Ng’ombe hazeeki maini, Waswahili ndivyo wanavyosema. Kazuyoshi Miura, ndiye anayetajwa kuwa mchezaji wa soka mwenye umri mkubwa zaidi duniani.

Inaelezwa kuwa licha ya kuwa na umri wa miaka 52, bado anasakata kabumbu katika timu ya Yokohama inayoshiriki Ligi Kuu nchini Japan. Miura pia anafahamika kwa jina la ‘King Kazu’, kutokana na kucheza miondoko ya ‘kazu’ pindi anapofunga magoli.

Miura ni mzaliwa wa Shizuoka, Japan. Alizaliwa mwaka 1967, baba yake ni Naya Nobuo, mama yake, Yoshiko Miura na mkewe anaitwa Risako Miura. Kaka yake anaitwa Yasutoshi Miura.

Miura alianza kucheza soka mwaka 1973 akiwa na umri wa miaka saba katika timu ya watoto ya  Jonai nchini Japan. Baadaye alijiunga na timu ya vijana ya Jonai Jr, mwaka 1979 hadi 1982. Baada ya hapo, alijiunga na timu ya shule ya Shizuoka Gakuen, ambayo aliichezea hadi mwaka 1986 na kujiunga na timu ya Brazil, inayoitwa Juventus – SP.

Amezunguka sehemu nyingi duniani katika kusakata kabumbu la kulipwa, akiweka rekodi ya kuzichezea klabu mbalimbali nchini Brazil ambako kuanzia mwaka 1981 mpaka 1990 alikuwa anachezea klabu za CRB, Santos na Coritiba nchini humo.

Miura hakuishia hapo, alichanja mbuga hadi katika klabu za Ulaya, ambako amewahi kutumikia klabu nyingi kama Genoa ya Italia, Zagreb ya Crotia na timu ya Sydney ya nchini Austalia.

Wengi tunafahamu namna ambavyo si rahisi kwa wachezaji wa mpira wa miguu kucheza soka la ushindani wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 50, lakini kwa mchezaji huyu hilo limewezekana. Katika ulimwengu wa soka, imekuwa ni kawaida kwa wachezaji wengi pindi wanapofikia umri wa miaka 30 uwezo wao wa kupambana ndani ya uwanja hupungua kwa kiasi fulani.

Watu wengi tumekuwa tukiamini wachezaji wenye umri kuanzia miaka 18 mpaka 29 ndio huwa na uwezo wa kupambana na ikifika miaka 35, wachezaji wengi hutundika daruga.

Uzoefu unaonyesha kuwa wenye fursa pana zaidi ya kucheza soka la kulipwa katika umri mkubwa ni magolikipa, hawa wanatajwa kuweza kuhimili mikiki ya ligi za ushindani. Kwa mfano, golikipa wa timu ya Taifa ya Misri, Essam El Hadary (45), alitajwa kuwa ni mchezaji mwenye umri mkubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2018 nchini Urusi, lakini katika nafasi ya mshambuliaji kucheza akiwa na miaka 45 mpaka 50 ni vigumu sana katika soka la ushindani.

Katika timu anayochezea Miura, timu ya Yokohama, Kocha wa klabu hiyo, Edson Traves, ana umri wa miaka 62 na utaona kuwa mchezaji huyo wamepishana miaka 10 na kocha wake, kwa hiyo tunaweza kusema kocha na mchezaji ni sawa na mtu na mdogo wake.

Miura bado anakuwa miongoni mwa wachezaji wa Japan mwenye mafanikio makubwa katika klabu alizochezea, lakini mafanikio makubwa ameyapata katika timu ya Verdy Kawasaki na katika mechi 192 alizocheza, ameifungia timu ya Kawasaki magoli 100 mwaka 1994, akiisaidia timu hiyo kutwaa taji mwaka 1996.

Aliandika historia ya kuwa Mjapani wa kwanza kuwa  mchezaji bora wa Ligi ya Italia. Vilevile amekwishawahi kutwaa ubingwa akiwa na timu ya Dinamo Zagreb ya nchini Croatia katika msimu wa 1998\1999.

Miura ni mchezaji pekee ambaye amefunga goli akiwa na miaka 50. Mwaka 1992 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Bara la Asia.

Aidha, Miura aliisaidia kuipandisha daraja timu yake ya Yokohama hadi Ligi Kuu ya Japan, baada ya kutwaa taji la ligi daraja la kwanza katika msimu wa 2005/2006.

750 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!