Balozi za Tanzania aibu tupu

 

*Baadhi hawajalipwa mishahara miezi sita, zimeajiri Wakenya

*Ufaransa pango Sh milioni 720, wanatumia anwani ya Uganda

*Ofisi zinaporomoka, Kikwete asema Richmond imeiponza nchi

*Membe alia Serikali kukata bajeti yake ikabaki asilimia 44 tu

 

Sura na heshima ya Tanzania nje ya nchi inashuka kwa kasi kubwa, kutokana na Serikali kuzitelekeza balozi zake nje ya nchi.

Yapo mambo mengi ya aibu yanayowakumba mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, kwani baadhi ya balozi zinashindwa kulipia huduma ya simu, maji, umeme na baadhi ya magari yanazimika na kuwashwa kwa kusukumwa kama ya uswahilini. Taarifa ya ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyotembelea balozi mbalimbali imeibua uozo wa ajabu.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati anafanya majumuisho ya bajeti yake, alieleza kwa masikitiko makubwa tatizo linalozikabilia balozi hizo na kuifanya sura ya Tanzania kuingia doa katika jamii ya kimataifa, ila akalia na kiwango cha bajeti kinachoifikia wizara yake.

 

Mishahara ya mabalozi kuchelewa

Taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa baadhi ya balozi za Tanzania nje ya nchi, watumishi na mabalozi wanaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu. “Hadi wajumbe wanafanya ziara katika Ubalozi huu [Stockholm, Sweden], watumishi wa Serikali walikuwa wamepata mishahara yao hadi kufikia Machi na hawakuwa wamepata mishahara ya miezi mitatu wakati wajumbe wa Kamati wanaondoka Stockholm tarehe 29 Juni, 2012,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

 

Tatizo la mishahara lipo katika balozi mbalimbali, na baadhi ya balozi kama Msumbiji wafanyakazi wamefikia uamuzi kuwa walipwe mishahara yao kupitia akaunti za benki zilizopo hapa nchini Tanzania, hali inayowanusuru kwani kwa njia hii wanapata mishahara kwa wakati sawa na watumishi wa Serikali waliopo hapa nchini. Katika eneo hili, vibarua wanaotumikia balozi za Tanzania katika sehemu mbalimbali duniani zilipo ofisi za balozi za Tanzania, wanadai malipo kwa muda mrefu na kupata usumbufu.

 

Kamati inapendekeza pia kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya balozi hizi, badala ya kupelekwa kwanza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kisha ndipo zitumwe kwenye balozi husika, utaratibu ubadilishwe, Hazina itume fedha hizo moja kwa moja kwenye balozi kama ilivyo kwa halmashauri za miji na manispaa hapa nchini.

 

Kodi ya pango, anwani ya Uganda

Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa unakabiliwa na changamoto nyingi ajabu. Tanzania haina jengo pale Ufaransa, hivyo inapangishwa katika jengo linalomilikiwa na Serikali ya Uganda, lakini pia kuna aibu ya ziada.

“Hakuna jengo la Serikali kwa ajili ya ofisi na nyumba za watumishi, hivyo umepangishwa (ubalozi) na Uganda pamoja na kutumia sanduku la posta la Uganda. Hata mkalimani anayetumika ni Mkenya,” inasema taarifa hiyo iliyosainiwa na Makamu Mwenyekiti, Mussa Zungu.

 

Baada ya kuona shida wanayopata watumishi wa Ubalozi wa Tanzania, New Zealand iliamua kuiuzia Tanzania jengo inalolimiliki nchini Ufaransa kwa bei nafuu, lakini Serikali ya Tanzania haijatoa jibu iwapo italinunua jengo hilo au la na ifikapo mwezi ujao wa Septemba, ofa hiyo itafutika. “Ubalozi umekuwa ukiathirika na gharama kubwa unayotumia kwa ajili ya kodi ya kupanga ofisi na nyumba sita za watumishi. Hali hii huugharimu ubalozi kiasi cha euro 31,435.40 (Tshs 59,727,260) kwa mwezi ambazo ni sawa na Th 716,727,120 kwa mwaka na ni asilimia 34 ya bajeti ya ubalozi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

 

Tatizo la kupanga na kulipa gharama kubwa ya pango liko katika balozi nyingi za Tanzania, hivyo Kamati imependekeza kuwa Serikali iziruhusu balozi kununua majengo kwa utaratibu wa kuweka mali rehani (mortgage financing), ili kiasi kinachotumika kulipa pango kwa sasa kitumike kulipia nyumba zilizonunuliwa baada ya muda ziwe mali ya Tanzania.

