CCM yashinda Siha, Kinondoni “Zaidi ya wapiga kura laki tatu wasusia”

*Zaidi ya wapiga kura laki tatu wasusia

DAR ES SALAAM

NA WAANDISHI WETU

Wagombea wa Chama Cha Mapinduzi, katika uchaguzi mdogo uliofanyika katika majimbo ya Siha na Kinondoni, wameibuka washindi. Jimbo la Siha, Dk.Godwin Mollel ametangazwa mshindi, huku Kinondoni akitangazwa Maulid Mtulia.

Wabunge hao wateule, wanarejea bungeni kwa mara nyingine baada ya kujivua uanachama wa vyama vyao vya awali, Dk. Mollel alikuwa Mbunge wa Siha, kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na Mtulia alikuwa mbunge wa jimbo la Kinondoni kupitia Chama Cha Wananchi-CUF.

Katika jimbo la Siha idadi ya waliojitokeza kupiga kura ni 32,277, kura halali ni 31,960, zilizoharibika 317 huku idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura ni 55,315. Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Godwin Mollel ameshinda kwa kura 25,611 dhidi ya mgombea wa Chadema Elvis Mossi aliyepata kura 5,905.

Wakati huo huo, katika jimbo la Kinondoni, mgombea wa CCM, Maulid  Mtulia, ametangazwa mshindi katika uchaguzi huo mdogo baada ya kupata kura 30,247 kati ya wapiga kura 44,500 waliojitokeza kutimiza haki yao ya kidemokrasia.

Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempa haki kila raia aliyetimiza umri wa miaka 18 kupiga kura.

Kwa mujibu wa vifungu vya 13(1), 13 (2), 35C, 61 (3) (a) na 63(1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 38 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) Sura ya 292.

Sifa za mtu kupiga kura ni lazima awe amejiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura, kadi ya mpiga kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuwa katika kituo alichojiandikisha kupiga kura.

Hata hivyo takwimu zinaonesha wapiga kura waliokuwa wameandikishwa katika jimbo la Kinondoni ni 355,131. Idadi hiyo ya waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura ikilinganishwa na waliojitokeza inaacha maswali mengi kwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo mdogo pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Idadi hiyo ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam, kunatoa dalili mbaya katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa, utaofanyika mwakani.

Katika Jimbo hilo jumla ya wapiga kura 355,131 ndio waliandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na waliojitokeza kupiga kura ni zaidi ya 44,500 kwa jimbo zima.

Vituo vyote vya kupigia kura vilikuwa na idadi ndogo sana wapiga kura, mfano kwa vituo vyote vilivyotembelewa na gazeti la JAMHURI ikiwemo kituo cha Mwangaza, Shule ya Msingi Kijitonyama Kisiwani, kituo A2, kituo namba 1, CCM ilipata kura 42, Chadema 22 na CUF kura 2.

Katika kituo hicho idadi ya wapiga kura walioandikishwa walikuwa 477 lakini waliojitokeza ni 67 tu, Kituo namba 2, CCM walipata kura 69, Chadema 28, CUF 0. Waliopiga kura 99, walioandikishwa 478.

Hali ilikuwa kama hivyo katika vituo vyote vilivyotembelewa na gazeti hili, huku idadi kubwa ya askari polisi ikionekana katika kila kituo huku wakiwa wamejiandaa kwa lolote ambalo lingeweza kujitokeza.

Mkazi wa Kata ya Hananasifu (Kisutu), Patrick Samba ameliambia gazeti la JAMHURI, amekata tamaa kutokjana na namna siasa za vyama zinavyokwenda hivyo hakuona sababu ya kwenda kupiga kura.

Samba amesema, licha ya lawama nyingi kupelekwa kwa Jeshi la Polisi, bado Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijaweka mazingira mazuri ya chaguzi mbalimbali nchini.

“Hapa watu wa eneo hili bado tumejawa na majonzi yaliyokana na kupigwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilin aliyeuawa wiki iliyopita wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana,” amesema.

Amesema kwa kawaida mtu anapoona damu ya mtu inapomwagika hali inakuwa tofauti kabisa, na hii ndio sababu nyingine ya watu wengi kushindwa kujitokeza kupiga kura.

Naye Ibrahim Kufakunoga, mkazi wa Hananasifu amesema wingi wa polisi waliokuwa kwenye vituo hivyo wakiwa na silaha za moto nao pia umechangia kuwatisha    wapiga kura.

