Fedha si msingi wa maendeleo! Haya ni maneno yaliyowahi kutamkwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Yalisemwa miaka mingi kabla dunia haijautambua utandawazi. Tunayaona ndani ya Simba inayotaka kumtimua Patrick Aussems. 

Mwalimu Nyerere alimaanisha kwamba fedha ni matokeo ya mchanganyiko wa mambo mbalimbali ambayo yakifanywa kwa kutumia busara na uvumilivu ni lazima yazae matunda mazuri. 

Ushahidi wa ukweli wa maneno hayo upo dhahiri pale mtu anapoamua kuzisoma historia za maisha ya matajiri wakubwa wa Marekani, Canada, Afrika Kusini, Japan, China na nchi za Ulaya. Matajiri wakubwa hawakuanza na mitaji kwa maana ya fedha, walikuwa na mawazo ya kibiashara ambayo kuyafanikisha kwake, ilibidi waongozwe na maisha ya kutokata tamaa. 

Fedha ikaja kupatikana baada ya juhudi na maarifa mengi pamoja na elimu na kuwekeza katika wakati uliostahili. Nimeutazama mkanda mmoja wa video ambao ni wa sekunde kadhaa, ukiwaonyesha mashabiki wa Simba wakisisitizia mabadiliko ndani ya klabu. 

Rais wa Simba kwa sasa, Mwina Kaduguda, anaonekana kuamini katika mabadiliko, ila bado anaonekana kutaka kutiwa moyo katika kufikia lengo lake. 

Mohammed Dewji anawekeza fedha na ameonyesha utayari wa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Simba. Hili ni jambo sahihi na linalofanyika katika wakati sahihi pia. 

Ni jambo la kimapinduzi ambalo kwa kweli kila Mwana Simba anayo kila sababu ya kuliunga mkono. Wengi walipinga zile nyakati za timu kuendeshwa kwa kubahatisha. Mambo yanatakiwa yaishe ya watu wachache kuombwa fedha mara kwa mara wakati Ligi Kuu inaendelea. 

Simba ambayo ni kampuni mpya yenye kumilikiwa na wanahisa ambao ni wanachama, inayo sababu ya kutambua kuwa fedha ni matokeo. Isiwe eti kwamba wanachama wameshangilia kuingia kwa Mo Dewji wakidhani fedha ndiyo utatuzi wa kila kitu. 

Ni kweli fedha inatakiwa ili mahitaji mengi ya klabu ya hadhi ya Simba yaweze kufanikishwa. Ninachokiona kikihitajika kuwepo tena mapema sana ni uwekwaji wa mfumo imara wa uendeshaji. 

Watu wa masoko wapewe kazi zenye kuhusiana na masoko. Watu wenye taaluma za habari wapewe uhuru wa kufanya kazi kwa kuzingatia miiko ya habari. Watu wenye kazi ya kumalizia ujenzi wa eneo la Bunju ‘B’ wawe ni wenye kuielewa taaluma ya masuala ya ujenzi kwa mapana yake. Kocha mkuu wa kikosi cha kwanza apewe uhuru kamili bila ya kuingiliwa. 

Simba yenye kumilikiwa na wanahisa si tena mali ya wachache ambao wanatumia fedha zao mara kwa mara halafu wanakuja kudai baadaye. Mwanachama ni mwanahisa, si mtu wa kushangilia wala kubakia kuwa mshangiliaji au mzomeaji wa uamuzi unaofikiwa kwenye mkutano mkuu. 

Hadhi ya uanachama huwa inapandishwa viwango katika timu ambazo wanahisa huwa na haki ya kufahamu kwa undani nini kinaendelea katika klabu waipendayo. Ndiyo sababu ya uwepo wa umuhimu kwa wanahisa hawa, kufahamu kuwa fedha peke yake si msingi wa maendeleo. 

Kilicho muhimu ni mipango sahihi inayofanyika wakati timu ikiwa na muundo wa usimamiaji wenye kuzingatia nidhamu kubwa. Manchester United imekuwa ni klabu inayotumia fedha nyingi kwenye manunuzi ya wachezaji, lakini inajikuta ikishindwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, matokeo yake makocha wanafukuzwa na fedha nyingine nyingi zinakwenda katika kulipia gharama za uvunjaji wa mikataba. 

Simba inatoka katika hali ya kuwa klabu ambayo inaweza kutajirisha wachache kwa sababu ni mali ya umma na inaingia katika hali ya kisasa zaidi. Wanachama waujue umuhimu wa hisa zao, iwe zimenunuliwa na Mo Dewji au iwe zimenunuliwa na wao wenyewe. 

Wakishakuwa na ufahamu wa wao ni kina nani ndani ya Simba ya kisasa, basi watajua kuwa maoni na fikra zao ni vitu muhimu sana, tena ndani ya muda wowote ule. Lakini kwanza klabu itambue kuwa fedha bila ya busara na nidhamu ya usimamiaji wa masuala ya timu, haziwezi kuwa na msaada wala umuhimu. 

Huu ni wakati ambao kwa ushirikiano wa Wana Simba wote, ni bora ukaandikwa mpango mkakati utakaomjulisha kila mdau kuhusiana na nini matarajio ya timu katika muda mfupi na mrefu ujao.

Fukuza fukuza

Tayari mambo ndani ya Simba yameanza, kwani wameiga yale ya Yanga kwa kuanza timua timua, kuanzia kocha mpaka wachezaji.

Hauwezi kuingilia, ila kwa suala la Kocha Patrick Aussems, kuna gundu lisilo gundu ambalo linaonekana moja kwa moja kwa kuonekana kocha huyo hafai.

Aussems kama atabaki Simba ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu na uhakika mkubwa mpaka kuanzia Januari 4, mwakani ataanza kuondolewa.

Wanaogopa kwa sasa, lakini lazima afukuzwe. Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda hataki kuingia kwa undani juu ya hili, lakini ana kitu anaficha.

“Tunataka kumhoji kwa mambo kadhaa, kama mambo yote yakiwa tayari tutaweka hadharani,” amesema Kaduguda wakati timu ikiwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi.

Mo Dewji

Uhakika ni kwamba kazi ya Aussems imeshikiliwa na bilionea wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye ana uamuzi uliochukuliwa na bodi ya wakurugenzi.

“Mapendekezo yote yapo kwa Mo, yeye anatakiwa awe na jibu moja tu, ‘ndiyo’ au ‘hapana’, kuhusu Aussems,” amesema mmoja wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi aliyeomba hifadhi ya jina.

Senzo Mazingisa

Huyu ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, ambaye anajua kila kitu, ila anakataa yote juu ya Aussems na kudai ndiye kocha mkuu na kusisitiza kila kitu kitajulikana tu.

“Kuna vitu tunataka kujua kutoka kwake, ila ndiye kocha wetu na ninalolijua ndilo hilo,” amesema Mazingisa ambaye kuna uhakika anatafuta makocha kutoka Afrika Kusini waje kuifundisha timu hiyo.

Ushauri

Ingizo la fedha za Mo Dewji pamoja na zile zinazotoka kwa wanahisa wengine ni ishara ya mwanzo mpya ndani ya Simba. Lakini  busara ya Mwalimu Nyerere isipuuzwe hata kidogo. Fedha si msingi wa maendeleo. Ikiwa na maana haiwezi kubadilisha yote kwa wakati mmoja.

By Jamhuri