Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Rukwa, kimemfuta uanachama na kumvua udiwani, Dickson Mwanandenje aliyekuwa diwani wa kata ya Majengo wilaya Sumbawanga mkoani hapa.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa huo, Shadrack Malila maarufu Ikuwo amesema leo Agosti 11 kuwa Baraza kuu la Chadema mkoa wa Rukwa lililokutana jana limeridhia kwa kauli moja kumfuta uanachama diwani huyo.

Amesema sababu ya kumfuta uanachama diwani huyo, ni usaliti ndani ya Chadema.

Amesema mara ya mwisho alipanda jukwaani katika mkutano wa hadhara wa mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly na kumsifia mbunge huyo na chama chake (CCM).
“Sisi tuna ushahidi wa kutosha kupitia ‘Clip’ alishiriki mkutano wa Mbunge wa CCM katika kata ambayo sio ya kwake (Mazwi) na kummwagia sifa mbunge huyo kwamba ameleta maendeleo kwenye jimbo hilo hususani kata ya majengo inayoongozwa na Mwanandenje, kitu ambacho sisi tumetafsiri ni usaliti”amesema.
Amesema kuwa kupitia taarifa za kiintelejensia wamebaini alikuwa kwenye mipango ya kujiunga na CCM kwa dau la zaidi ya Sh 20 milioni hivyo walikuwa kwenye mazungumzo ya mwisho na walipanga kumtangaza katika moja ya mikutano yao ya kisiasa.

Akizungumzia taarifa hizo Mwanandenje amesema kuwa yeye hana taarifa ya kufutwa uanachama wa Chadema japo amesikia tu mitaani.

Akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwake, Mwanandenje amesema kushiriki mkutano wa Mbunge sio dhambi ya kufanya avuliwe uanachama na hizo za kuwa katika mchakato wa kujiunga na CCM zimejaa ukakasi tu.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Njovu alipohojiwa amesema amezisikia taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii lakini kama zitawasilishwa rasmi ofisini kwake ndipo wataangalia kanuni na taratibu zinasemaje kama chama kikimfuta uanachama diwani wake.

By Jamhuri