Ingawa kuna mambo mengi hapa katika u-kisasa, kwa leo nitagusia maeneo matatu tu. Mosi, kuweka biashara katika mifumo rasmi; pili kuwa na maono; na tatu kutengeneza mfumo wa kurithisha biashara kutoka baba kwenda kwa watoto – kutoka kwa wajukuu kwenda kizazi cha pili. Biashara katika mifumo rasmi ina dhana pana, lakini kwa urahisi kabisa ni kuendesha biashara katika mifumo inayoelezeka. Ni ile hali ambayo mmiliki unapokuwapo au kutokuwapo biashara inaendelea kama kawaida. Tunagusia usajili rasmi wa biashara na utamaduni wa kuendesha biashara. Kwenye usajili unaweza kusajili kama mfanyabiashara binafsi, kama mshirika na kama kampuni. Nia yangu hapa ni kutaka kuzungumza kwa ufupi kuweka biashara katika mfumo wa kampuni. Wafanyabiashara wengi hawaelewi dhana ya biashara katika kampuni. Wengi wanaposikia neno kampuni huwa wanapata picha ya kuwa huenda ni dude kubwa sana, lenye magari na majumba mengi pamoja na utitiri wa wafanyakazi.

Tofauti na imani za wengi, kampuni ni utaratibu tu wa kusajili biashara unaotenganisha ukomo wa madeni na utendaji baina ya biashara husika na wamiliki wa biashara hiyo. Unaposajili kampuni, tayari kampuni inakuwa ni mtu kamili kisheria. Ukiwa na kampuni, unapokwenda kukopa benki anayekopa ni kampuni, na si wewe mfanyabiashara. Ukishindwa kulipa deni kinachofikishwa mahakamani ni kampuni na si mmiliki wa kampuni, na wala mali binafsi za mmiliki haziguswi kufidia deni la kampuni.

Tatizo la biashara za sisi Watanzania ni kuwa hazitenganishi kati ya mmiliki na biashara. Mmiliki ndiyo biashara na biashara ndiyo mmiliki. Mmiliki akifa na biashara lazima ife. Lakini huku kwenye kampuni, kikawaida kampuni huwa haifi kutokana na kifo cha wamiliki wake. Ukifa anaweza kurithi mtoto hadi wajukuu. Unaposajili biashara zako katika mfumo wa kampuni unaanza urasimishaji wa kiutendaji. Utahitaji uwe na rekodi za hesabu, utawala, masoko na rasilimali watu.

Mwanzoni unaweza kuwa ukifanya kazi hizi zote peke yako, na mke wako, au na mshirika wako kibiashara, lakini kadiri unavyokua kutakuwa na urasmi zaidi na zaidi. Kwa namna mfumo wa kampuni ulivyo rahisi, ni kuwa ukifa leo au ukiwa hupo, mtu yeyote anaweza kutumia kanuni na ndoto zilizopo kuendesha biashara yako. Huu ni mfumo unaokuwezesha kumiliki duka Songea hata kama unaishi Dar es Salaam na bado ukawa ukivuna faida bila hata kuibiwa.

Pengine kitakachowatisha wengi ni mtaji unaopaswa kuwa nao ili kusajili kampuni pamoja na gharama za usajili. Hapa ndipo mahali rahisi kuliko pote! Unaweza kusajili kampuni kwa mtaji wowote hata shilingi laki moja tu! Gharama za kusajili kampuni pale Ofisi za Usajili wa Biashara (BRELA) ni kuanzia laki moja na kitu tu, kulingana na thamani ya mtaji ulio nao.  Ukitoa gharama za uandaaji wa nyaraka za kampuni (Articles of Association & Memorandum of Association), utaona kuwa unaweza kusajili kampuni yako kwa gharama ya shilingi hata laki moja tu! Ukiwa na daladala moja, wewe mwenye boda-boda moja, uwe na duka dogo au kubwa, hata uwe na nyumba moja ya kupangisha, kila mmoja anaweza kusajili kampuni na kunufaika na biashara katika mifumo rasmi na ya kisasa.

Bahati nzuri ni kuwa huhitaji uwe umesoma ili kuendesha biashara katika mifumo rasmi na ya kisomi. Kuendesha biashara kisasa ni rahisi sana ukilinganisha na kuendesha kienyeji. Binafsi niliyumba na kufilisika biashara ile ya chuo kutokana na kuendesha kienyeji. Biashara ilikuwa ndiyo mimi na mimi ndiyo biashara. Sikuwa na mbinu za kuishi na wafanyakazi, sikuwa na utaratibu wa kukuza biashara na kubwa lililonimaliza ni kuwa niliridhika kupita maelezo! Nilipojiona nimekuwa milionea ‘mtoto’ ndiyo saa niliyokuwa nikiangamia! Hili linawapata wafanyabiashara wengi na Watanzania kwa ujumla.

Inasemekana kuwa Watanzania wengi tuna hulka ya kuridhika mapema kwa mafanikio kidogo tunayoyapata. Nije sasa kinagaubaga katika suala la biashara na maono (vision). Ili biashara ziwe na dira ya muda mrefu, mfanyabiashara anatakiwa kuwa na mipango ya angalau miaka 50 ijayo. Je, wangapi wana mipango madhubuti ya biashara zao kwa miaka angalau 50 ijayo? Mfanyabiashara anatakiwa kujua atakuwa na mtaji wa kiasi gani baada ya miaka 10, 20, 30 na kuendelea.

Ni lazima kufahamu ni nani atarithi biashara au mali zako utakapofariki dunia. Si tu kumjua, lakini kumwandaa huyo mrithi ili naye aje awe na nafasi ya kuwarithisha wengine – kama ni mtoto wako, mjukuu au mtu mwingine. Siyo unakuwa na nyumba ya kupangisha halafu ukifa, hao unaowaachia hawakumbuki kujenga nyingine zaidi ya kula kodi na kunyanyasa wapangaji tu. Niharakishe kusema kuwa moja ya mambo yaliyosababisha biashara za marehemu baba yangu kumfuata kaburini ni kutokuwa na ndoto za muda mrefu kuhusu biashara zake. Biashara zilikuwa za kienyeji, hazikuwa na mfumo rasmi, hazikuwa na mipango ya muda mrefu na wala hakumuandaa mapema wa kuzirithi.  Watazania tunahitaji ushindi wa kiuchumi. Tuonane wiki ijayo.

stepwiseexpert@yahoo.com 0719 127 901

980 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!