 

Majengo yana hali mbaya

Majengo mengi ya Balozi za Tanzania nje ya nchi yamechakaa kwa kiwango cha kutisha. Mapaa yanavuja, mifumo ya umeme haifanyi kazi, na baadhi ya majirani wanalalamika kuwa uchakavu wa majengo ya Tanzania unapunguza thamani ya nyumba zilizo jirani na majengo hayo katika miji mbalimbali.

 

Ottawa, Canada

Hapa kuna tatizo la uwakilishi mpana, Kamati imependekeza kuwa ufunguliwe ubalozi nchini Cuba badala ya kutegemea Ubalozi wa Canada.

 

Pia kuna tatizo la Watanzania wanaofanya kazi ubalozini kulipishwa kodi, ila hii imetokana na Tanzania kuwalipisha kodi watumishi wa Ubalozi wa Canada waliko Tanzania, hivyo nchi hiyo inasema mabalozi wao nao wakiacha kulipishwa kodi nao wataacha kuwalipisha kodi watumishi wa Ubalozi wa Tanzania.

 

Washington, Marekani

Jengo Na 2139 R Street, NW Washington DC, linalomilikiwa na Serikali jijini Washington, limeendelea kuchakaa kwa Serikali kutotoa ruhusa likarabatiwe.

 

Hadi sasa wamejitokeza wapangaji wenye nia ya kupanga katika jengo hilo ambao wangelipa wastani wa kodi ya dola 400,000 kwa mwaka, karibu Sh milioni 600 za Tanzania, lakini kwa mwaka mzima sasa Serikali imeshindwa kutoa uamuzi wa kuwakubalia wapange jengo hili linaloendelea kuoza.

 

Pia ubalozi huu una kashfa ya kuajiri Watanzania ‘waliojilipua’ nchini Marekani kama watumishi wenyeji. “Kuna watumishi wenyeji (local based) ambao ni Watanzania waliozamia nchini humo [Marekani] kitu ambacho ni kinyume cha sheria,” inasema taarifa hiyo.

 

New York, Marekani

Kwenye ubalozi huu kuna tatizo la kukosa ruhusa ya kutumia maduhuli wanayokusanya. Nyumba ya Balozi wa Tanzania UN 30 Overhill Road, Mount Venon, ina hali mbaya kiasi kwamba haikaliki. Kamati imeshauri ikarabatiwe haraka.

 

Kamati imeishauri Serikali kununua nyumba ambayo kwa sasa Ubalozi wa Tanzania unapanga inayouzwa Na. 86 Judson Avenue, Dobbs Ferry, New York. Kwa kuwa katika Umoja wa Mataifa kuna masuala mengi, Kamati imependekeza kila wizara hapa nchini iwe na dawati la Umoja wa Mataifa litakalosaidia kuratibu shughuli za umoja huo.

 

Beijing, China

Katika ubalozi huu kuna tatizo sawa na balozi nyingine wakati jengo la ubalozi limechakaa sehemu kubwa inavuja na lina nyufa. Pia sheria ya China inataka gari liendeshwe si zaidi ya miaka 10, lakini ubalozi unatumia gari lililonunuliwa mwaka 2001 hivyo Tanzania inavunja sheria kwa balozi kuendesha gari chakavu.

 

Pamoja na umuhimu wa pekee ilionao China katika uchumi wa dunia ya sasa, hadi leo hakuna Mtanzania mtaalamu wa masuala ya uchumi anayefanya kazi katika ubalozi huu. Kamati inapendekeza mtu huyu ateuliwe haraka.

 

Kamati pia inashauri kutokana na China kuwa na fursa nyingi za kiuchumi, Balozi wa Tanzania nchini China awe na wasaidizi wawili huku ikipendekeza uanzishwe Ubalozi Mdogo katika mji wa viwanda wa Guang-zhou.

