Akwiline azidi ‘kumliza’ Waziri wa JPM

NA ANGELA KIWIA

Kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) cha jijini Dar es Salaam, Akwiline Akwilina kinaendelea ‘kutesa’ mioyo ya watu.

Akwiline aliuawa Februari 16, mwaka huu baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye daladala. Risasi hiyo inadaiwa kufyatuliwa na mmoja wa askari polisi waliokuwa wakiwatanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi katika chuo cha NIT jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni ni miongoni mwa wanaoguswa na kifo cha Akwiline, akisema kimeuumiza na kimekuwa mfano wa mwiba kwake.

Katika mahojiano na JAMHURI, Masauni aliyekuwa mmoja wa viongozi wa Serikali waliokwenda kuombeleza msiba huo, amesema hata alipokwenda kutoa pole kwa familia ya marehemu, kifo cha Akwiline kilibaki kuiumiza nafsi yake.

Masauni amesema siku ya kuuaga mwili wa Akwilina, alijitahidi kufika NIT ili  kutoa heshima za mwisho, lakini alikuwa katika wakati mgumu zaidi baada ya kuuona mwili wa mwanafunzi huyo ukiwa ndani ya jeneza.

“Nilipouona mwili wa Akwiline umelala kwenye jeneza, kidogo nilie lakini nilijizuia, nilipatwa na uchungu kuona binti mdogo, ndoto zake zimezimika na amelala kwenye jeneza. Nilikuwa na wakati mgumu sana, suala hilo binafsi linaniumiza mno,” amesema Masauni.

Alipoulizwa hatua zilizochukuliwa kwa askari wanaodaiwa kusababisha kifo cha binti huyo, amesema uchunguzi  unaendelea na utakapokamilika, wahusika watachukua hatua za kisheria.

“Siwezi kuongelea suala hili kwa sasa. Tuviache vyombo vya dola vitekeleze wajibu wake, tutapata majibu mapema na yenye uhakika. Uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa ya ripoti hiyo,” amesema.

UHAMIAJI HARAMU

Masauni amezungumzia pia kukithiri kwa wahamiaji haramu wanaokamatwa nchini, akisema hali hiyo haivumiliki.

Amesema wapo baadhi ya watumishi wa idara hiyo wanaojihusisha na biashara ya kuwaingiza wahamiaji haramu nchini na kuongeza, “haiwezekani idara nyeti kuwa na watumishi wa aina hiyo”.

Masauni amsema wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, imeandaa mkakati wa kudhibiti hujuma zinazofanyika kwenye mipaka ya nchi.

Amesema wizara inatafuta fedha za kutekeleza mkakati huo kutokana kwa wafadhili na kutumia rasilimali za ndani.

 “Mpaka wa nchi yetu ni mkubwa na upo wazi kiasi kwamba wapo baadhi ya watu wamefikia hatua ya kujenga ndani ya hifadhi, mfano ni kule Tunduma, Namanga na kwingineko,”amesema.

Hata hivyo Masauni amesema udhibiti wa mipaka hiyo si jambo rahisi kwa vile unahitaji rasilimali watu, fedha na vitendea kazi vya kisasa, lakini Serikali imejipanga ili kufanikisha azma hiyo.

UINGIZAJI SILAHA ZA KIVITA

Amesema baadhi ya wahamiaji wanaingia nchini na silaha za kivita zinazotumika kufanya uhalifu, hivyo kutanua wigo wa athari za uhamiaji haramu nchini.

Kwa mujibu wa Masauni, kuwepo kwa tishio la kigaidi kwenye nchi za jirani, kunaweka mazingira ya kutokea kwa hali hiyo nchini iwapo hatua za udhibiti hazitachukuliwa.

“Kuna wahamiaji haramu na wapitaji haramu. Tanga ni eneo tatizo lakini tumejiandaa kuwa na operesheni maalumu kwa mkoa huo ambao unaonekana ni sugu, tatizo si wahamiaji haramu tu, pia vitu haramu,” amesema.

Amesema idara ya Uhamiaji inahitaji kuwa na askari wenye weledi na wanaotumia teknolojia za kisasa hususani katika doria za mara kwa mara.

1042 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons