Bilionea Mjapani kwenda kutalii mwezini

 

Kampuni ya tajiri maarufu, Elon Musk, ya SpaceX imetangaza nani atakuwa abiria wake wa kwanza, mtalii, ambaye atasafirishwa kwenda kuuzunguka mwezi.
Mtalii huyo atakuwa ni bilionea Mjapani Yusaku Maezawa, 42, ambaye pia ni mjasiriamali na mwenye biashara kubwa ya uuzaji wa mitindo ya mavazi na ubunifu kupitia mtandao.
Mwenyewe ametangaza: “Nimeamua kwenda mwezini.”
Anatarajiwa kusafiri kwa kutumia chombo cha roketi kwa jina la Big Falcon Rocket (BFR), ambacho ni chombo cha usafiri wa anga za juu kilichozinduliwa na Musk mwaka juzi.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa binadamu kwenda kwenye mwezi tangu safari zilizofanywa na wana anga waliounda chombo cha Apollo 17 cha Shirika la Anga za Juu la Marekani (Nasa) mwaka 1972.
Tangazo kwamba Yusaku atakuwa wa kwanza kufanya ziara hiyo ya kihistoria lilifanywa katika makao makuu ya SpaceX mjini Hawthorne, California, Jumanne iliyopita.
Kampuni hiyo inasema safari hiyo itakuwa “hatua kubwa sana katika kuwezesha watu wa kawaida ambao wamekuwa na ndoto ya kusafiri anga za juu wakati mmoja maishani.”
Awali kwenye Twitter, Musk alikuwa tayari amesema kwamba abiria huyo atakuwa wa kutoka Japan.
Ni wanadamu 24 pekee ambao wamewahi kusafiri kwenda kwenye mwezi na wote walikuwa Wamarekani.
Waliokuwa kwenye safari za Apollo 8, 9 na 13 waliuzunguka mwezi bila kutua. Hata hivyo bado haijabainika bilionea huyo atafanya safari yake wakati gani.
Hii ni kutokana kwamba itategemea chombo cha anga za juu ambacho bado hakijaundwa kufikia sasa.
Mwaka jana Musk alitangaza kwamba atakuwa akiwatuma watalii wawili ambao watalipia gharama ya safari hiyo kwenda kuuzunguka mwezi.

Mwisho