Siku 10 baada ya kutokea ajali iliyokatisha ndoto za wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya St. Lucky Vincent, JAMHURI limefanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo na kubaini mambo ya kutisha.
Mmoja wa madereva wakongwe wa shule hiyo, Hamis Omary (59), ambaye amekuwa dereva katika shule hiyo kwa miaka saba sasa, ameliambia JAMHURI kuwa yeye alikuwa miongoni mwa madereva waliohusika kusafirisha wanafunzi siku hiyo.
Omary amesema siku ya tukio kulikuwa na magari matatu, yaliyotoka shuleni St. Lucky Vincent kwenda Karatu. Gari analoendesha yeye T 407 AZG lilikuwa la kwanza kuondoka katika msafara huo, na waliondoka bila kuachana umbali mrefu.
Gari lililopata ajali namba lenye namba za usajili T 871 BYS, lilikuwa likiendeshwa na dereva anayemkumbuka kwa jina moja la Dismas, ambaye naye alipoteza maisha katika ajali hiyo na gari la tatu ni lenye namba ya usajili T 752 BHU lililokuwa la mwisho.
Omary ameliambia JAMHURI kuwa waliondoka vizuri kuelekea Karatu, huku yeye akiwa wa kwanza kufika Shule ya Tumaini, ambako wote walitakiwa kufika kwa ajili ya kufanya mitihani ya ujirani mwema, lakini muda mfupi baada ya kufika shuleni hapo alipigiwa simu na mmoja wa walimu kuwa gari la pili limepata ajali katika Mlima Marera hivyo hivyo akawashusha wanafunzi na kurejea eneo la ajali kutoa msaada.


“Niliacha wanafunzi pale shuleni, nikaondoka na gari langu likiwa tupu… nilipofika pale nilistushwa na nilichokiona maana gari lilikuwa korongoni na wanafunzi walikuwa wameanza kutolewa na kulazwa barabarani.
“Kuangalia vizuri nililiona gari la Issa likiwa limepaki huku wanafunzi waliokuwa kwenye gari hilo wakipiga makelele. Wakati huo Issa alikuwa anasaidia kuokoa wahanga wa ajali.
“Kwa utu uzima wangu jambo la muhimu pale ilikuwa ni kuwaondoa wale watoto ili wasiendelee kushuhudia lile tukio linaloendelea mahala pale. Nilichukua funguo za gari na kuendesha hilo gari la Issa mpaka shule ya Tumaini.
“Huko njiani ilinilazimu kuongea na watoto na kuwaeleza kuwa wenzao ni wazima hivyo watulie, lakini ilikuwa kazi kubwa. Nilipofika shule niliomba wanafunzi wale walioshuhudia ajali ile wasichanganywe na wenzao kwanza maana hawakuwa wakijua kitu, waliposhuka wote niliondoka na lile gari kurudi eneo la ajali na baada ya kumalizika zoezi la kuondoa wanafunzi wote kila mmoja alichukua gari lake wote tukaelekea shule ya Tumaini,” Omary ameliambia JAMHURI.


Omary amesema, waliondoka shule ya Tumaini, kurudi jijini Arusha baada ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliopata ajali wameondolewa katika eneo la tukio jambo lililoleta nafuu ya kisaikolojia kwa wanafunzi waliobaki.
Dereva huyo mzoefu, hakusita kutoa pongezi kwa namna watu walivyojitolea kuokoa maisha ya wanafunzi, huku akieleza kwa masikitiko kuwa huduma zote zilizotolewa hazikusaidia kuokoa maisha ya wanafunzi walio wengi, maana tayari walishafariki.
Akizungumza kuhusu dereva mwenzake aliyefariki katika ajali hiyo (Dismas), amesema alikuwa amekafikisha mwaka mmoja tangu ajiunge shuleni hapo kama dereva. Amesema kijana huyo hakuwa mlevi, wala mvuta sigara, isipokuwa mtu anayependa kufanya ibada.
Amesema gari lililopata ajali halikuwa na hitilafu yoyote na kuongeza kuwa lilinunuliwa na shule hiyo mwaka jana.


