url-7Wakati joto likizidi kupanda kuhusu hatma ya kiwanda cha saruji cha Dangote kilichoko Mkoani Mtwara, JAMHURI limebaini kuna mgogoro mkubwa wa uongozi ndani ya kiwanda hicho, lawama zikielekezwa kwa serikali.

Mmoja wa maafisa wa kampuni ya Dangote, ambaye amezungumza na JAMHURI kwa masharti ya kutotajwa gazetini, amesema yapo mambo ambayo hayakubaliki yanayofanywa uongozi wa kiwanda hicho cha kuzalisha saruji.

Amesema kuna watu wa kati (madalali) ambao wanayumbisha uongozi huku wakishauri malighafi zinunuliwe kutoka nje ya nchi, kinyume na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Dangote.

“Kuna watu wenye asili ya Asia wamekuwa watu wa kati na hawataki kabisa Dangote atumie kitu chochote kupitia mashirika ya hapa Tanzania. Mpaka wamefikia hatua ya kuitafuta kampuni moja (jina tunalihifadhi) kutaka kuingia makubaliano na Shirika la Maenedeleo la Petroli Tanzania (TPDC) ili wauziwe gesi na kampuni hiyo ndiyo iwauzie Dangote.

“Hata wabia wa TPDC nao walimfuata Dangote wakitaka wamuuzie gesi. Je Nigeria, Ethiopian na Zambia ambako kampuni ya Dangote inafanya kazi pia wanafanya hivyo?” kilihoji chanzo chetu.

Chanzo chetu kinasema, yanatengenezwa mazingira kuonesha kwamba makaa ya mawe hapa nchini hayakidhi viwango ili waendelee kutumia yale yanayotoka Afrika ya Kusini, huku wakitaka kupatiwa unafuu wa kodi.

“Aliko Dangote anashangaa sana na aliwahi kuniuliza mbona Watanzania waninisumbua sana kwa simu na maneno? Wananichanganya kwani nimewekeza kwenye nchi zaidi ya 25 barani Afrika lakini kwenu pametia fora,” chanzo chetu kinanukuu maneno kiliyoambiwa na Dangote.

Kutokana na kuwepo kwa tuhuma za makaa ya mawe kutokidhi viwango, JAMHURI limezungumza na meneja mauzo wa Tancoal, Emmanuel Constatinides, anayesema kampuni yao inao uwezo wa kuvisambazia viwanda vya saruji makaa ya mawe.

Constatinides amesema kampuni ya Tancoal imekuwa ikiviuzia viwanda kadhaa makaa ya mawe na hapajawahi kujitokeza malalamiko kutoka kwa wateja wao.

“Sisi tunawauzia makaa ya mawe viwanda vya saruji Tanga, Maweni-Tanga, Mbeya, Lake pamoja na Kigamboni, kwa ujumla mahitaji yao ni takribani tani 275,000. Kwa hiyo sisi bado hatujashindwa kuwahudumia Dangote.

“Ninakuhakikishia kwamba tunao uwezo wa kuwahudumia Dangote kiwango cha makaa ya mawe wanachokihitaji…tumekuwa tunafanya hivyo kwa makampuni kadhaa yanayotengeneza saruji hapa nchini,” amesema Constatinides.

Akizungumza na JAMHURI, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba, amesema hawezi kuzungumzia kuhusu kuwepo kwa madai ya kampuni inayotaka kufanya udalali kwenye gesi inayotakiwa kupelekwa kwenye kiwanda cha Dangote.

“Sisi tunaendelea na mpango wetu wa kumpelekea gesi Dangote, maana yeye ndiye centre kwetu. Kuhusu nani ataingia kwenye suala la kuzalisha umeme sasa hilo ni la Dangote mwenyewe,” anasema Musomba.

Katika taarifa yake, TPDC imesema si kweli kwamba shirika hilo limeshindwa kukiuzia gesi asilia Kiwana cha Dangote kwa bei rahisi kilichopo mkoani Mtwara na hiyo kuchangia kusimamisha uzalishaji wa kiwanda hicho.

“TPDC imefanya jitahada mbalimbali kuhakikisha kwamba kampuni ya Dangote inapata nishati hiyo muhimu kwa ajili ya kuzalisha saruji, ikiwemo kufanyika kwa vikao mbalimbali, pamoja na makubaliano yaliyofanyika kwa Dangote kuridhia nia yao ya kutumia gesi asilia kuzalisha umeme kwa ajili ya kiwanda hicho,” amesema Musomba.

Akizungumza kuhusu suala la bei kubwa ya gesi, kigezo ambacho kimekuwa kikitumiwa na maofisa wa kampuni ya Dangote, amesema bei elekezi ambayo inakua inapendekezwa na TPDC lazima iridhiwe na ipitishwe na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ndipo ianze kutumika.

“Dangote kama mtumiaji wa matumizi ya viwandani amekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na TPDC, tumekubaliana kuwauzia kwa Dola za Marekani 5.14/mmb …kiwanda hicho kimeomba kupewa gesi asilia kwa bei ambayo ni ndogo ikilinganishwa na gharama za kununua gesi ghafi kutoka kisimani,” amesema Musomba.

