Tumeshaelewa hoja ya Edward Lowassa, nadhani sasa ni wakati wa kuelekeza juhudi zetu katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Ni muhimu tukampongeza Lowassa kwa kuwa kiongozi wa kwanza nchini kulipa suala hili uzito unaostahili, lakini tutambue pia kwamba Lowassa si mtu wa kwanza kuzungumzia tatizo hili, kwani kwa wale wanaosoma utafiti mbalimbali, kwa miaka mingi sasa taasisi za utafiti kama vile REPOA, ESRF, na nyingine nyingi nje ya nchi (Benki ya Dunia n.k), zimekuwa zikilijadili suala hili na kutoa tahadhari kwa muda mrefu.

 

Kitu muhimu alichofanya Lowassa ni kuamsha watu kutokana na upeo wake mkubwa na uelewa, juu ya masuala yanayozunguka jamii za Dunia ya Tatu, kupitia usomaji wa utafiti na ripoti mbalimbali, tofauti na viongozi wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao ni mchanganyiko wa wavivu wa kusoma na wasiojua kusoma kwa kuelewa.

 

Suala jingine muhimu, pengine zaidi ni kwamba, kitendo cha Lowassa kulizungumzia suala hili ni ishara kubwa kwamba pengine sasa suala hili litapata utashi wa kisiasa (political will), kwani ‘lack of political will’ ni moja ya vikwazo vikubwa vinavyotukabili kama Taifa katika jitihada za kutokomeza umasikini, na vilevile kuchukua uamuzi mgumu kwa masilahi ya Taifa.

 

Ni vigumu kulielewa tatizo la ajira kwa vijana bila ya kuwa na takwimu za kulitazama na kulielewa kwa undani, kwani tatizo hili ni la kimfumo kuliko kitu kingine chochote. Ukosefu wa uchambuzi usiozingatia takwimu na pia kulielewa tatizo hili kimfumo, ni moja ya mapengo makubwa yanayotawala mijadala juu ya suala hili.

 

Nia yangu ni kujaribu kuziba pengo hilo, ili kwa pamoja tusaidiane kuondokana na siasa katika mjadala huu na kuhamia katika mikakati ya kutegua bomu hili kabla halijalipuka.  Nitakachofanya hapa hakitakuwa uchambuzi, bali kwanza kuweka takwimu muhimu ili, kwa pamoja, tufanye uchambuzi na pengine kupata ufumbuzi angalau kimjadala.

 

Nitaanza na mfumo wa elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu na kumalizia na mawazo yangu kuhusu masuala muhimu ya kutazama kabla ya kuanza kunyooshea vidole Serikali au chama chochote cha siasa.

 

Elimu yamsingi

Kufikia mwaka 2012, mfumo wetu wa elimu ya msingi unakadiriwa kuwa na watoto karibu milioni 10. Hili ni ongezeko la karibu watoto milioni 2.5 ndani ya kipindi cha miaka mitano tu, kwani mwaka 2007 mfumo huu ulikuwa na jumla ya watoto milioni saba na nusu;

 

Inakadiriwa kwamba watoto wanaofanikiwa kumaliza elimu ya msingi ni asilimia 80 ya watoto wote, huku asilimia 20 wakishindwa kufika darasa la saba kutokana na sababu mbalimbali. Kwa maana hii, kila baada ya miaka kadhaa, watoto wasiopungua milioni moja huingia mitaani wakiwa primary school drop-outs.

 

Hii ni nje ya idadi ya watoto wasiofanikiwa kujiandikisha darasa la kwanza, hivyo kufanya idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 wanaoishia mitaani bila elimu ya msingi kuwa kubwa zaidi, kila baada ya miaka kadhaa.

 

Tumeona kwamba ni asilimia 80 ya watoto ndiyo wanaofanikiwa kuhitimu darasa la saba. Sasa kati ya hawa, wanaofanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari ni asilimia 20 ya hao asilimia 80.

 

Kwa maana hii, nje ya wale watoto zaidi ya milioni moja tuliobaini kwamba hawafiki darasa la saba, kuna mamilioni wengine wasiofanikiwa kuendelea na elimu sekondari kila baada ya miaka kadhaa. Kwa hiyo ukichanganya makundi haya mawili (primary school drop-outs na standard seven failures), unakuta mamilioni ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 wanaishia mitaani kila baada ya miaka kadhaa.

 

Elimu ya sekondari

Ukiachilia mbali kundi la watoto wanaoishia ngazi ya elimu ya msingi, kuna tatizo pia kwenye ngazi ya sekondari. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (mwaka 2010), katika kipindi cha mwaka 2000-2010, wanafunzi milioni 1.3 walihitimu elimu ya sekondari Tanzania. Matokeo yao mitihani kidato cha nne yalikuwa kama yafuatayo:

 

•Daraja la kwanza 3% (wanafunzi takribani 39,000)

•Daraja la Pili 5% (takribani wanafunzi 65,000)

•Daraja la Tatu 15% (takribani wanafunzi 195,000)

•Daraja la Nne 50% (takribani wanafunzi 650,000)

•Waliofeli 26% (takribani wanafunzi 338,000)

 

Iwapo tunachukulia kwamba wanafunzi waliopata madaraja ya Kwanza hadi Tatu ndiyo wanaoendelea na elimu ya juu, basi ina maana kwamba kati ya wanafuzi milioni 1.3 waliohitimu elimu zao za sekondari katika kipindi hicho (2000-2010), waliofanikiwa kuendelea na elimu ya juu ni asilimia 25 tu [sawa na wanafunzi 325,000 kati ya wanafunzi 1,300,000].

