Serikali imetenga Sh bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya huduma za saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando ili kusogeza huduma katika mikoa minane ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza kwa niaba ya waziri mkuu wakati wa kuweka jiwe la msingi la jengo hilo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, anasema litakuwa la ghorofa tatu huku likigharimu Sh bilioni 5.4.

Anasema litakapokamilika litawasaidia wananchi kupunguza muda wa kufuata huduma ya saratani katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.

“Dhamira ya Rais John Magufuli ni kuimarisha huduma za afya maeneo mengi nchini, hususan kuboresha huduma za saratani kwenye hospitali za rufaa za kanda, hivyo kuwapunguzia kero wananchi na kudhibiti ugonjwa huu kwa kufuata mtindo bora wa maisha,” anasema Dk. Dorothy.

Jengo hilo linajengwa kwa mfumo wa ujenzi shirikishi (force account), litakuwa na vitanda 120, sehemu ya mionzi tiba, eneo la kupumzika baada ya kupata mionzi, ushauri, matibabu na wodi ya kulazwa wagonjwa.

“Niwapongeze Bugando kwa utaratibu wa ujenzi mlioutumia na kudhibiti matumizi. Msingetumia utaratibu huu, jengo hili lingegharimu Sh bilioni 7 na zaidi,” anasema.

Dk. Dorothy amewataka wananchi waliofika Bugando kwa ajili ya uchunguzi wa saratani kudhibiti magonjwa hayo kwa kubadili mtindo wa maisha, kufanya mazoezi, kutovuta sigara, kunywa maji mengi, kutokunywa pombe kupitiliza na uzito mkubwa.

Anasema magonjwa yasiyoambukiza kama presha, moyo, kisukari na mengine yanaweza kuzuilika kwa kila mtu kutekeleza anayoelekezwa na wataalamu, na kwamba siri ya kudhibiti magonjwa ipo kwenye maarifa yaliyotolewa na mababu kwa kutumia tiba asili.

Katika kuadhimisha siku ya saratani duniani, Bugando imefanya uchunguzi wa saratani kwa wakazi wa Mwanza kwa siku mbili.

Watu 217 wamepata huduma hiyo bila malipo na waliogundulika kuwa na viashiria vya saratani wameshauriwa kuanza huduma za vipimo katika hospitali hiyo.

611 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!