Ujenzi wa gati ya Bandari ya Magarini ukiendelea katika Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera.

Katika makala hii tutaangazia miradi inayotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa bandari zinazosimamiwa na Bandari ya Mwanza ndani ya Ziwa Victoria.

Katika Ziwa Victoria, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inamiliki na kusimamia bandari kubwa za Mwanza Kaskazini, Mwanza Kusini, Nansio, Kemondo Bay, Bukoba na Musoma.

Pia kuna bandari nyingine ndogo ndogo (Cluster Ports) ambazo ziko katika mwambao wa ziwa hilo. Bandari hizo ni pamoja na Maisome, Kome, Bukondo, Kahunda, Nkome, Miharaba, Buchesi, Solima na Karumo, Ntama, Kanyala/Lushamba (Mkoa wa Mwanza); Chato na Nyamirembe (Mkoa wa Geita); Kyamkwikwi na Magarini (Mkoa wa Kagera) na Shirati na Kinesi (Mkoa wa Mara). 

Bandari hizi zimekuwa kiunganishi muhimu kati ya Bandari ya Mwanza na Bandari Kuu ya Dar es Salaam. Bandari ya Mwanza na bandari zake zina uwezo wa kuhudumia wastani wa tani za mizigo 1,000,000 (milioni moja) kwa mwaka pamoja na abiria 1,000,000 (milioni moja) kwa mwaka.

Aidha, Bandari ya Mwanza ina umuhimu sana kwa maendeleo ya nchi na kwa watumiaji wa bandari. Bandari ya Mwanza ni kiungo muhimu cha kiuchumi na biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, nchi za Afrika Mashariki na maeneo jirani.

Bandari zinarahisisha huduma za kijamii kama vile usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka na kwenda sehemu mbalimbali, vikiwemo visiwa vilivyomo Ziwa Victoria kama vile Ukerewe na Goziba.

Kupitia shughuli za kibandari ambazo kimsingi ni huduma na biashara, nchi inajipatia mapato na wananchi kupata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Jamii pia inafaidika kwa kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na bandari kwa dhana/sera ya uwajibikaji kwa jamii (CSR); mfano utoaji wa madawati kwa shule na uchimbaji visima vya maji.

Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TPA imeamua kuwekeza kwenye miradi ya kuzijengea uwezo bandari hizo ili ziweze kuwa chachu ya maendeleo na kiungo muhimu cha uchumi na biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine. 

Miradi ya TPA inayotekelezwa katika Ziwa Victoria ni pamoja na ujenzi wa gati  ya Bandari ya Ntama iliyopo wilayani Sengerema katika Halmshauri ya Buchosa mkoani Mwanza. Mradi huu kwa sasa umefikia katika hatua za kumalizia jengo la abiria, vyoo na mnara wa tenki la maji.

Mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Sengerema, Halmashauri ya Buchosa ni ujenzi wa gati katika Bandari ya Lushamba, jengo la abiria,  jengo la mizigo, uzio, vyoo, mnara wa tenki la maji pamoja na ujenzi wa chumba cha mashine ya umeme. 

Kwa upande wa Wilaya ya Musoma katika Mkoa wa Mara, Mamlaka ya Usimamzi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshakamilisha tayari ujenzi wa gati katika Bandari ndogo ya Mwigobero kwa ajili kutoa huduma bora kwa abiria na mizigo. 

Mradi mwingine ambao TPA inautekeleza ni ujenzi wa gati katika Bandari ya Nyamirembe iliyopo wilayani ya Chato, Mkoa wa Geita. Pamoja na ujenzi wa gati hilo pia kuna ujenzi wa jengo la abiria,  jengo la mizigo, uzio, vyoo, mnara wa tenki la maji pamoja na ujenzi wa chumba cha mashine ya umeme na chumba cha walinzi. Itakumbukwa kwamba Bandari hii ya Nyamirembe ilikuwa bandari maarufu tangu enzi za ukoloni. 

Bandari hii ya Nyamirembe itakapokamilika itakuwa ni kiunganishi muhimu kwa mizigo ya Burundi na Rwanda, kwani ni jirani sana. Pia bandari hii itawawezesha watalii kwenda visiwani, ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo. 

Pamoja na miradi hiyo, pia TPA inatekeleza ujenzi wa Gati la Bandari ya Magarini katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Kama ilivyo kwa bandari nyingine katika Bandari hii ya Magarini pia kuna ujenzi wa jengo la abiria,  jengo la mizigo, vyoo, mnara wa tenki la maji pamoja na ujenzi wa chumba cha mashine ya umeme na chumba cha walinzi. 

Bandari ya Kemondo Bay mkoani Kagera kuna ukarabati wa majengo ya abiria na mizigo, ukarabati wa daraja la mabehewa ya treni (Link Span) na gati. Bandari hii maarufu ambayo ilijengwa mwaka 1971 – 1973 ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya meli za mizigo kwenda na kutoka nchi jirani za Uganda na Burundi pamoja na Mkoa wa Kagera na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa. 

Kwa upande wa Bandari ya Bukoba ambayo ilijengwa mwaka 1945, TPA inatekeleza miradi ya ukarabati wa ofisi na jengo la abiria, ujenzi wa jengo la abiria kwa ajili ya boti za kwenda visiwa vya Kerebe, Goziba na Makwiba. Pia katika Bandari hii ya Bukoba, TPA inatekeleza mradi wa kukarabati maghala ya kutunzia mizigo, lengo likiwa ni kuboresha huduma kwa abiria na mizigo ya wateja. 

Aidha, mradi mwingine unaotekelezwa na TPA ni mradi wa Bandari Kavu ya Fela wilayani Misungwi katika Mkoa wa Mwanza. Eneo lililotwaliwa lina ukubwa wa ekari 1,178.69 na wahusika walishalipwa tayari fidia. Eneo hilo tayari limetangazwa kumpata mzabuni mshauri kwa ajili ya upangaji wa matumizi ya eneo hilo kibandari.

Lengo la bandari kavu hiyo ni kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa Uganda  wasisumbuke kwenda hadi Bandari ya Dar es Salaam, badala yake mizigo yao wawe wanaichukulia Mwanza ikiwa ni njia rahisi na nafuu ya kusafirisha mizigo yao, hivyo kuifanya Bandari ya Mwanza kuwa kiunganishi cha uhakika katika ukanda wa maziwa makuu na nchi jirani.

Utekelezaji wa miradi hii unaonyesha jinsi gani Serikali ya Awamu ya Tano kupitia TPA inavyotelekeza ahadi zake za kuboresha maisha ya wananchi wake kuwapeleka katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda. Bandari hizi ni daraja muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda katika kusafirisha mali ghafi na bidhaa ambazo tayari zimeshatengenezwa.

217 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!