanda una changamoto zake kwenye suala la maji. Katika maeneo mengine, maji yana madini ya fluoride iliyozidi, ambayo huathiri meno na mifupa kwa kiasi kikubwa,” amesema Dk. Hilonga.

Mtafiti huyo amesema mtambo huo ndiyo umeingizwa sokoni na maeneo ambayo tayari wananchi wameanza kunufaika nao ni pamoja na mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Kilimanjaro na Manyara.

Dk. Hilonga ameliambia JAMHURI, kwamba tayari mahitaji ya teknolojia hiyo yameanza kuwa makubwa duniani, huku akipata kandarasi kadhaa kutoka baadhi ya nchi za Afrika, India na Pakistan. Amesema ana Imani kuna siku teknolojia hiyo kutoka Tanzania itasambaa kote duniani.

Ameshinda tuzo nne za kimataifa na tuzo moja ya kitaifa kwa ajili ya ubunifu wake wa mtambo wa Nanofilter. Tuzo ya kwanza inaitwa Africa Prize for Engineering Innovation 2015 iliyofadhiliwa na The Royal Academy of Engineering, United Kingdom.

Kwenye tuzo hiyo alipata zawadi ya kwanza ambayo ni Sh milioni 80. Ameliambia JAMHURI kuwa pesa hizo zilimsaidia kuanzisha kampuni yake inayoitwa Gongali Model ambayo sasa ina waajiriwa zaidi ya 20. 

Amesema tuzo nyingine tatu alizipata jijini London, Uingereza, ikiwepo tuzo ya Pitch at Palace ya Mwana wa Malkia Elizabeth akishirikiana na tajiri wa Afrika, Aliko Dangote na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

Tuzo ya kitaifa aliyoipata inaitwa National Health Innovation Award by NIMR, tuzo aliyotakiwa kupewa na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, na alikabidhiwana aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

 

Utafiti umepokelewaje?

“Utafiti wangu umepokelewa kwa furaha wengi wamenipongeza kwa njia nyingi, hasa kupitia mitandao ya kijamii – facebook na twitter. Wote tumejivunia kuona Mtanzania anaweza kupenya na kuwa mshindi kwenye mashindano ya kidunia, kama yaliyofanyika London – tulishindana na nchi kadhaa kutoka mabara manne; Europe, Africa, Asia, and South America,” amesema Dk. Hilonga.

Watu zaidi ya 200 wameshanunua mitambo hiyo, ambapo mtambo mmoja unauzwa Sh 300,000. Amesema kwa sasa tayari kampuni yake inavyo vituo 150 vinavyoendeshwa na wajasiriamali waliokodishiwa mitambo hiyo ya kuchuja maji.

Mjasiriamali anachuja na kuuza maji na kulipa Sh 6,000 kwa wiki kwa Gongali Model. Pato lote lililobaki ni lake. Wengine wanaingiza mpaka Sh 20,000 kwa siku. Na kwa sasa huduma imewafikia watu 8,000.

2463 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!