Omary ameliambia JAMHURI, ajali hiyo imemuachia taswira mbaya kichwani mwake, huku akikiri kuwa ni vigumu taswira hiyo kuondoka kichwani mwake kwani wanafunzi waliokuwa alikuwa amezoea kuonana na kutaniana nao kama wajukuu zake.
Wakati yeye akihimili taswira hiyo mbaya, hali ni tofauti kwa dereva mwenzake aitwaye Issa, aliyeshiriki katika uokoaji miili ya wanafunzi waliokufa. Kwa sasa yuko kwenye wakati mgumu kutokana na kuweweseka mara kwa mara.
“Issa alipata mshtuko mkubwa kwa sababu mtoto mmoja wa kike aliyembeba kumtoa kwenye gari iliyopata ajali alikuwa amepasuka kichwa na ubongo unamwagika… Jambo hilo limemchanganya sana akili. Amechanganyikiwa kabisa na anaweweseka. Kuna kipindi anaweweseka kutokana na hali hiyo. Tunajitahidi kumshauri, lakini bado hali hiyo haimuondoki,” amesema Omary.

Mwalimu Mkuu Tumaini azungumza
JAMHURI limezungumza na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tumaini, Paul Indimuli akiwa shuleni kwake Karatu ambaye amesema kutokea kwa ajali hiyo kumewaathiri.
Indimuli amesema, walipopata taarifa kwamba wanafunzi wamepata ajali, walipatwa na ganzi.  Mwalimu Indimuli amesema walichukua hatua ya kuwatenga wanafunzi wa St. Lucky Vincent na kuwaweka chumba cha maktaba ya shule hiyo wasichangamane na wanafunzi wa shule nyingine waliokuwa wamefika shuleni hapo kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema.
“Tukio hili lilituuma sana kama shule. Ule mtihani uliokuwa ufanyike haukuweza kufanyika maana isingewezekana tena. Shule nne za mkoa wetu ndizo zilikuwa zinashiriki kufanya mtihani huu ambazo ni Costiga English Medium, Charm English Medium hizi ni za hapa Karatu, St. Lucky Vincent pamoja na shule yetu ya Tumaini.


“Wanafunzi wote wa shule za Costiga na Charm walikuwa tayari wamefika hivyo tulikuwa tunawasubiri wa St. Lucky Vincent, ili mitihani ianze. Lakini baada ya ajali ilibidi tukae na kuongea na wanafunzi waliotakiwa kufanya mtihani nao wakaruhusiwa wakaondoka tukabaki na wanafunzi wa St. Lucky Vincent tu,” amesema Mwalimu Indimuli.
Amesema shule yake pamoja na St. Lucky Vincent, zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu kuanzishwa kwake, mwaka 2004 na kupata usajili mwaka 2005 wamekuwa wakishirikiana na shule za Mkoa wa Arusha.
Mwalimu Indimuli, ameliambia JAMHURI, wanafunzi waliopata ajali na kupoteza maisha, tangu wakiwa darasa la sita (mwaka jana) wamekuwa na ukaribu na wanafunzi wenzao wa Tumaini wakishirikiana kimasomo na hata wanapopata safari za kimafunzo ambazo huwalazimu kupita Karatu wamekuwa wakifika kwanza shuleni hapo kisha kuendelea na safari.
Kuhusu mitihani ya ujirani mwema, amesema wamekuwa na utaratibu wa kufanya mitihani ya ujirani mwema kila mwaka ambayo imekuwa ikisaidia kuboresha na kuinua taaluma kwa wanafunzi husika ikiwa ni pamoja na kufahamiana na wanafunzi wa shule nyingine.

Kibali cha safari
Mwalimu Indumuli, amesema kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kuandaa ratiba ya masomo ya mwaka ambayo huwasilishwa Ofisi ya Kata na wilayani ambayo inakuwa inaeleza ratiba ya kuinua elimu pamoja na ziara za kitaaluma.
Amesema miaka yote baada ya kuwasilisha ratiba hiyo wamekuwa wakiendelea kutekeleza ratiba hiyo ikiwa ni pamoja na kusafiri bila kutakiwa kuwa na kibali kwani ofisi husika huwa na taarifa.

