Mpita Njia (MN) anatanguliza salamu zake za Sikukuu ya Pasaka kwa Wakristo wote nchini ambao bila shaka wataungana na wenzao wa maeneo mengine duniani kwa ajili ya siku hiyo ya kiimani kwao.

Tukiachana na hayo, kama ilivyo kawaida yake, MN wiki hii alikuwa mkoani Tanga kwa ajili ya shughuli zake za ujenzi wa taifa. Loh! Tanga kuna mengi yaliyo mazuri, ingawa vilevile machache ya hapa na pale yenye kasoro hayawezi kukosekana.

Mpita Njia akiwa huko amebahatika kukatiza mitaa kadhaa ya Jiji la Tanga wakati wa pilikapilika zake hizo za ujenzi wa taifa, na eneo mojawapo ni Uwanja wa Mpira wa Mkwawani, maarufu Mkwakwani Stadium.

Mkwakwani Stadium ni uwanja wenye historia pana, na unapozungumzia soka, basi uwanja huo ni sehemu ya uhai wa timu zilizopata kuwika mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla, timu za Coastal Union FC na African Sports, na hata JKT Mgambo. Huu ni uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu (watazamaji) hadi 15,000.

Alichokibaini MN ni kwamba, Halmashauri ya Jiji la Tanga bado iko nyuma katika kuboresha mandhari ya jiji hilo lenye kaulimbiu ya kisasa ya ‘waja leo-kuondoka majaliwa’ ikichukua nafasi ya ile ya kale ‘waja leo waondoka leo’.

Mtazamo wa MN ni kuwa sehemu mojawapo ambayo ingeweza kubadili kwa haraka mandhari ya mji wa Tanga ni Uwanja wa Mkwawani. Hali ya sasa ya uwanja huu inasikitisha. Kuta ni chafu, vibanda vya wajasiriamali katika kuta za uwanja huu ni uchafuzi mwingine wa mandhari.

MN amejaribu kutafakari zaidi na kujiuliza, hawa wajasiriamali waliopanga kwenye maduka ya uwanja huu wanalipa kodi? Kama wanalipa kodi, kwa nini sehemu ya kodi hiyo isitumike kuboresha mandhari ya maeneo yao ya biashara? Inakuwaje uwanja wenye mapato, sehemu ya mapato hayo yanashindwa kutumika katika ununuzi wa taa za nje kuzunguka uwanja huo?

Kuna mambo mawili anayoamini MN yanaweza kufanyika. Kwanza, ukarabati wa uwanja huo mashuhuri nchini – kwa kuupaka rangi kiasi cha kubadili mwonekano wake wa uchakavu kama ilivyo sasa. Pili,  wapangaji wa ‘fremu’ zinazozunguka uwanja huo kupitia umoja wao (kama upo) wawe sasa wakali kudai mazingira safi kwa kuwa hata vyoo vilivyopo hali yake si nzuri. Haya yakifanyika bila shaka Tanga yenye maeneo mahiri kama Makorora, Chumbageni, Ngamiani, Tangamano, Mtaa wa Swahili, sambamba na mitaa ya 14, 15, 16, 17, 19, 20 na 21 itahamasika na kuwekwa katika hali ya kupendeza zaidi.

830 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!