Lango kuu la biashara za SADC

 

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na nyinginezo nchini Tanzania ni lango kuu la biashara kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji na Zimbabwe.

Bandari hizi zilijengwa kabla ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, na zimekuwa zikifanyiwa maboresho katika kutoka huduma, hususan Bandari ya Dar es Salaam na Mtwara – kuzifanya kuwa bandari bora kabisa Afrika. Mageuzi makubwa katika bandari hizi yanafanyika zaidi katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, anasema maboresho yanayofanywa ni pamoja na kupanua bandari zote nchini na kuimarisha huduma, hivyo kupunguza siku za mzigo kukaa bandarini na kuimarisha ulinzi na usalama wa wateja na mizigo yao.

Kwa mfano, Kakoko anasema katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni kwamba gati linalojengwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya magari lina uwezo wa kukaa magari 10,000 kwa wakati mmoja.

Anasema magati ya zamani, hususan gati Na. 1 na Na. 7 katika Bandari mashuhuri ya Dar es Salaam kwa eneo hili la Afrika yanaimarishwa kuweza kuhudumia mizigo mingi zaidi.

Anasema bandari pia inapanua lango ambalo meli zinaingilia kutoka wastani wa mita 150 za sasa kwenda mita 170, huku kina cha sasa kilichoko cha mita kati ya 10.5 hadi mita 11 kikiongezwa kufikia mita 15.5.

 

Usalama madhubuti

Kuhusu usalama, Mhandisi Kakoko anasema ulinzi na usalama umeimarishwa kiasi cha kutosha katika Bandari ya Dar es Salaam na nyinginezo nchini, kiasi kwamba kwa sasa ‘hata sindano ikidondoka chini’ bandarini inaonekana.

Anasema ulinzi na usalama wa mali za wateja kwa sasa hauishii kwenye bandari pekee, bali hata nje ya bandari, ikiwa ni pamoja na kwenye bandari kavu.

Anasema wanaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi kwenye barabara zote, mfano kutoka Dar hadi Tunduma, barabara ya kwenda Isaka hadi Rwanda, kwenda mpaka Mutukula, kuingia Rusumo, kwenda mpaka Kabanga, kwenda hadi Namanga na kadhalika kuhakikisha wanaondoa kabisa wizi unaoweza kutokea barabarani.

Anasema katika suala hilo hilo la usalama, wanashirikiana vizuri na Jeshi la Majini (Navy) kiasi kwamba matatizo kama ya kuvamiwa kwenye meli hayapo tena.

TPA inawahakikishia wateja wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam kwamba si tu kwamba mizigo yao iko salama muda wote, bali bandari inahakikisha pia inakuwa salama kwa walaji au watumiaji wanaolengwa.

Bandari ina mifumo na usimamizi mzuri wa ukaguzi na ulinzi wa mizigo inayoingia kutoka nje au kupita kwenda nchi jirani na inayopitia bandarini kwenda nje ya nchi katika kuhakikisha usalama wake na usalama wa walaji.

Kwa sasa haiwezakani kifaa chochote cha gari kupotelea katika Bandari ya Dar es Salaam. Kimsingi gari hukaguliwa mara tatu linapofika bandarini. Mara ya kwanza anasema ni ukaguzi ndani ya meli, ukaguzi nje ya meli baada ya gari kushuka na ukaguzi wakati gari linapochukuliwa na mteja kwenye yadi.

Ufanisi na gharama nafuu

Kwa sasa utoaji wa mizigo au kuisafirisha ni wa haraka zaidi kuliko huko nyuma. Tozo zinazotozwa na Bandari za Tanzania pia ni shindani na rahisi kulinganisha na bandari nyingine, kwani kila wanapokuwa wanaandaa tozo, suala la kuhakikisha gharama zinakuwa ahueni kwa mteja linaangaliwa kwa umakini mkubwa.

Katika kupanga gharama, TPA inaangalia huduma inazotoa, gharama za uendeshaji na faida kidogo. TPA inahakikisha inatoa bei ambayo mteja anaweza kuimudu.

Tofauti na washindani wa TPA, mteja akienda TPA hakuna tozo inayofichwa na kwamba ukichukua kitabu cha tozo utakuta kila kitu kiko wazi.