 

China pia imeipa Tanzania fursa ya kulipia ada wanafunzi 100 ikiwa Tanzania itaamua kusomesha idadi kama hiyo. Kamati imeishauri Bodi ya Mikopo kutumia fursa hiyo kwa kupeleka Watanzania masomoni China (scholarships).

 

Tokyo, Japan

Ubalozi huu una uhaba wa magari na watumishi. Lakini pia wana tatizo la msingi: “Ubalozi unapoomba taarifa na ufafanuzi wa masuala muhimu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hukosa taarifa hizo au kupata kwa kuchelewa,” inasema taarifa ya kamati. Hili ni tatizo sugu kwa balozi karibu zote.

 

Pia kuna tatizo kuwa asasi za kiraia za Japan zilitoa msaada wa kompyuta 1,000 kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na magari ya wagonjwa kwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, isipokuwa Serikali hadi sasa haijarudisha ‘export certificate’ kuonyesha kuwa msaada huo uliwafikia walengwa, hali inayowatia shaka Wajapani kudhani kuwa labda uliyeyukia njiani. Kamati imeona fursa na inapendekeza Tanzania ianze mara moja mkakati wa biashara na nchi hii.

 

Kuala Lumpur, Malaysia

Ubalozi umeshindwa kulipa ankara za umeme, maji, gesi, simu na matibabu hadi kufikia hatua ya kukatiwa huduma hizo. Maafisa wa ubalozi wameanza kujilipia ankara hizo bila kurejeshewa.

 

Pia katika kile kinachoonyesha kuwa aibu kwa taifa, ubalozi umeshindwa kulipa deni la kampuni ya ulinzi hadi ukaandikiwa barua na wakili wa kampuni hiyo inayotaka kuushitaki ubalozi mahakamani kwa kulimbikiza deni.

 

New Delhi, India

Mbali na hati za utambulisho kwa nchi ambazo Balozi wa Tanzania nchini India analiwakilisha taifa, kuna tatizo la mawasiliano duni kati ya Ubalozi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

 

Majengo ya kisasa ya ubalozi yaliyoanza kutumika mwaka 2007 hadi sasa hayajatengewa fedha kwa ajili ya kuyafanyia ukarabati kwa miaka mitatu mfulululizo. Kamati imependekeza ubalozi uwezeshwe kifedha.

 

London, Uingereza

Mbali na kucheleweshwa kwa kibali cha kutumia fedha zinazotokana na mauzo ya viza, ubalozi una kiwanja Na. 19 Denewood Road, N64AQ kilichotelekezwa katikati ya Jiji la London.

 

“Sasa hivi Serikali ya Uingereza inaweza kukichukua kiwanja hicho, kwani kinahatarisha usalama wa wananchi wa eneo husika kwa jumla,” inasema taarifa hiyo.

 

Pia Serikali imetakiwa kufanyia matengenezo nyumba Na. 6 Colindeep Gardens, NW4 4RU ambayo nayo imetelekezwa kwa sasa haitumiki kabisa.

 

Kikwete akutana na Kamati London

Kamati hiyo Julai 12, 2012 chini ya Mwenyekiti wake, Edward Lowassa, ilikutana na Rais Jakaya Kikwete jijini London, baada ya Kamati kumweleza Rais Kikwete matatizo ya fedha na mengine yanayozikabili balozi za Tanzania nje ya nchi, hali inayoshusha heshima ya nchi, Rais Kikwete alisikitika ila kwa mujibu wa ripoti maalumu ya Kamati iliyowasilishwa bungeni, akasema:

 

“Alikubaliana na maoni ya Kamati kuhusiana na tatizo la urasimu wa uendeshaji wa kazi za Serikali linalosababisha kutotoa uamuzi kwa wakati, jambo linalotokana na hofu ya  watendaji wa Serikali baada ya viongozi na maafisa mbalimbali kuwajibishwa katika kadhia ya Richmond,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

 

Mbali na kuipongeza Kamati, Rais Kikwete alitoa msimamo wa Tanzania juu ya suala la Sahara Magharibi inayokaliwa na Morocco, akisema wananchi wanapaswa kuamua wenyewe hatima yao kwa njia ya amani itakayoongozwa na mazungumzo.