“Hatujawahi kuambiwa suala la kupata kibali cha masomo. Tumekuwa tukisafiri mara nyingi sana na mwaka jana tulikuwa Jijini Arusha kwa siku tatu na shule za Arusha zinakuja huku. Machi 18, mwaka huu shule ya Kilimanjaro English Medium, Mecsons English Medium na Dominion zilikuja zikafanya mtihani na kuondoka, hili la kibali ndio nalisikia sasa,” amesema Mwalimu Indimuli.

Madhara ya ajali
Mwalimu Indimuli amesema kutokana na ajali hiyo shule yake imesitisha safari zote za kimasomo zilizokuwa zimepangwa kufanyika mwaka huu ikiwa ni pamoja na mitihani ya ujirani mwema.
“Ajali hii imetukatisha tamaa, hatujui kama tutaweza kusafiri kwani kwa mwaka huu haitowezekana, tumeanza kushindanisha wanafunzi wetu wenyewe kwa wenyewe kimkondo,” amesema Mwalimu Indimuli.
Mwalimu huyo ameliambia JAMHURI, siku tatu za kwanza baada ya ajali kutokea, wanafunzi wa Tumaini hawakuwa na utayari wa kusoma, hivyo iliulazimu uongozi wa shule kufanya juhudi za kuzungumza nao ili kuwajenga kisaikolojia ikiwa ni pamoja kuwapatia siku moja ya mapumziko.
“Sasa baada ya kuanza kufanya maombi na viongozi wa dini pamoja na watu mbalimbali wanafunzi wameanza kutulia hivyo tumeanza kwa kuwapatia mitihani ya majaribio ambayo wanaifanya kwa vikundi, baada ya hapa ndio tutaanza kuona njia,” amesema Indimuli.
Upendo Joel (37) mkazi wa Karatu, ameliambia JAMHURI, tangu kutokee ajali hiyo hajisikii tena kusafiri wala kuruhusu watoto wake kusafiri kwani ameingiwa na woga.
“Hapa nilipo natamani muda wote niwe nawaona wanangu. Wakae karibu yangu, lakini ni jambo ambalo ni gumu kwani mimi ni mfanyabiashara ndogo ndogo na siwezi kutembea na watoto wangu muda wote. Lakini ajali hii imetutikisa kuliko ajali nyingine zilizowahi kutokea. Mapenzi ya Mwenyezi Mungu yatimizwe maana ilishatokea hatuna jinsi zaidi ya kuwaombea malaika hao,” amesema Upendo.


Boaz Urio (45), amesema, ajali hiyo imetokea kwenye eneo ambalo halina historia ya ajali, na hiyo ni mara ya kwanza kutokea ajali katika mlima huo na kwamba hata mazingira ya ajali yanashangaza kwani eneo hatarishi walikuwa wameshalivuka.
“Dereva kama mimi nashangaa kuona ajali inatokea sehemu kama hiyo. Kama angepata ajali kona ya kwanza ningemuelewa, lakini pale ni ajabu kabisa maana sio miongoni mwa sehemu hatarishi.   Kama angepata ajali pale Kilima Tembo, pale Manyara, kwani pale ndipo pana historia ya kutokea kwa ajali,” amesema Urio.
Amesema ajali ile ilisababisha kusimama kwa shughuli zote Karatu watu wakakimbilia eneo la ajali na kusababisha vilio kwa wakazi hao ambao wameumizwa na vifo vya watoto hao.