Faida nyingine anayopata mteja kwa kutumia bandari za Tanzania ni kupewa mchanganuo wote wa gharama zikiwemo za usafirishaji kutoka bandarini hadi kwake (total road cost analysis).

Katika kuandaa gharama hizo, TPA huwa inashirikiana na wadau wengine waliomo kwenye sekta ya kushughulikia mizigo wakiwemo wasafirishaji.

Kwa kufanya hivyo, ni rahisi kwa mteja anayetumia bandari za Tanzania kulinganisha bei na shoroba nyingine, ambapo mara nyingi TPA gharama zake ni ahueni sana.

Matumizi ya TEHAMA

Katika kuwapunguzia usumbufu wateja, wanaweza kufanya malipo kwa njia ya mtandao (online) kwa muda mwafaka na haraka.

Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) haitumiki kwenye usalama tu, bali inatumika pia vilivyo katika kurahisha shughuli bandarini.

Kabla bandari haijaanza kutumia TEHAMA kama ilivyo sasa, ilikuwa inachukua muda mwingi kushughulikia upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini.

Wateja wanahimizwa kutembelea tovuti ya TPA ambayo ni www.ports.go.tz ambamo watapata taarifa zote muhimu kuhusu TPA pamoja na taarifa za namna mtu anavyoweza akatuma au kutoa mzigo wake bandarini.

Ofisi katika nchi zinazohudumiwa

Ili kutoa huduma bora katika nchi ambazo zinategemea bandari za Tanzania, TPA imeona ni muhimu kufungua ofisi katika nchi zinazotumia bandari zake au kuwa na mawakala wake ili kusogeza huduma karibu na wateja wao.

“Kupitia ofisi hizo wafanyabiashara wa nchi hizo hawana sababu ya kusafiri hadi Dar es Salaam,” anasema Mhandisi Kakoko.

TPA imefungua ofisi katika Jiji la Lusaka nchini Zambia, Kigali nchini Rwanda, Lubumbashi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Bujumbura nchini Burundi.

Katika nchi nyingine, TPA iliona kwamba si lazima iwe na maofisa wake bali mawakala wa kuwawakilisha, hivyo kupunguza pia gharama za uendeshaji. Nchi zenye mawakala wa TPA ni pamoja na miji ya Bukavu na Goma ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Kampala nchini Uganda.

Anasema wateja pia wanaweza kufikisha malalamiko yao kama yapo kwenye ofisi hizo au kwa mawakala na kuyapatia ufumbuzi kwa wakati.

Uboreshaji miundombinu

TPA pia imekuwa ikiboresha Bandari ya Mtwara na bandari zilizo katika maziwa ya Nyasa na Tanganyika ambako nchi za SADC, hususan za Malawi, Msumbiji, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinaweza pia kupitishia mizigo yao.

Wakati TPA ikiboresha bandari zake nyingine nje ya Dar es Salaam, serikali pia imekuwa ikiboresha usafiri wa barabara na reli, ukiwamo ujenzi wa reli mpya ya kisasa (SGR), hivyo kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya barabara au reli kutokea Dar es Salaam.

Yapo maboresho makubwa yanayofanywa na Reli ya TAZARA inayounganisha Tanzania na Zambia pamoja na Reli ya Kati inayokwenda hadi Kigoma na Mwanza. Reli hizi huko nyuma zilikuwa zimelegalega, lakini sasa, mbali ya kukarabitiwa zimekuwa pia zikiboresha huduma zake mara dufu.

Chuo cha Bandari

Chuo cha Bandari kilichoko Dar es Salaam pia kimekuwa kikipokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali, lakini kwa sasa kimekuwa kikipokea wanafunzi zaidi kutoka Comoro.

Mkuu wa chuo hicho, Dk. Joseph Kakeneno, anasema chuo chake kinatoa diploma na kozi fupi si katika sekta ya majini pekee, bali pia masomo wanayofundisha yanagusa au kufanana na ya sekta kadhaa zikiwemo za madini.

Ni kwa mantiki hiyo, anakarabisha pia wanafunzi kutoka Tanzania na nchi za SADC kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya kozi mbalimbali.

By Jamhuri