Taarifa kwamba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, kumtaka aliyekuwa mgombea wa urais wa CCM, Bernard Member kufika ofisini kwake kujibu tuhuma za kuendesha mikakati ya “kukwamisha” juhudi za Rais John Magufuli zimepandisha kidogo joto la kisiasa, zimetawala mijadala.

Kisichoelezwa wazi katika tuhuma hizo ni kuwa Membe anafanya mikakati ya kumuengua Rais Magufuli kuwa mgombea wa urais wa CCM mwaka 2020, ingawa zipo taarifa nyingine ambazo zimeyasema hayo kwa uwazi zaidi.

Hatutapata ushahidi wa kimahakama kubaini ukweli wa tuhuma hizi. Lakini tunafahamu siasa ni vita na kila mbinu hutumika kummaliza adui. Kwa hiyo inawezekana kabisaMembe amesukiwa zengwe la kumpunguzia kasi.

Lakini ukweli au uongo si jambo muhimu sana kwenye siasa. Muhimu zaidi ni nini matokeo ya huo ukweli au uongo. Wapigakura watafikia uamuzi bila kuwapo ushahidi wa kimahakama na watafanya uamuzi au kuimarisha au kudhoofisha malengo yaliyokusudiwa.

Kama yanayosemwa ni kweli yanaweka msingi mpya kabisa wa jinsi gani CCM inabadilisha viongozi wake wa ngazi ya juu. Mabadiliko si jambo la ajabu kwenye siasa. Ni mabadiliko bila maandalizi ambayo huamsha matatizo ambayo hatuwezi kutabiri yataleta athari zipi.

Rais wa CCM aliyepo madarakani katika awamu yake ya kwanza huteuliwa tena na chama chake, bila upinzani, amalizie ngwe ya pili ya urais. Anaenda kulala kila siku na changamoto lukuki za uongozi, lakini bila hofu kuwa yuko mwanachama mwenzake anawania nafasi yake.

Haijatokea mwanachama wa CCM kupata ujasiri na kutamka hadharani kubadilisha na kutelekezwa utaratibu huu. Atakayefanikiwa atafanikisha mapinduzi ya bila kumwaga damu. Ingawa tofauti kidogo, itatukumbusha alivyoondolewa Rais Mugabe madarakani.

Wapo wanaoamini kuwa kitendo chochote ambacho kinaweza kujibanza chini ya fasili ya “demokrasia” ni kitendo ambacho hakiwezi kuwa na kasoro yoyote. Hilo silikubali hata kidogo.

Ni kujidanganya kuamini kuwa tunaweza kupokea bila matatizo taratibu ya zile nchi ambazo mifumo yake ya siasa inaruhusu kumuondoa kiongozi madarakani halafu kesho yake akutane na aliyefanikiwa kumuondoa madarakani wanywe pamoja chai kwa vitumbua bila “aliyepinduliwa” kuwa na kinyongo.

Inawezekana kuwa tunaposhuhudia Rais Magufuli akipiga picha ya pamoja na marais waliomtangulia: Mwinyi, Mkapa, Kikwete, na ambao hawajakimbia nchi mpaka sasa, sababu moja iliyochangia ni waliyotangulia kuepushwa njama za kuenguliwa na warithi wao.

Tukikubali mapinduzi ya aina hii yatafurahisha mashabiki wa hiyo demokrasia, lakini tutaunda hali inayotuongezea makundi ya kisiasa yasiyo na tija. Baadhi ya wanasiasa na mashabiki wao wamejijengea uwezo mkubwa wa kuendeleza harakati za kushika hatamu zisizoisha.

Naielewa hofu ya CCM kuwepo makundi yanaofanya harakati hizi za kudumu. Si makundi ya kupuuzia. CCM inayo mifano kadhaa ya watu waliotumia muda na rasilimali kwa muda mrefu kujijengea mazingira na nguvu kubwa ya kujihakikishia kuteuliwa kuwa wagombea wa urais na kufanikiwa kuhujumu utaratibu rasmi wa chama hicho wa kumpitisha mgombea.

Anayeongoza harakati hizo, hasa kama ni kiongozi tayari, anaweka jitihada kubwa zaidi za kupamba wasifu wake kuliko kuchukua uamuzi ambao utaleta manufaa mapana zaidi. Aidha, hawezi kufanya hivyo kwa kumsifia aliye madarakani la sivyo haitakuwapo sababu ya kumuunga mkono. Matokeo, kwa vyovyote, hayatakuwa mazuri zaidi ya kujenga makundi na uhasama wa muda mrefu.

Siasa hubadilika. Hata utamaduni wa uongozi pia hubadilika. Inawezekana kufikia hatua ya kubadilisha viongozi kama Italia ambayo kati ya mawaziri wakuu 58, 18 kati ya hao wameshika wadhifa kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Tukifikia hatua hiyo kwa kufuata mlolongo wa kawaida wa kubadilika kwa mazingira ya kisiasa na mabadiliko ya mitazamo ya jamii juu ya uongozi haitakuwa jambo baya. Kushabikia tu dhana ya demokrasia bila kutafakari mazingira tuliyonayo na bila kuchambua wapi inatupeleka ni kukumbatia ujinga.

590 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!