BAADA YA YANGA KUKAZIWA NA MWADUI LEO NI ZAMU YA SIMBA DHIDI SINGIDA UNITED UWANJA UHURU

Wachezaji wa simba wakiwa mazoezini 

 

Kikosi cha Singida United Iktakachozeza na Simba Sc Leo
Kikosi cha Simba

Timu ya Yanga jana ilitoka sare ya kutokufunga na timu ya Mwadui, na  leo ni zamu ya Simba kukabiliana na timu Singida united kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
SIMBA ndiyo vinara wa Ligi Kuu Bara, lakini wanaweza kuwa ni wenye hofu zaidi wanapokutana na Singida United katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Simba kinakutana na Singida United kwa mara ya kwanza tokea ipande Ligi Kuu Bara na tayari Singida imekuwa ni timu tishio kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo.

Baada ya mechi 12 za ligi, tayari Singida United imeshinda saba, sare tano na imepoteza mechi moja tu. Hii inaifanya hadi sasa katika msimamo iwe katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 23.

Simba ambao ni vinara wao wamekusanya pointi 26, tofauti ya tatu tu dhidi ya Singida United na kama Singida watashinda maana yake watafikia idadi ya pointi za Simba na huenda hii ndiyo hofu kubwa zaidi waliyonayo watu wa Msimbazi.

Ubora wa Singida, uwezo wa Kocha Hans van Der Pluijm ambaye alikuwa akiisumbua Simba akiwa na Yanga pia kikosi cha Singida chenyewe, kinawafanya Simba kuwa na hofu zaidi na kulazimika kujipanga hasa.
Tayari Singida imeshinda mechi mbili za ugenini dhidi ya Stand United ikiwa Kambarage Shinyanga na dhidi ya Njombe Mji ambayo walishinda kwa mabao 3-1.

Simba wameshinda mechi nne, dhidi ya Stand, Ndanda, Mbeya City na Prisons lakini wao wataangalia zaidi matokeo yao ya nyumbani na katika mechi 12 wameshinda tatu tu wakiwa Dar es Salaam ambazo ni dhidi ya Ruvu Shooting, Mwadui na Njombe Mji.

Watakachoangalia Simba hapa ni sare nne nyingi walizopata Dar es Salaam ingawa dhidi ya Azam FC walicheza ugenini, sare nyingine ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga pia Lipuli FC.

Maana yake timu zenye presha dhidi yake kama Azam FC, Yanga na Mtibwa Sugar, Simba imeshindwa kuonyesha cheche na kushinda na badala yake imeambulia sare.
Mchezo dhidi ya Singida utaona ni presha inayofanana kwa kiasi fulani. Maana yake Simba wanapaswa kujipanga mapema na ikiwezekana watangulie kufunga.

Kama Simba wataruhusu kufungwa, presha itaangukia kwao mara mbili na kwa kocha kama Pluijm ni mjanja katika ulinzi na Singida wana uwezo wa kukaa na mpira muda mwingi, wanaweza kujilinda zaidi wakimiliki mpira, hii itakuwa nguvu zaidi kwa Simba.

Kama watatangulia kufunga na ikawa mapema, wakaimarisha ulinzi na kuanza kutafuta bao la pili, watapeleka presha hii Singida.
Kingine ambacho ni presha kwa Simba ni kutokana na Singida kuwa na wafungaji wasiofahamika. Maana hauwezi kujua nani ni hatari kati ya Michael Katsaivro, Tafadzwa Kutinyu, Deus Kaseke au Danny Usengimana huku wakiutumia zaidi upande wa beki Shafiq Batambuzi lakini bado upande wa kulia wa Michael Rusheshangoga ni hatari pia.

Pluijm anatumia presha kubwa kupitia walinzi wa pembeni na Kocha Masoud Djuma lazima apeleke presha nyingi pembeni kuwazuia mabeki hao wawili kuingia mara kwa mara kwenye eneo lake la hatari.

Singida ni hatari kwa mipira ya vichwa na hasa Usengimana, pia ni mchezaji mjanja anayeweza kuiwahi mipira mbele ya kipa au mabeki na hii itakuwa ni hofu nyingine ambayo Simba wanapaswa kuiziba na kuifanyia kazi mapema.

Katika mpira, lolote linaweza kutokea lakini hofu ya Simba ni kubwa zaidi kutokana na ukubwa wa timu na hali halisi ya sasa, kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho, kutimuliwa kwa kocha mkuu, mfumo mpya, kutolewa mapema Mapinduzi. Hivyo lazima wafanye kazi ya ziada.