 

Berlin, Ujeruman

Mwakani meli ya mv Liemba inayofanya kazi katika Ziwa Tanganyika inatimiza miaka 100. Ujerumani imejitolea kuikarabati, lakini haipati mwitikio wowote kutoka Tanzania, hali inayowakatisha tamaa kuwa huenda Tanzania haihitaji msaada huo.

La kushangaza hata kiwanda cha saruji cha Wazo Hill kimejitolea kutoa msaada wa euro milioni 2.5 kwa ajili ya ukarabati wa meli hiyo, lakini Serikali imeukataa msaada huu.

 

Moscow, Urusi

Ofisi na nyumba ya Balozi wa Tanzania vipo katika jengo la Serikali ya Urusi lililojengwa mwaka 1886. Tanzania ilianza kutumia jengo hili mwaka 1964 na hadi leo halijawahi kufanyiwa ukarabati. Ubalozi unadaiwa deni kubwa la pango katika jengo hili.

 

“Kwa sababu hiyo hali ya jengo ni mbaya sana kiasi kwamba ilitokea katika Ofisi ya Ubalozi, udongo wa dari (concrete) wenye uzito wa nusu tani ulianguka ofisini kwa balozi na kuacha nondo zote zikiwa wazi,” inasema taarifa hii.

Pendekezo la ubalozi ni kununua jengo lililopo jirani na ubalozi lenye ghorofa sita kwa wastani wa dola milioni 10 (sh bilioni 16), ambalo wao watatumia ghorofa mbili na nyingine kupangishwa.

 

Maoni ya jumla

Kamati imependekeza Serikali ianzishe chombo maalumu kitakachoshughulikia uamuzi wa kukarabati na kununua majengo kwa ajili ya balozi za Tanzania nje ya nchi.

 

Pia badala ya Serikali kutoa fedha kununua majengo, Kamati inapendekeza utumike utaratibu wa kuweka rehani majengo yanayokusudiwa kununuliwa kisha yapangishwe na kuzalisha fedha, huku fedha zilizokuwa zikitolewa kama pango zikitumika kulipia mikopo hiyo (mortgage financing).

 

Wanapendekeza wizara hii ipewe fedha za kutosha na ikama ya watumishi ikamilishwe kwa nia ya kutekeleza vyema Sera ya Diplomasia ya Uchumi iliyoanza kutumika tangu mwaka 2004.

 

Membe aeleza masikitiko

Membe alisema katika bajeti anayoomba kwa mwaka anaishia kupata asilimia 44 na tatizo limezidi kuwa kubwa baada ya Serikali kubadili utaratibu wa kutoza viza za kuingia nchini. Wageni wanalipa viza wakiwa kwenye viwanja vya ndege vya hapa nchini, hivyo kuzikosesha balozi mapato.

 

“Suala hili si tu linazikosesha balozi zetu mapato, bali pia ni hatari kwa usalama wa nchi yetu. Wageni wanapewa viza baada ya kuwa wameingia nchini. Hii ni hatari,” Membe aliliambia Bunge.

 

Kuhusu upungufu wa bajeti, Membe aliliambia Bunge: “Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kupata mgawo kidogo sana wa bajeti isiyokidhi mahitaji katika mwaka wa fedha 2011/2012. Katika kipindi tajwa, Wizara yangu ilipata asilimia 44 tu ya Bajeti iliyoombwa.  Bajeti ndogo tunayopewa imekuwa changamoto kubwa katika kutekeleza  Diplomasia ya Uchumi kwa kiwango kinachostahiki.”

 

Wakati Membe akionyesha masikitiko kwa kupewa bajeti kiduchu na kubadilishwa kwa utaratibu wa kutoa viza, hali inayozikosesha mapato balozi, Ripoti ya Bunge ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inaisukumia Serikali mzigo wa kushindwa kufanya uamuzi kupitia Wizara ya Membe, hali inayodumaza juhudi za watumishi na mabalozi.

 

1082 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons