Nitatumikia nchi yangu na watu wake wote. Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote. Nitasema ukweli daima, fitina kwangu mwiko. Hizi ni ahadi tatu kati ya kumi za mwanachama wa TANU. 

Ukizitazama kwa utulivu na ukazitafakari ahadi hizi utabaini zimebeba neno UKWELI na kuacha neno UONGO. Si kwa TANU tu chama cha siasa, bali hata baadhi ya vyama vingine vya siasa, taasisi za dini, maabara ya sayansi, jamii adilifu na serikali sikivu na aminifu zimekubali ukweli na zimekataa uongo. 

Leo TANU haipo. Lakini falsafa zake zipo na zimejaa vichwani mwa watu (Watanzania). Mathalani fuatilia malumbano katika taasisi nilizotaja awali, utaona watu wenye tabia ya ukweli dhidi ya watu wenye tabia ya uongo. Ukweli umekubaliwa na uongo umekataliwa na Mwenyezi Mungu. 

Unapotoa ahadi maana yake unajipa sharti kulitimiza jambo. Ni kauli, ni agano kwako. Ahadi tatu hizi ni mapatano kati ya mtu na kusudio lake kutenda kwa watu. Watu wataamini na watakubali ahadi inapotimizwa au hawataamini isipotimizwa. Huo ndio ukweli na uhakika wa jambo. 

TANU ilijitahidi kuzuia uongo kutawala anga zake. Wenye tabia kama hii walitolewa au walijitoa wenyewe katika chama, kwa sababu uongo ni tabia ya kudanganya, kusema maneno yasiyo na ukweli. Wale waliosema ukweli walijenga na kuimarisha chama na sifa zake kusambaa duniani kote. 

Uongo ni kama pindo la nguo lenye matamvua: hupendeza, hukubalika na huzingatiwa na watu wasemaji na wasikilizaji. Uongo ni hadaa, vunga, laghai, ghalati, geresha na kadhalika. Mtu mwenye tabia ya uongo ni hatari sana, kwa sababu anavunja umoja wa watu, anafifisha maendeleo yaliyopatikana na anafifiliza mipango ya maendeleo yakusudiwayo. 

Mtu mwenye ukweli ana ahadi. Hutumia chake na muda wake kwa faida yake na wenzake. Huona faraja na kujaa furaha elimu yake inapotumika katika kutoa maarifa mbalimbali kwa watu. Haoni shida au tabu kutoa ufahamu na ujuzi wake kwa manufaa ya wote. Huu ndio ukweli. 

Kinywa cha mtu wa ahadi daima hujaa maneno ya ukweli, maneno ya kujenga heshima, upendo, umoja, utu na mshikamano. Fitina jamii ya uongo haina nafasi ndani ya nafsi na moyo wa mtu mkweli. Ukweli hauzai fitina ila uongo huzaa na kulea fitina. Hili ni tatizo duniani. 

Baadhi ya taasisi zetu za umma nchini, kwa maana katika michezo, haki, uchumi, usalama, kazi na huduma za jamii zimekumbwa na watu wenye tabia ya ukweli na tabia ya kudanganya. Wote wanazungumzia haki, usawa na amani. Ni juu yako kupima na kuona haki ya ukweli na haki ya kudanganya. 

Ukweli una uchungu na ladha ya ukakasi. Uongo una utamu na ladha ya sukari. Angalia watu wenye tabia ya ukweli wanavyosakamwa na maneno ya kuwavunja mioyo washindwe kutimiza malengo na kufikia mafanikio. Sikia maneno hadaa, laghai na uchuku yanavyowashambulia watu wa ahadi na ukweli.

Ukweli wenye uchungu na ukakasi ndiyo tiba, njia salama na kituo cha mafanikio. Uongo wenye utamu na sukari ndiyo sumu, njia ya ufu na kituo cha mauti. Watanzania naomba tuwe makini tunapowasikiliza wote wawili. Maelezo yao changanya na akili zako. Usihadaike na udogo na urembo wa mbayuwayu.

Maendeleo yanapoletwa katika jamii husika yanakumbana na changamoto za ukweli na za uongo. Miradi inapapaswa na kuhujumiwa. Ushoga ni laana lakini unatetewa na kusifiwa. Elimu na utaalamu unafutikwa mkobani na uzuzu unafurahiwa. Mambo kama haya hayana budi kukodolewa macho. 

Unapotafakari ukweli na uongo, kumbuka mawazo ya ukweli yana hofu halisi na yamezingirwa na hofu za kuchonga. Zitafute hofu zote mbili na zichambue upate majawabu. Mtanzania elewa tunahitaji Tanzania mpya ya viwanda na uchumi wa kati.

464 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!