 Amesema gesi ghafi kutoka kisimani hupitishwa kwenye mitambo ya kuchakata gesi asilia kufikia viwango vinavyokubalika kwa mtumiaji na baadaye kusafirishwa kupitia bomba kwenda kwa mtumiaji.

“TPDC haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei ya kisimani kwa sababu kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na kuisafirisha gesi hiyo…tayari tumeshafanya majadiliano ya mkataba ya awali na Dangote kwa ajili ya kuwauzia gesi asilia itakayotumika kuzalishia umeme utakaotumiwa na kiwanda hicho,” amesema Musomba.

Akizungumza na JAMHURI, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema ni lazima Dangote atumie mali ghafi za hapa nchini katika kutimiza dhana ya kutengeneza ajira kwa asilimia 40.

Amesema baada ya kuteuliwa kuwa waziri, alihakikisha makaa ya mawe yanakuwa na bei nzuri, kutoka Dola za Marekani 50 za mwaka 2015, mpaka Dola za Marekani 39,  kiasi cha kushindana na nchi nyingine kama Afrika Kusini, ambako anasema kimahesabu ni rahisi zaidi kununua makaa ya mawe ya Ngaka, kuliko kuagiza kutoka nje ya nchi.

“Tancoal ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) liko chini ya wizara yangu, hivyo tulilazimika kushusha bei kutoka Dola za Marekani 50 mpaka Dola za Marekani 39, ili kumudu ushindani, lengo la serikali ni kukuza uchumi na kuwafanya wananchi washiriki kwenye uchumi wao.

“Yakinunuliwa makaa ya mawe hapa nchini, wachimbaji watapata, mama ntilie watapata, ajira za madereva zaidi ya 1000 zitatengenezwa, wauza vipuli vya magari pia watapata bila kuwasahau wauza matairi,” amesema Mwijage.

Anasema bei ya makaa ya mawe Afrika Kusini kwa tani moja, ni Dola za Marekani 83 ukijumlisha na gharama ya usafiri ambazo ni Dola za Marekani 35 (Sawa na Sh 70,000/-), inakuwa kama Dola za Marekani 118, wakati makaa ya mawe ya Ngaka yanauzwa kwa Dola za Marekani 60 (ambazo ni sawa na Sh 120,000/-) kwa tani, ukichanganya na usafiri Dola za Marekani 30, bado haifiki hata Dola za Marekani 100 (ambazo ni sawa na Sh 200,000/-).

“Anapoguswa Dangote sio jambo dogo, Dangote anazalisha tani milioni 3, uwezo wa viwanda vyote kama vingefanya kazi ni tani milioni 8.7, soko la Tanzania linahitaji tani milioni 4.3, kwa hiyo Dangote sio wa kupuuza, amebadilisha mchezo.

“Nimezungmza na Dangote kupitia kwa katibu Mkuu Dk Adelhelm Meru, amemuita Mkurugenzi Mtendaji, anasema ni tatizo la ufundi, kiwanda kipya ambacho hakijakamilisha miaka miwili ni jambo la kawaida,” amesema Waziri Mwijage.

Mtoa taarifa wetu anasema, kuna waagiza saruji wakubwa kutoka nje ya nchi ambao biashara zao zimekufa baada ya kuanza kwa uzalishaji wa kiwanda cha Dangote, wanaongoza kampeni kuhakikisha kwamba Dangote hafanikiwi ili warudi kwenye biashara.

Anavitaja viwanda vingine vya saruji vilivyokuwapo kabla ya Dangote, kuwa sehemu ya mkakati wa kukiua kiwanda cha Dangote ili waendelee kuwalangua watanzania.

Anataja sababu nyingine inayoonekana kukwamisha utendaji katika kiwanda cha Dangote, kwamba uongozi wa kiwanda hicho asilimia 70 ni watu wenye asili ya Asia, ambao wanatafuta namna ya kuwapatia biashara makampuni ambayo wana nasaba nayo.

“Ni kweli kuna kundi fulani la wafanyabiashara linafanya kila njia kumhujumu na kumgonganisha Dangote na serikali kwasababu zao, ila nimekuwa nikimkumbusha Dangote kwamba wakati ananza ujenzi, Rais Magufuli alikuwa waziri wa ujenzi, hivyo anajua kila kitu kinachoendelea,” kimesema chanzo chetu.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema si kweli kwamba hakuna makaa ya mawe ya kutosha kutoka nchini.

Amesema Tancoal wanazo zaidi ya tani milioni 400, ambazo wanaweza kuzichimba kwa miaka 40. Hivyo kusisitiza kamba kuna makaa ya mawe ya kutosha.

“Haitatokea na ruhusa haitatolewa kwa mtu kwenda kununua makaa ya mawe nje ya Tanzania, kwa hiyo wenye viwanda vya saruji wote lazima watumie mali ghafi kutoka hapa nchini, lazima watumie jasi na makaa ya mawe kutoka Tanzania,” amesema Prof. Muhongo.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe, ameliambia JAMHURI, amefanya utafiti mdogo kuhusu sekta ya saruji hapa nchini kutoka kwa baadhi ya wazalishaji wa saruji.

Zitto amesema amegundua kwamba suala la makaa ya mawe sio suala la Dangote pekee bali ni suala la sekta yote ndogo. Amesema ni jambo ambalo linahitaji kuingiliwa na mamlaka za juu za nchi ili kuokoa uzalishaji nchini na kupambana na ukiritimba unaotengenezwa kwa makusudi katika uzalishaji wa makaa ya mawe.

“Kimsingi Wizara ya Nishati na Madini inatengeneza kwa makusudi biashara ya Tancoal. Nani yupo nyuma ya kampuni hiyo? ukiachana na kwamba Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ina hisa asilimia 30, katika hisa asilimia 70, kuna mwekezaji ndugu yetu mtanzania ambaye alikuwa mzabuni wa mafuta TANESCO. Huyu ndiye anayelindwa na Wizara ya Nishati na Madini,” amesema Zitto.

Mbunge huyo amesema hakuna ubaya katika kumlinda, bali tatizo ni kwamba Tancoal haiwekezi kwenye uzalishaji na matokeo yake uzalishaji wao ni mdogo mno. Hawawezi kukidhi haja ya kiwanda kimoja kidogo cha kuzalisha saruji.

“Tancoal inauza makaa ya mawe ambayo hayajachakatwa, ambayo mnunuzi akinunua inabidi apoteze asilimia 25 ya mzigo kwani ni majivu. Maana yake katika kila malori 4 yanayobeba makaa kutoka Ngaka mpaka Mtwara au Tanga, lori moja ni majivu. Hii inasababisha makaa kutoka Afrika Kusini kuwa nafuu Kwa sababu yanakuwa yamechakatwa tayari kuondoa majivu,” amesema Zitto.

Zitto amesema, hata ulinganifu wa bei unaofanywa ni sawa na kulinganisha bei ya embe dhidi ya bei ya juisi ya embe. Ameshauri serikali ikae na wenye viwanda ili kuwasikiliza kwanza waelewe jambo lenyewe. Pamoja na kukaa na serikali ameshauri serikali imtake Tancoal kuongeza uzalishaji.

“Akiba ya makaa ya mawe ni nzuri, kinachotakiwa ni mwekezaji, kuwekeza kwenye kiwanda cha kuchakata makaa ya mawe na kuyaongezea ubora, Ili makaa yanayonunuliwa na Viwanda yasiwe na majivu,” amesema Mbunge wa Kigoma Mjini.

Amesema madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na viwanda vya saruji, vinaweza kufungwa kwa sababu ya gharama kubwa za uzalishaji zitazosababisha bei ya saruji inayozalishwa nchini kuwa kubwa na hivyo kutoa fursa ya saruji kutoka nje ya nchi kujaa nchini kwani gharama ni nafuu kutokana na serikali za nchi hizo kutoa ruzuku Kwa wazalishaji.

Chanzo chetu kingine ambacho hakikupenda kutajwa gazetini, kimesema tatizo kubwa ni uelewa mdogo na maono madogo katika suala hilo. Chanzo hicho kinasema kuliangalia suala hilo kwa jicho tu la kiwanda cha saruji (majengo) ni mtazamo finyu.

“Kugundulika kwa gesi Mtwara kulikuja na matarajio na hofu kwa wananchi wa Mtwara kiasi kwamba kukawa na harakati za kuzuia gesi isitoke zilizohatarisha hali ya usalama. Katika kutuliza joto na kudhibiti hofu na matarajio kwa wananchi, Serikali iliahidi kuwa wananchi wa Mtwara watanufaika na gesi na moja ya faida hizo ni viwanda na ajira.

“Serikali ililazimika kufanya jitihada za kutafuta Viwanda kwenda Mtwara ili kuishamirisha Mtwara. Ikumbukwe Mtwara si eneo la viwanda au linalovutia miongoni mwa wawekezaji hivyo kumfanya mtu awekeze Mtwara…kutumia wasta akapatikana Dangote.  

“Katika uchumi kuna kitu kinaitwa upendeleo na fursa maalum kwa anayewahi (first movers advantage). Ililazimu mazingira haya kuandaliwa kumvutia aweke kiwanda chake Mtwara. Makampuni mengine hamsini na kitu yanayoshughulika na mbolea, plastiki na madawa (bidhaa zitumiazo gesi asilia) vilihamasika kutaka kuwekezs Mtwara,” kinasema chanzo chetu.

Chanzo hicho kinasema, alihitajika mwekezaji mkubwa wa hadhi ya Dangote kuwekeza Mtwara ili wengine wavutike. Chanzo hicho kimesema wawekezaji wakubwa wanasikiliza na kuamini ushuhuda wa mwekezaji mkubwa kuliko kauli nzuri za Serikali pekee. Hivyo, Dangote alipaswa kuwa ndio kivutio na chambo cha wawekezaji wengine. Habari kuwa Dangote ameshindwa inawavunja moyo wengine kujaribu kuwekeza.

By Jamhuri