Mombasa

Na Dukule Injeni

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC) imepitisha wagombea wanne miongoni mwa zaidi ya 50 walioomba kuwania urais kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, mwaka huu; ila ni wawili tu ndio wanapewa nafasi kubwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Wagombea hao ni Naibu Rais, William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, wakiwapiku kwa mbali David Wahiga na Profesa George Wajackoyah.

Mikutano mingi ya kampeni inayowahusisha Odinga na Ruto imekuwa ikikusanya umati mkubwa, hivyo wagombea hawa kutumia fursa hiyo kutoa ahadi za kuboresha maisha ya Wakenya, pia nini wanachotarajia kukifanya ndani ya siku 100.

Ruto wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) anawania urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza, mgombea mwenza wake akiwa Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua, wakati Odinga ambaye ni kinara wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) anasaka urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance, mgombea mwenza wake akiwa kinara wa Chama cha Narc Kenya, Martha Karua.

Kutokana na Odinga na Ruto wote kukimbilia wagombea wenza kutoka eneo la Mlima Kenya, lenye idadi kubwa ya wapiga kura, kinachoangaliwa kwa sasa ni sera na ahadi wanazozitoa kama zina mashiko na zinatekelezeka.

Kinachodhihirika wazi kwenye mikutano yao ya kampeni, wagombea hawa wawili wakuu wanakuja na sera na ahadi zinazowalenga watu maskini, wanawake, vijana, wafanyabiashara wadogo na ruzuku katika sekta za kilimo, viwanda na maeneo mengine makuu yanayochochea uchumi.

Ni ahadi tamu lakini changamoto wanashindwa kuelezea kwa kina namna gani watazitekeleza ahadi ambazo zitahitajika kutungiwa sheria na Bunge la Taifa na Bunge la Seneti. Aidha, kuna giza ni wapi watapata mabilioni ya fedha kuzifanya ahadi ziwe za kutekelezeka, ukizingatia bajeti ya taifa imebana.

Ruto ameahidi ndani ya siku 100 za kwanza akiwa ofisini, atatenga Sh bilioni 50 za Kenya kuunda ‘Mfuko wa Hustlers’, asilimia 50 ya Baraza la Mawaziri litajumuisha wanawake, atatekeleza theluthi mbili ya suala tata la usawa wa jinsia katika nafasi za uteuzi na kuchaguliwa na kuzuia tuhuma za watu ‘wasiopendwa’ kulengwa kwa ajili ya uchunguzi kisha kuhukumiwa kwa kesi za ufisadi.

Tafsiri ya neno ‘hustler’ kwa Ruto ni mtu anayepambana kufanikisha maishani, akijitolea mfano alivyotokea katika familia maskini na kupambana kuanzia ngazi ya chini hadi kuwa Naibu Rais na azima yake sasa ni kuwa Rais wa Tano wa Kenya.

Aidha, Ruto anaahidi kumtengea Naibu Rais wake na anayependekezwa kuwa Mkuu wa Waziri (cheo ambacho hakina tofauti na cha Waziri Mkuu) majukumu maalumu, kuunda taasisi ya haki za wanawake katika ofisi ya rais na kuondoa vikwazo kwenye bima ya afya.

Kwenye ahadi za Ruto imo kutenga fedha kwa kaunti zote 47 yenye lengo ya kukuza uchumi na kuteua majaji sita waliopendekezwa ambao Rais Kenyatta aliwakataa na kusababisha mvutano na Jaji Mkuu Martha Koome na aliyemrithi David Maraga.

Naye Odinga ndani ya siku 100 za kwanza ofisini ataongeza mgawo wa mwezi kwa familia maskini kutoka Sh 2,000 za Kenya hadi Sh 6,000 na kuhakikisha walimu wote ambao hawana kazi wanajumuishwa kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya serikali.

Aidha, atahakikisha huduma za afya ni kwa Wakenya wote, ameapa kudhibiti deni la taifa, kuboresha ulinzi, kupambana dhidi ya ufisadi, kuanzisha uchumi wa kidijiti, kuzisaidia biashara ndogo na za kati na kuanzisha utaratibu wa bima ya mifugo.

Ukizitazama na kuzisikia ahadi za Ruto na Odinga, zote zinavutia ila jukumu linabaki kwa mamilioni ya wapiga kura kung’amua ni ahadi za nani zinatekelezeka na zenye kuwapeleka ‘Nchi ya Ahadi’.

Katiba ya Kenya iliyopitishwa mwaka 2010 ilisisitiza theluthi mbili ya usawa wa jinsia katika nafasi za kuchaguliwa na uteuzi, jambo ambalo limekuwa pasua kichwa kwa wagombea urais japo Odinga ameonyesha mwanga kwa kumteua mgombea mwenza mwanamke, Martha Karua, huku Ruto akiahidi mambo mazuri kwa wanawake.

Wote kwa pamoja; Odinga na Ruto, wametoa ahadi ya kupunguza makali ya maisha muda mchache tu baada ya kuapishwa kwa kulenga zaidi kupunguza bei ya mafuta, unga na data za simu, ikiwamo kutanua elimu ya bure hadi sekondari na chuo kikuu.

Kwa kifupi, jukumu kubwa lililopo mbele ya Ruto na Odinga ni mapambano dhidi ya ufisadi, kuwawezesha wanawake na vijana, kufufua sekta ya afya na kuhakikisha utawala bora.

By Jamhuri