 

Hivyo, katika kipindi hiki, wanafunzi wa sekondari walioishia mitaani ni karibu 975,000. Hata kwa wale waliofanikiwa kuendelea na elimu ya juu, kama tunavyoelewa, bado suala la ajira huko mbele si la uhakika.

 

Benki ya Dunia inakisia kwamba takribani vijana 850,000 wenye umri kati ya miaka 15 na 25 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka nchini Tanzania, huku asilimia 40 ya hawa ikiwa ni waliofeli kidato cha nne; Benki ya Dunia inazidi kukadiria kwamba ifikapo mwaka 2015 kutakuwa na nyongeza ya vijana milioni 1.3 katika soko la ajira.

 

Kwa mujibu wa takwimu nyingine kutoka African Economic Outlook (mwaka 2010), asilimia 60 ya Watanzania hawajavuka miaka 25, na inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2015, asilimia 75 ya Watanzania watakuwa chini ya umri wa miaka 25.

 

Elimu vyuo vikuu

Kuanzia kipindi cha Uhuru hadi mwisho wa miaka ya 1980, inasemekana kwamba asilimia 90 ya wahitimu wa vyuo vikuu Tanzania kila mwaka walikuwa wanapata ajira (wage employment). Lakini ilipofikia mwaka 1999 idadi hii ilishuka hadi asilimia 70. Leo hii, inasemekana kwamba wahitimu wa vyuo vikuu wanaopata ajira kila mwaka haivuki asilimia 50.

 

Baadhi ya changamoto

•Idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu inazidi kukua kwa kasi kuliko uwezo wa uchumi kuzalisha ajira.

 

•Vilevile vijana wengi wanaohitimu darasa la saba, sekondari na pia baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu hawana ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira.

 

•Vijana wengi wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu pia hawana ujuzi unaohitajika kujiajiri wenyewe, ukiachilia mbali tatizo la mitaji ya kuanzisha biashara.

•Chini ya mfumo wa soko huria, Serikali bado haijafanikiwa kuja na sera zenye kuleta matumaini kwa vijana walio wengi.

 

•Nchi wahisani, hasa kupitia Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) hawana nia ya dhati ya kulitatua tatizo hili, kwani hali iliyopo inayapa mataifa makubwa faida kubwa kiuchumi.

 

Sekta kuu za ajira nchini

•Kilimo ni takribani asilimia 80.

•Sekta isiyo rasmi (informal sector) takribani asilimia 9.

•Sekta binafsi/iliyo rasmi (viwanda na huduma) takribani asilimia 5.

•Serikali/sekta ya umma karibu asilimia 2.5.

•Kazi za nyumbani (shamba boys, n.k) karibu asilimia 3.5.

 

Baadhi ya masuala muhimu ya kuzingatia

Kwanza, chini ya mfumo wa soko huria unaofuata kanuni za kiliberali na ubepari, uchumi unaendeshwa kwa kufuata nguzo kuu tatu ambazo ni PRIVATIZATION, LIBERALIZATION & MARKETIZATION.

 

Pili, moja ya maeneo muhimu kisera katika mfumo huu yanayosimamiwa kwa ukaribu na Benki ya Dunia, IMF na WTO ni pamoja na kupunguza mfumuko wa bei, kuondoa vikwazo vya biashara (ili bidhaa za nje ziingie kwa urahisi na kupata soko) na kuondoa vikwazo kwa FDI, (ili iwe rahisi kwa mitaji ya nje kuja kuwekeza kwenye sekta ambazo ni resource-based), kupunguza matumizi ya serikali (hasa matumizi katika uwezekezaji kwenye sekta ya umma na badala yake kuachia nguvu za soko zifanye hilo) n.k; yote haya kwa imani kwamba yatasaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

 

Tatu, chini ya mfumo huu, Serikali haina nafasi ya kuwa mzalishaji, mtengenezaji wa ajira, na kadhalika, badala yake hayo hutegemea zaidi nguvu ya soko. Kazi kubwa ya Serikali inabakia kuwa mwezeshaji.

 

Hii ni tofauti na enzi za Ujamaa ambako Serikali ilikuwa na nafasi ya kuzalisha huduma na bidhaa kwa wingi, kutengeneza ajira na kadhalika, hasa kupitia umiliki wake wa njia kuu za uchumi.

 

Na nne, tofauti na jinsi nchi tajiri zinavyoendesha sera za uchumu katika nchi zao, kwa mfano kwa kulipa suala la ukosefu wa jira uzito mkubwa sambamba na ukuaji uchumi na mfumuko wa bei, mataifa haya hayataki kushughulika na suala la ukosefu wa ajira kwenye nchi zetu.

 

Badala yake hujikita zaidi kwenye ukuzaji uchumi (ili mitaji yao ipate soko zaidi) na mfumuko wa bei (ili dhamana za wawekezaji zisiathirike). Kuondoa vikwazo kwa biashara na vitegauchumi kutoka nje, inasaidia wakubwa hawa kuua uwezo wetu to industrialize, na kuwa na a skilled pool of employees/labour force, kwani tukifanikiwa katika haya mawili na kujitosheleza kwa bidhaa, tutaweza kuleta ushindani dhidi ya bidhaa zao zinazoingia kwa urahisi kupitia soko huria.

 

Hizi ni baadhi ya changamoto muhimu ambazo Serikali ya CCM au Chadema; zote zitakumbana nazo Ikulu, na ni suala ambalo lipo katika nchi zote za “Dunia ya Tatu”.

 

Ni muhimu katika mjadala wetu juu ya ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana, tukawa na ufahamu juu ya changamoto hizi hasa kuhusu nini Serikali inaweza kufanya, na nini Serikali haiwezi kufanya bila ya kujali ni chama gani cha siasa au mtu gani anaingia Ikulu mwaka 2015.

By Jamhuri