Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Awadhi Haji amewataka askari wote wa Usalama barabarani katika Mkoa wake kusimamia maadili ya kazi hiyo na kuonya juu ya askari wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya upokeaji rushwa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la JAMHURI, kwenye vituo vya daladala zinazotoa huduma maeneo ya pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam umebaini kuwepo kwa daladala zinazotoa huduma kwa kutoa rushwa kwa baadhi ya askari wa usalama barabarani.

Uchunguzi huo umebaini kuwepo kwa baadhi ya daladala ambazo hazikidhi vigezo vya kutoa huduma kwa abiria, lakini zimekuwa zikitoa huduma hiyo kwa kutoa rushwa kwa askari wenye jukumu la kuzikamata ama kuzizuia kuendelea kusafirisha abiria huku zikihatarisha maisha yao.
Vituo vilivyotembelewa na JAMHURI ni pamoja na Mbagala Rangitatu-Kingugi, Mbagala Rangitatu-Kilungule, Mombasa- KwaMkoremba, Gongo la Mboto-Viwege, Majohe-Gongo la Mboto-Pugu Mnadani na Kimara-Mpigi Magohe.
“Hapa tunaunga-unga tu, unajipanga tu mradi askari apate chake halafu unafanya kazi kibishi. Unahakikisha kila siku una kiasi kama cha elfu nne hivi kwa ajili ya askari si unajua wanavyotukomalia,” amesema Hamidu Ali, mmoja wa madereva.

Amesema kiwango hicho cha fedha ni kwa ajili ya kuwapoza askari wa zamu ambao husimama barabarani kuhakiki ubora wa magari na vigezo vya madereva.
Hamidu amekiri kuwa gari analoliendesha halikidhi vigezo ila anafanikiwa kuendelea na biashara hiyo kwa mtindo wa kutoa hongo kwa askari na kuruhusiwa kuendelea na kazi ya usafirishaji. Amesema kuwa hutumia takribani shilingi 80,000 kwa mwezi kupitia utaratibu huo.
“Lakini hawana roho mbaya kihivyo, siku zingine unaweza kuwaambia biashara mbaya askari wakakuelewa na ukitokea mambo yameenda vizuri unampoza,” amesema Hamidu.
JAMHURI limezungumza na Kamanda wa Usalama Brabarani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Awadhi kuhusiana na uwepo wa daladala zisizokidhi vigezo kuelekezwa maeneo ya pembezoni mwa jiji na kuendelea kutoa huduma kwa mgongo wa rushwa.

“Askari wenye tabia hizo hawatufai katika jeshi letu. Chombo kinapopoteza sifa ya kutoa huduma ni lazima kisiruhusiwe kuingia barabarani.
“Naomba kutumia fursa hii kuwaonya askari wenye tabia hiyo na kuwaomba wananchi kutoa taarifa ya vyombo vibovu vya usafiri, ambavyo wanahisi havistahili kutoa huduma hiyo,” amesema ACP Awadhi.
Kamanda Awadhi amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kutoa taarifa kwa maofisa wa jeshi hilo juu ya uwepo wa daladala zisizokidhi vigezo mahali popote walipo ili askari na wamiliki wa daladala hizo wachukuliwe hatua.
“Kwasababu baadhi ya askari wameshindwa kusimamia maadili ya kazi yao, nawaomba wananchi watupe taarifa ya vyombo hivi vibovu kwa usalama wa maisha yao. Wanaweza kuwasiliana na RTO Ilala kwa simu 0658 376476, RTO Temeke 0658376477 na 0658376478 kwa RTO Kinondoni,” amesema ACP Awadhi.

Kaimu Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mkoa wa Dar es Salaam, Beatrice Chao, amekili uwepo wa tatizo hilo na kwamba mamlaka hiyo imekuwa ikifanya operesheni za kushitukiza na kukamata magari yasiyokidhi vigezo.
“Tumekuwa tukifanya ukaguzi wa magari ya abiria lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba magari hayo yana leseni za Sumatra za usafirishaji na kuona kama wasafirishaji wanazingatia vigezo na masharti ya leseni hizo,” amesema Beatrice.

Mwanaisha Juma, Mkazi wa Kingugi jijini Dar es Salaam ameliambia JAMHURI, wanalazimika kupanda magari hayo kutokana na kutokuwepo kwa mbadala ya usafiri katika eneo analoishi.
“Tunapanda tu lakini muda wowote gari linaweza kuwaka moto likiwa na abiria ndani. Muda mwingine unashangaa tu gari limezima ghafla barabarani.
“Magari ni mabovu, machafu kiasi kwamba hata kunguni wamo kwenye magari haya,” amesema Mwanaisha.
Kiongozi wa Madereva wa Daladala katika kituo cha Kingugi, Antony Makombe, amesema daladala zote zilizopo katika kituo hicho zina ubora wa kuendelea kutoa huduma.
“Mimi sioni kama daladala hizi ni mbovu kama wanavyosema baadhi ya abiria kwa sababu zimefuata taratibu wote na trafiki wanajua. Baadhi ya hizi daladala zimekatiwa hadi bima usizione hivi.
“Mwenye uwezo wa kusema gari ni mbovu ni trafiki tu mbona hawasemi? Kama mtu anaona gari ni mbovu akapande bodaboda,” amesema Makombe.

3544 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!