Busara itumike katika matumizi ya maneno

Na Angalieni Mpendu
Dhani na Ongopa ni maneno ambayo baadhi ya watu duniani huyatumia ima kwa
nia njema, au kwa nia mbaya ya kuwagombanisha, kuwafarakanisha,
kuwaangamiza, au kuwaua watu wengine katika familia, jumuiya au taifa.
Ukweli maneno haya ni vitenzi, na vinapotumika mara nyingi vinatoa majibu
mabaya. Mtu anayetumia maneno haya hana budi kuwa makini, mwingi wa
busara na mwingi wa utu kuepuka madhara; ama sivyo atatumbukia ndani ya
maovu.
Tangu dunia iumbwe, baadhi ya watu wamekuwamo katika michakato ya
kubwatizana, kurushiana makonde, kuchapana bakora, kulengeana mitutu ya
bunduki na mizinga na kutupiana mabombomu na makombora kwa lengo la
kuvuruga utulivu na amani ya dunia.
Wajuzi na wataalamu wa lugha wanatambua vyema maana na hasara ya
matumizi ya dhani na ongopa. Kadhalika viongozi wa dini wanafahamu uzito wa
dhambi inayopatikana katika kudhani na kuongopa. Makundi haya yako mbali na
matumizi ya maneno haya.
Ibilisi alimshawishi na alimwongopea Bibi Hawa, asipokula tunda
(lililoharamishwa) na mume wake Adamu, aelewe Adamu ataoa mke mwingine,
atamdhulumu na atamkimbia. Hawa alifanya kila hila ya kumlisha tunda Adamu.
Hakika walikula wote.
Matokeo walijitambua na kuficha tupu zao na majani. Mwenyezi Mungu aliwatoa
Peponi na kuwaleta ardhini. Walianza maisha ya dhiki na taabu kwa sababu ardhi
haikuwa na mimea na hawakuzoea kupata taabu. Bibi Hawa alinung’unika sana.
Utamaduni huo wa kutaabika tunao sisi watoto wao hadi leo.
Tazama katika nchi ya Misri, mke wa waziri fulani alivyoongopa na kumsingizia
Nabii Yusuf a.s. (Joseph) alitaka kumbaka. Ilhali yeye mke wa waziri ndiye
mbakaji. Nabii Yusuf a.s. alitupwa gerezani, hadi mkono wa uokovu ulipotokea na
kumtoa gerezani na kuwa huru.
Angalia kizee kichawi Gagula kilipoongopa kwa watu weupe wa kutoka kwenye
nyota (Wazungu), kwamba Twala ndiye Mfalme halali wa nchi ya Wakukuana.
Umbopa si Mfalme wa nchi hiyo. Ukweli Umbopa ndiye aliyestahiki kuwa Mfalme.
Nchi iliingia katika umwagaji damu za watu baada ya ngoma ya kufichua wachawi.
(kitabu: Mashimo ya Mfalme Sulemani).
Rudisha simanzi zako pale taifa kubwa duniani (Marekani) lilipoitangazia dunia
kuwa Rais Saddam Hussein wa Irak alikuwa anamiliki silaha kali na ni mtu hatari;
alikamatwa na aliuawa. Uchunguzi wa kina ulibaini pasi na shaka ulikuwa ni
uwongo.
Taifa hilo hilo na washirika wenzake walipiga propaganda nchini Libya na duniani

kuwa Rais Muammar Muhammad al Qadhaf (Gaddafi) ni dikteta na walimwekea
vikwazo vya kiuchumi. Wakubwa hao walianzisha vita ya wenyewe kwa wenyewe
na kumuua Gaddafi. Ukweli Gaddafi hakuwa dikteta, alikuwa ni kipenzi cha watu.
Juzi juzi tulimsikia Rais wa Marekani, Donald Trump, akilalama baadhi ya
watumishi wa Ikulu nchini humo, wanaacha kazi kutokana na maneno maneno
(dhani na uwongo) kuhusu vitendo vya ngono na unyanyasaji wa kingono.
Rais Trump amesikika akisema kwa hisia kali kwamba maneno haya yanakera,
yanaharibu taratibu za kazi na kuvunja heshima ya watu. Ni vyema watu
wakaacha tabia hiyo.
Nimetoa mifano hiyo michache kukumbusha na kutoa hadhari juu ya matumizi
ya neno dhani na ongopa. Busara iliyoje kuwa makini na matumizi ya maneno
kwa lengo na nia ya kuweka vyema mustakbali wa amani ya Taifa letu!
mwisho