Ujenzi wa barabara unaendelea kwa kasi katika Jiji la Dar es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa foleni za magari zinapungua na hivyo kuondoa usumbufu na kuokoa mabilioni ya shilingi yanayoteketea kila siku. Tunaipongeza Serikali, na hasa Wizara ya Ujenzi kwa kazi hiyo nzuri ambayo inaonekana jijini humo na sehemu mbalimbali nchini.

Pamoja na pongezi hizo, bado tunadhani kuwa kuna kasoro kubwa kwenye ujenzi wa barabara hizo. Kwa mfano, Barabara ya Morogoro, foleni yake haisababishwi na njia chache pekee.

 

Tatizo kubwa la msongamano wa magari katika barabara za Morogoro na Sam Nujoma pale Ubungo linasababishwa na kusubiriana. Kitendo cha magari ya upande mmoja kusubiri ya upande mwingine yapite ndicho kinachosababisha foleni katika barabara hizo.

 

Hatua sahihi kabisa ya kupunguza kero hiyo ni kujengwa kwa flyover katika eneo hilo. Hatua hiyo itayafanya magari ya kila upande yaendelee na safari bila kusubiriana.

 

Ndiyo maana tunasema kwamba pamoja na juhudi za ujenzi wa barabara, hasa kwa mradi wa mabasi yaendayo kasi, tatizo la foleni katika barabara za Dar es Salaam kamwe halitakoma. Ili likome, ni lazima ujenzi wa flyover uzingatiwe katika maeneo ya Ubungo, Mwenge, Morocco, Magomeni, Tazara, Faya, Kamata, na mengine mengi.

 

Lakini ili flyover ziweze kujengwa, zinahitaji maeneo makubwa. Kama hivyo ndivyo, Serikali ina kila sababu za kuangalia sasa utaratibu wa kuzuia ujenzi wa vitegauchumi vikubwa katika maeneo mbalimbali.

 

Madhara ya ujenzi wa miundombinu ya aina hiyo tunayaona Ubungo ambako Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), yamejengwa ndani ya hifadhi ya barabara.

 

Pia maeneo kama ya Barabara ya Zamani ya Bagamoyo idadi yake ya magari inazidi kuongezeka kila siku. Foleni ni kubwa mno. Ni vema basi, kwa muda huu, Serikali ikaweka utaratibu utakaozuia ujenzi wa majengo makubwa ili endapo upanuzi wa barabara utahitajika, basi Serikali imudu kulipa fidia.

 

Tunatoa ushauri huu tukiamini kuwa suala la miundombinu ni endelevu, hasa kutokana na kasi ya ukuaji miji.  Dar es Salaam na miji mingine kama Mwanza inapaswa kuwa mfano mzuri wa kuwafanya wataalamu na viongozi wetu kuipanga miji mipya inayojengwa.

 

Tunasisitiza kuwa kwa Dar es Salaam, bila kujengwa flyover katika maeneo kama Ubungo, kazi yote inayofanywa sasa ya upanuzi wa barabara itakuwa kazi bure. Tena basi, ieleweke kuwa upanuzi huo utahamasisha watu wengi zaidi kujitutumua kununua magari kwa imani kwamba barabara zipo, na foleni hakuna!

 

Majirani zetu-Kenya na Uganda- wanaifanya kazi hii kwa juhudi kubwa. Miuondombinu yao inamwonekano wa kukidhi mahitaji ya miaka 50 au 100 ijayo. Tusiwe wa kujenga na kubomoa kila leo. Flyover Ubungo haiepukiki kama kweli tunataka kukomesha foleni katika Barabara ya Morogoro.

 

 

By Jamhuri