Mkazi wa Mwananyamala Kisiwani, Maulid Hassan ameliambia gazeti la JAMHURI kuwa kwa sasa nchi inahitaji Katiba Mpya ambayo italinda demokrasia na uhuru wa watu kutoa michango ya mawazo yenye staha bila kujengewa mazingira ya hofu.

Hassan amesema hali iliyojitokeza katika uchaguzi uchaguzi huo mdogo na chaguzi nyingine zilizopita haioneshi uhalali wa kazi za siasa katika mfumo wa vyama vingi nchini.

“Kama watu tunajengewa hofu hata ya kutoa mchango wa mawazo yetu kwa maana ya kuingizwa katika tuhuma za kashfa, na hili la kumwaga askari wengi kutoka mikoa mitatu linaonesha hali halisi ya nchi ilivyo kwa sasa,” amesema.

Anderson Richard Mkazi wa Kinondoni Biafra amesema kutokana na ugumu wa maisha kwa wapig kura wengi     Kinondoni, baadhi wameona hakuna sababu ya kushiriki uchaguzi kwasababu hauwezi kuwafanya kuwa na maisha bora.

Richard amesema hakuona umuhimu wa kwenda kupiga kura kutokana na kile alichokiita mabavu ya askafri polisi ambao walikuwa walinzi wa amani katika uchaguzi huo mdogo.

Yaliyotokea katika uchaguzi 

Kituo cha Mwananyamala Shule ya Msingi A3 kilichokuwa na wapiga kura 355 ndicho kilichoonekana na idadi kubwa ya watu waliopiga kura ni 350, huku CCM ikipata kura 348, Chadema ikiambulia kura 1.

Katika kituo hicho hicho CCK awali inaonekana iliambuli kura moja na baadaye kufutwa na kuwekwa kura mbili jambo ambalo linatiliwa shaka na wapiga kura lakini matokeo haya nayo yamefutwa.

Mawakala kutopewa barua za utambulisho mapema na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hadi upigajia kura ulipokuwa unaendelea huku wengine kuzuiliwa na wasimamizi, inatajwa kama sababu ya uchaguzi huo kutiliwa shaka na wapiga kura.

Vyama vyashindwa kushawishi wapiga kura

Andrew Bomani, Kaimu Katibu Mwenezi wa chama cha UDP amesema, vyama vya siasa vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Kinondoni havikuhamasisha watu vya kutosha ndiyo maana watu wamejitokeza kwa uchache katika uchaguzi huo.

Akilinganisha idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi huo na chaguzi nyingine zilizopita amesema ni aibu kwa vyama vyote vya siasa hapa nchini kuendelea kupoteza wapiga kura kwa kukosa hoja na ushawishi kwa wapiga kura wao.

Amesema kitendo cha aliyekuwa  Mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF kabla ya kujiondoa kwenye chama hicho, na kugombea ubunge tena katika jimbo hilo hilo kupitia chama cha CCM kimewakatisha tamaa wapiga kura wengi  katika jimbo hilo.

Ameongeza kuwa idadi ndogo ya wapiga kura kwa upande mwingine inachangiwa na watu kupuuzia chaguzi hizo kwasababu baadhi zinajitokeza pasipo sababu za msingi hivyo wanaona hawana sababu ba kupoteza muda.

Profesa Safari awalaumu polisi

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Profesa Abdallah Safari, amesema, watu wa Dar es Salaam wana akili sana ndiyo maana wameususia uchaguzi huo.

Amesema tukio la askari polisi kuwashambulia wanachadema na kusababisha kifo cha mtu mmoja siku moja kabla ya uchaguzi yamesababisha idadi ya wapiga kura wengi kuhofia kujitokeza katika upigaji kura.

Prof. Safari, amesema askari polisi wa hapa nchini wanashika nafasi ya tatu kwa ukatiri barani Afrika  kwa sababu ya maovu ambayo wamekuwa wakiwatendea wapinzani na wafuasi wao hasa kwenye chaguzi ndogo.

Amesema kitendo cha polisi kujaa kila kona ya jimbo la Kinondoni siku ya kupiga kura kilikuwa na ishara ya kuwaogopesha wapiga kura. Prof Saafari amesema wanaopaswa kulaumiwa ni CCM na serikali nzima kutumia askari polisi kwa jambo ambalo lilipaswa kufanyika kidemokrasia na kwa uhuru zaidi.

Safari amesema kutokana uchaguzi huo kugubikwa na upendeleo mkubwa uliokuwa ukifanywa na wasimamizi wa uchaguzi huo katika vituo vingi vya kupigia kura ni muda sasa wa kudai kwa nguvu Tume huru ya uchaguzi.