Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshusha riba ya mikopo ya fedha inayoyakopesha mabenki ya kibiashara nchini kutoka asilimia 16 ya awali hadi asilimia 12.

Katika barua yake yenye kumb.GA.302/389/01 Vol VII ya Machi 3,2017,  Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dk. Natu Mwamba, ameziandikia benki zote za biashara kuziarifu kuhusu mabadiliko hayo na kwamba yataanza rasmi Machi 6, mwaka huu.  

Wataalamu kadhaa wa masuala ya uchumi wameupongeza msimamo huo wa Benki Kuu, huku wakisema utaleta ahueni kwa mabenki ya biashara kuimarisha ukwasi wake. 

Mmoja wa wataalamu ambaye hakutaka kutajwa gazetini, ameliambia JAMHURI, punguzo hilo la Benki Kuu, litasadia mabenki ambayo hayana ukwasi ila yana hati fungani (Treasury Bills).

“Kama Benki ina dhamana zenye thamani ya Sh bilioni 50 na unataka fedha kutoka Benki Kuu, maana yake ni kwamba watakupatia fedha hizo kwa chini ya asilimia 1, hivyo utapata fedha nyingi zaidi,” amesema mtaalamu huyo.

Ameongeza kuwa, zamani ukitaka ilikuwa mabenki yakitaka fedha taslimu, huku ukiwa na hati fungani, mabenki yalikuwa yanapatiwa kwa riba ya asilimia 16.

JAMHURI limezungumza na baadhi ya wachumi ambao wameonyesha kuunga mkono na kuipongeza hatua hiyo ya kushusha riba ya mikopo ya mabenki.

“Hatua hii itaakisi gharama za mabenki ya biashara kwa kushusha gharama za riba ya mikopo inayowakopesha walaji wake. Kama benki zilikuwa zikikopa kwa riba ya asilimia 16 maana yake zenyewe zilikuwa zikiwakopesha walaji wake kwa riba ya juu zaidi ya hiyo,” amesema Profesa Prosper Ngowi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lenny Kasoga, amesema kuwa hatua hii itasaidia pesa kurudi mtaani kwa kiasi fulani kutokana na watu waliokuwa na nia ya kukopa fedha kwenye mabenki ya kibiashara kuwa na fursa nzuri ya kufanya hivyo.

“Sekta binafsi na wafanyabiashara watakuwa wamepata ahueni ya riba hivyo watakuwa na wigo wa kukopa zaidi ya ilivyokuwa awali maana watavutika kwa riba ndogo,” amesema Dk. Kasoga.

Ameongeza kuwa hatua hii yaweza kuchangia kupungua kwa kasi ya mfumko wa bei kwa kurahisisha mazingira ya ufanyaji wa biashara.

Itakumbukwa kwamba Novemba 2013, Benki Kuu iliziandikia barua benki zote za biashara nchini ikiziarifu kuwa riba ya mkopo ilipangwa kuwa ya asilimia 16.

Kulingana na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania inasimamia kisheria mabenki na taasisi za fedha ambazo zinachukua amana kutoka kwa wateja. 

Mpaka kufikia mwezi Oktoba 2016, taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu zilifikia 66 zikiwapo benki za biashara 38.

Akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia kitaaluma ni mchumi, Zitto Kabwe, amesema Benki Kuu ni mkopeshaji wa mabenki pale wengine wowote hawawezi kukopesha.

Amesema waraka uliotolewa na Benki Kuu kushusha riba ya kuuza hati fungani kutoka asilimia 16 mpaka 12 inaonesha kuwa Benki Kuu inapunguza gharama za mabenki kukopa kwake kwa asilimia 4 ambazo ni nyingi sana. 

“Hii ni ishara kuwa uchumi hauna fedha na hivyo Benki Kuu inawezesha mabenki kuuza hati fungani ili wawe na fedha na kutoa mikopo kwa watu na hivyo kupunguza uhaba wa fedha kwenye uchumi. 

“Njia hii ni ya muda mfupi, njia bora zaidi ni serikali kutumia mapato na matumizi yake kuingiza fedha kwenye uchumi kwa kupunguza baadhi ya kodi kwenye mapato ya watu na kuongeza matumizi kwenye miradi mikubwa yenye kuajiri watu wengi,” amesema Zitto.

By Jamhuri