Chadema yahofia wapiga kura wachache

NA WAANDISHI WETU
Takribani siku nne kabla ya kufanyika uchaguzi mdogo katika majimbo ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro, hofu ya kujitokeza
wapiga kura wachache imeibuka kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHDEMA).
Mgombea ubunge katika jimbo la Kinondoni (Chadema), Salum Mwalimu,
amesema hofu hiyo inatokana na matukio yaliyoibua dhana ya kuwapo wizi wa
kura, hivyo baadhi ya watu kutokuwa tayari kujitokeza.
Mwalimu amesema hofu ya wananchi kutojitokeza kwa wingi kupiga kura ni jambo
lenye umuhimu lililojadiliwa pia na Kamati Kuu ya chama hicho, ili kupata namna
bora ya kukabiliana nalo hususani wakati wa kampeni.
Amesema miongoni mwa uamuzi uliofikiwa kukabiliana na hofu hiyo ni
kuuhamasisha umma hususani wakazi wa Kinondoni na Siha ili wajitokeze kwa
wingi siku ya uchaguzi na kuhakikisha wanalinda kura zao.
Amesema Chadema kwa kushirikiana na vyama washirika wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), imejiandaa kushiriki uchaguzi huo kwa lengo la kupata
ushindi.
“Tumejiandaa kuanzia majukwaani na kampeni za nyumba kwa nyumba ili
kuwashawishi wapiga kura watupatie ushindi,” amesema.
Vipaumbele vyake
Mwalimu amesema akichaguliwa kuwa mbunge wa Kinondoni, atawekeza katika
kipaumbele cha kuboresha mazingira ya uchumi mdogo kwa wananchi wa jimbo
hilo.
Amesema vijana wengi wa Kinondoni jimboni humo wanajihusisha na biashara
ndogo-ndogo ili kupata fedha za kujikimu kimaisha.
Mwalimu amesema kwa kushirikiana na wachumi waliopo ndani na nje ya
Chadema, atahakikisha vijana na wanawake wanajiunga ama kuimarisha vikundi
vya ujasiriamali ili kupata mikopo itakayokuza mitaji yao.
Kwa mujibu wa Mwalimu, hatua hiyo itajumuisha urasimishaji wa biashara ili
kuviwesha vikundi hivyo kukopesheka.
Eneo jingine la kipaumbele kwa Mwalimu ni uboreshaji wa makazi ya watu
wakiwamo wanaoishi kuzunguka mto wa Ng’ombe.
Mwalimu amesema uboreshaji wa huduma za afya na kuchagiza kasi ya
kuwezesha kila kata ya jimbo hilo kuwa na kituo cha afya kwa mujibu wa Sera ya
Taifa ya Afya, ni miongoni mwa mambo ya msingi kuyashughulikia ikiwa
atashinda ubunge.
Haki ya kugombea

Amesema hoja inayoenezwa na washindani wake kwamba hafai kuchaguliwa kwa
vile si mkazi wa jimboni humo haina mashiko.
Amesema ni mkazi wa Kinondoni aliyezaliwa katika eneo la Morocco alipokuwa
akiishi na wazazi wake.
Mwalimu anasema wanaoeneza propaganda kwamba ni Mzanzibari asiyekuwa na
haki ya kuchaguliwa wanapaswa kupuuzwa kwa vile licha ya kuwa ni mzaliwa wa
jimboni humo, lakini ana haki zinazopingana na ubaguzi unaojidhihirisha kwa
washindani wake wa kisiasa.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya
67 (1), mtu atastahili kuchaguliwa kuwa mbunge iwapo ana sifa za kuwa raia wa
Tanzania, mwenye umri wa miaka 21 au zaidi.
Mwalimu amesema sifa nyingine ni awe anajua kusoma na kuandika kwa
Kiswahili na Kiingereza, mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama
cha siasa chenye usajili kamili.
Pia anasema sifa nyingine ni hajawahi kutiwa hatiani na Mahakama kwa kosa la
kukwepa kulipa kodi katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.
“Sifa zote hizo ninazo, ninachowaomba wapiga kura wa Kinondoni ni kuniamini ili
niwe mtumishi na mwakilishi wao,” amesema Mwalimu.
Uzoefu katika siasa
Amesema uzoefu alioupata ndani ya Chadema hadi kufikia kuwa Naibu Katibu
Mkuu (Zanzibar) mwaka 2014 hadi sasa, unatosha kutekeleza majukumu ya
kibunge.
CUF yaonya wizi wa kura
Mgombea ubunge wa Kinondoni kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Rajab
Juma, amesema mikakati inayopangwa kufanikisha wizi wa kura, haitafanikiwa
kwa vile wamejipanga kuidhibiti kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Akizungumza kupitia kwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa
Umma wa CUF (anayeumuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba), Abdul
Kambaya, amesema wamejizatiti kudhibiti wizi wa kura na kwamba chama
kinachotarajiwa kutangazwa ‘ushindi wa bao na mkono’ hakitafanikiwa.
Amesema mgombea wa CUF anafaa kuchaguliwa kwa vile anafuata imani
na itikadi ya chama hicho inayojikita katika kusimamia rasilimali za umma.
“Hii ni tofauti na mbunge aliyetangulia ambaye hakutaka hata kutumia ofisi yake
na kuamua kupanga chumba sehemu nyingine,” amesema.
Bomoabomoa
Amesema Juma akishinda nafasi hiyo, atasimamia sheria na haki za watu
ikiwamo ubomoaji holela wa nyumba za watu jimboni humo.
Amesema mbunge aliyetangulia, kujiuzulu kisha kuteuliwa na CCM kuwania kiti
hicho, Mtulia aliwatetea wananchi wanaobomolewa makazi yao hususani katika
kata ya Kinondoni inayoongoza kwa makazi hatarishi, lakini hawezi kufanya hivyo
akiwa ndani ya CCM.

Elimu na afya
Amesema elimu ni kipaumbele cha mgombea wa CUF ili kujenga mazingira
mazuri kwa watoto na wananchi wengine kupata elimu bora.
Amesema watahakikisha kuwa kila mwanafunzi katika shule za jimboni humo,
anapata walau mlo mmoja kwa siku.
Kambaya amesema kama Mwalimu Julius Nyerere aliweza kufanya hilo huku
wanafunzi wakipewa vitabu na madaftari bure, mgombea wao hawezi kushindwa
kufanikisha azma ya kupatikana kwa mlo mmoja kwa siku kwa wanafunzi jimboni
humo.
Amesema fedha zitakazotumika kuboresha elimu ni zile za mfuko wa jimbo. Pia
ametaja kipaumbele kingine kuwa ni uboreshaji wa sekta ya afya.