Baadhi ya mila na desturi tunazozitupa zina manufaa kwa jamii

Jambo moja la msingi linalopambanua binadamu ni mila zao. Wanaweza kufanana kwa mwonekano, lakini utawatofautisha kwa mila na desturi zao.
Nimeyawaza hayo baada ya kusikia hivi karibuni taarifa kuwa, kwa mara ya kwanza, seneta mwanamke nchini Australia amekuwa mbunge wa kwanza katika historia ya nchi hiyo kumnyonyesha mwanae ndani ya Bunge wakati kikao cha Bunge kikiendelea.
Kwa maelezo yaliyotolewa, kanuni za Bunge la Senate la Australia zilibadilishwa ili kuruhusu wabunge kuingia na watoto wao wachanga ndani ya vikao, pamoja na kuwanyonyesha ikibidi kwa madhumuni ya kuwapa haki ya kuwapo ndani ya vikao bila pingamizi hiyo.
Ni kanuni ambayo bila shaka ipo kwenye mabunge mengi duniani, na si vigumu kuona namna gani mtoto mchanga anavyoweza kuvuruga majadiliano katika vikao vya aina hii.

Hata hivyo, inafahamika kuwa suala la kunyonyesha au kutonyonyesha hadharani ni suala ambalo linakubalika au kutokubalika kutokana na mila na desturi za maeneo mbalimbali duniani.
Ndiyo sababu naamini kuwa kubadilishwa kwa kanuni kuruhusu seneta mwanamke kunyonyesha ndani ya kikao cha seneti hakubadilishi mtazamo ndani ya jamii ambayo, kwao, utaratibu unaokubalika wa kunyonyesha mtoto, ni ule wa kufanyika kwenye faragha.
Ni baadhi yetu ambao tumekulia kwenye mila, desturi na tamaduni mseto ndiyo hujikuta kwenye mazingira ambapo misimamo juu ya tukio la aina hii inakinzana baina ya jamii moja na nyingine.
Leo hii nakiri hata mimi ninapojikuta mbele ya mama anayenyonyesha mtoto hadharani kichwani kwangu nahesabu kama tukio, ingawa kwa kawaida sitalizungumzia wazi au kuliandikia habari. Mahususi, kwangu linakuwa tukio ambalo linaibua ni jinsi gani jambo moja ndani ya jamii moja linaonekana la kawaida, na ndani ya jamii nyingine likaonekana siyo la kawaida.

Majuma kadhaa yaliyopita niliketi miongoni mwa kundi la wazee kwenye msiba kijijini Butiama, wakati alipofika binti mwenye mtoto mchanga akazunguka kutuamkia wote kisha akaketi chini akiendelea kuongea na mzee mmoja kwenye kundi lile la waombolezaji.
Alivyoketi tu mwanae alianza kulia na binti, bila kupoteza muda, akaanza kumnyonyesha mbele yetu, tukiwa wanaume pekee kama ishirini hivi.
Kwa mila na desturi zetu suala la mama kumnyonyesha mwanae hadharani halipaswi kuwa habari kwa kigezo chochote kile. Mtoto akililia chakula chake sehemu yoyote ile mama anafahamu kuwa wajibu wake ni kumpa mtoto anacholilia.
Lakini kama nilivyosema, kutokana na mwingiliano wa mila zetu na zile za nje, baadhi yetu tunabaini hitilafu kwenye matukio ambayo yanapaswa kuwa ya kawaida kabisa. Nina hakika kuwa ni mimi peke yangu kwenye kundi lile pale msibani kuona kuwa lilikuwa tukio la ajabu kidogo.

Nasisitiza kidogo, siyo sana. Wengine waliendelea na mazungumzo ya kawaida ya kwenye msiba bila hata kuona niliyoyaona mimi. Na si ajabu leo nikiuliza anayekumbuka yule binti kunyonyesha mbele yetu hatatokea anayekumbuka.
Nasisitiza kuwa ni tukio la ajabu kidogo kwa sababu nafahamu vyema mila na desturi zetu. Kidogo, kwa kuwa mimi, kama Watanzania wengi wengine tumekulia kwenye mkanganyiko wa mila zetu na zile ambazo tumezipokea kutoka kwa jamii nyingine.
Hatupo huku wale kule, tupo katikati. Na hata hapo katikati tulipo hatuna msimamo wowote madhubuti unaotubainisha kwa mila na desturi. Tunaweza kufananishwa na boya linaloelea kwenye maji na litaelekea mkondo au upepo unapolipeleka.
Na hii ndiyo inakuwa sababu ya kuwashangaa sana wale wanaoishi kwenye jamii ambapo mama analazimika kunyonyesha faragha, na kumshangaa kidogo binti ambaye alinyonyesha hadharani kwenye msiba. Ni tukio bado tunalishuhudia kijijini lakini ni tukio ambalo linaendelea kupotea kwenye maeneo yetu ya mijini.

Mshangao huu mdogo unaibua ukweli kuwa pamoja na kuzikubali baadhi ya mila na desturi zetu bado tunabeba athari ya mila na desturi nyingine na matokeo ni kutumbukia kwenye mikanganyiko ya kila aina.
Na mikanganyiko siyo midogo. Ingetokea nimpige picha yule binti aliyebaki kifua wazi mbele yetu na kuiweka kwenye mtandao bila shaka angetokea mwendesha mashitaka mmoja ambaye angetafakari kama nimekiuka Sheria ya Makosa ya Mtandao. Tunamkubali akikaa kifua wazi mbele yetu, lakini tukimuona kwenye Facebook tunaanza kushikana mashati.
Tunaambiwa kila wakati kuwa hakuna chakula bora zaidi kwa mtoto mchanga kuliko maziwa ya mama yake, lakini kutokana na karne na karne za kuambiwa kuwa hatuna mila na desturi za maana tumekuwa tunazionea aibu kiasi kwamba tumerithi mila na desturi, hasa kwa wale wanaoishi mijini, za kuwalisha watoto maziwa yanayotengenezwa viwandani na kupoteza faida kubwa za maziwa asilia ya mama.

Hii mifano michache ya kuiga visivyopaswa kuigwa ni sehemu ndogo tu ya mlolongo wa mila na desturi tunazopokea kutoka nje bila kutafakari athari zake kwa jamii.
Kubadilishwa kwa kanuni zilizompa nafasi seneta wa Australia kunyonyesha bungeni, zilihusiana zaidi na kupunguza pingamizi kwa wanawake kushiriki kwenye masuala ya uamuzi wanapohitajika kufanya hivyo, pamoja na kubeba majukumu yao ya kulea. Labda faida ya hii habari ambayo nilisema haifai kuwa habari ni kutuamsha walimwengu wengine kutafakari kwa kina ni desturi gani ambazo tuliziacha ambazo zina manufaa makubwa kwa jamii.

 

Na G. Madaraka Nyerere
Barua pepe: [email protected]
Twitter: @MadarakaN
Simu: 0777209546