Na Deodatus Balile, Arusha

Wiki hii nimerejea katika ukumbi huu. Msomaji wangu niwie radhi sikuweza kuandika katika wiki mbili zilizopita, kwani nilikuwa na maandalizi mazito ya mkutano mzito ulioileta Afrika Tanzania. Huu si mwingine, bali ni mkutano wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD) uliofanyika Arusha, Tanzania.

Sitanii, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan. Siku hii Mei 3, 2022 imeadhimishwa siku iliyokuwa na ratiba ngumu mno kwa Rais. Ilikuwa ni siku ya Eid el Fitr, hivyo Rais alilazimika kuswali kwanza Swala ya Idd Dar es Salaam, baadaye akaja Arusha kufungua mkutano wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo kwa Afrika imeadhimishwa Tanzania na jioni akahudhuria Baraza la Eid Dar es Salaam.

Kwa hakika tumeiona faida ya usafiri wa uhakika, yaani matumizi ya ndege. Ingekuwa magari, nakuhakikishia Rais asingeweza kufanya ziara hizi zote akazikamilisha kwa wakati. Na hii niongezee. Ndiyo maana napingana na wanaomshutumu Waziri Nape Nnauye kwa kutumia helikopta katika kukamilisha mradi wa anwani za makazi.

Umefika wakati sasa viongozi wa kitaifa watumie helikopta au ndege. Kwa mawazo finyu tunaweza kudhani wanapata raha, si kweli. Fikiria kwa mfano Rais ana mkutano Kilimanjaro asubuhi, na jioni anapaswa kuwa Mpanda. Tukiwaza kwa ufinyu, litatolewa jibu la haraka kuwa haiwezekani, lakini tukitumia ndege na helikopta ni jambo la kawaida. Marekani wanafanya hivyo, na hata majirani zetu Kenya mawaziri wanatumia helikopta.

Ukimwambia mtu kuwa helikopta inapunguza gharama, utabishiwa. Lakini fikiria msafara wa magari, muda unaopotea barabarani na hatari za ajali zilizopo. Waziri Nape usife moyo, najua unashambuliwa kwa kutumia helikopta, lakini kila jambo lazima liwe na wa kulianzisha. Katika hili umeonyesha njia na si muda mrefu wengine watafuata. Mjadala huu una sura nyingi, wapo wanaolizwa na posho kwa kuwaza kuwa wakitumia magari idadi ya siku za safari inaongezeka, lakini kwao ufanisi na uchovu hawayafikirii.

Sitanii, nimeligusa la Nape baada ya kuona nchi inaacha mambo makubwa inajadili vitu visivyoongeza tija. Mama, Mheshimiwa Rais nakwambia sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau wa habari, umetupa heshima kubwa. Ungeweza kumtuma mwakilishi katika mkutano wetu na ugumu wa ratiba yako ungeeleweka kwa kila mtu.

Nikushukuru pia kwa kuwajulisha kuwa nilipowasiliana na wewe tukakubaliana usiahirishe ujio wako katika shughuli hii kwa kuwa maandalizi yalikwishakamilika, maana wapo waliokwishaanza kusambaza umbea kuwa nimewadanganya usingekuja. Ulipofika, aibu imewazingira kila kona. Asante sana Mhe. Rais kwa heshima kubwa uliyotupa wanahabari kwani ni mara ya kwanza mkutano huu kuhudhuriwa na Rais.

Sitanii, naamini pia wasaidizi wako wanapitia kwenye vyanzo vya habari. Utakubaliana na mimi kuwa mkutano huu umeitangaza Tanzania kwa uzuri nje ya nchi haijapata kutokea. Hotuba yako iliyogusa Bara la Afrika na kututaka waandishi kulijenga bara letu, imekuwa habari kubwa katika vyombo vya kimataifa. 

Tanzania imemwagiwa sifa kedekede. Wageni wa kimataifa waliotembelea mbunga zetu hadi kesho wanatamani kurudi tena Tanzania. Baadhi wameniambia watawashawishi marais wa nchi zao nao watengeneze Filamu ya Royal Tour kama uliyoitengeneza wewe.

Ujio wa Rais Samia kwenye Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Arusha umekuza heshima ya Tanzania kimataifa usipime. Mfano, ukitumia Google ukapekua maneno; “President Samia World Press Freedom Day 2022” kwenye mtandao, kuna habari 299,000 zinazomhusu Rais Samia na siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Ukiongeza neno Africa, zinakuja 242,500, ukiweka Tanzania, zinakuja 42,500. Hii ni kwa siku nne tu za mkutano, yaani Mei 1 hadi 4, 2022.

Sitanii, mkutano huu umenifundisha jambo. Ingawa tumefitiniwa na baadhi ya wenzetu wakati tunauandaa, ila uhalisia umelitangaza taifa letu. Rais Samia alifanya uamuzi sahihi kushiriki mkutano huu na wahariri kutoka Afrika katika nchi 54. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza. Natamani mikutano ya hivi tuiandae kila wakati. Nchi za wenzetu zilifanikiwa kupata majina makubwa kwa kuandaa mikutano kama hii. Asante sana Rais Samia, naamini hata mabadiliko ya sheria uliyoagiza, Mhe. Waziri Nape atayatekeleza kwa wakati. Mungu akubariki sana.

By Jamhuri