JAMHURI limefanya mahojiano na Meneja wa Shule ya Lucky Vicent, Casmir Moshi, kuhusu athari zilizotokana na ajali hiyo, amesema kwa sasa ni vigumu kuzungumzia suala hilo kwani bado ajali inamuumiza.
“Nashindwa cha kukwambia… akili inazunguka hapa nilipo, siwezi kusema chochote kuhusu hilo kichwa kimevurugika kwa kweli. Pia mimi sio msemaji wa shule, isipokuwa ni msemaji huko huko ndani kwenye kikao na watu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra),” amesema Moshi.
JAMHURI lilitaka kufahamu iwapo magari ya kusafirisha wanafunzi ya shule hiyo kama yamektiwa bima na yamekatiwa bima ya aina gani.


Moshi amebainisha kuwa magari ya shule yote yana bima ya “third party” ambayo imekatwa kwa Kampuni ya Metropolitan (T). Lakini gari lililopata ajali halikuwa limekatiwa bima kwa kampuni hiyo kutokana na kununuliwa hivi karibuni hivyo kutobadilishwa nyaraka zake za bima.
Alipoulizwa darasa la saba lilikuwa na wanafunzi wangapi, amesema darasa hilo lilikuwa na wanafunzi 106, lakini baada ya ajali wamebaki na wanafunzi 74.
Kuhusu walimu waliofariki katika ajali hiyo amesema walikuwa walimu tegemeo kubwa kwa shule kutokana na maandalizi na juhudi zao katika ufundishaji wa masomo ya Kingereza na Sayansi.
“Unajua kuna vitu vinaumiza. Hawa walimu walikuwa na urafiki mkubwa na wanafunzi wao. Walimu hawa walipopanda kwenye basi wanafunzi wakaanza kugombea kupanda basi hilo hilo, hivyo wanafunzi ndio waliowafuata walimu mpaka ikafikia kuwapunguza kwani kila mmoja alitaka kupanda basi hilo.
“Lakini uzuri walielewa na safari ikaanza. Sasa wamejikuta wanapata ajali pamoja. Hili jambo linaumiza jamani,” amesema Moshi.


Sumatra imetuma timu ya wataalamu mkoani Arusha, ambao wamekuwepo humo kwa wiki moja sasa kuchunguza ajali hiyo na wataalamu hao wamekuwa na kikao na Shule ya St. Lucky Vincent ambacho kilifanyika, Ijumaa ya wiki iliyopita, shuleni hapo.
JAMHURI limeshuhudia jinsi timu ya wataalamu kutoka Sumatra makao makuu, Dar es Salaam, ilivyokuwa inahangaika kuzunguka katika ofisi mbalimbali ili kupata taarifa mbalimbali.
Ijumaa ya wiki iliyopita, timu hiyo ilifika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi, anayehusika na Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Nuru Selemani.
Majira ya mchana timu hiyo ilikuwa kwenye ofisi ya Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha (TRA) na kufanya kikao na Meneja wa TRA. Jioni timu hiyo ilikuwa katika shule ya msingi Lucky Vincent na kufanya mahojiano na uongozi na baadhi ya wafanyakazi wa shule hiyo ikiwa ni pamoja na Hamis Omary ambaye ni dereva wa shule hiyo.
Wataalam hao wa Sumatra walifika shuleni hapo majira ya saa 08:00 mchana na kuondoka saa 11:00 jioni.

Polisi
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kimesema kuwa wamebaini uzembe wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha (Tanroads) kutotimiza wajibu wake wa kuweka alama za barabarani kama inavyohitajika katika eneo ilipotokea ajali, huku wachunguzi wa mambo wakisema kutokuwepo kwa alama ni moja kati ya sababu zilizochangia ajali hiyo.
Eneo la mlima Merera, Tanroads hawakuwa wameweka alama yoyote ya tahadhari hivyo madereva wamekuwa wakipita kwa kutumia uzoefu jambo ambalo ni hatari kwa madereva wageni wa barabara hiyo.
“Tumeelezwa kwamba dereva huyu alikuwa mgeni katika barabara hiyo. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupita hapo. Lakini unapopita katika barabara hiyo ya Karatu baada ya kumaliza eneo la kijiji kuelekea mlima Merera unakutana na kibao kinachokuruhusu kuongeza mwendo kutoka 50 (mwisho wa spidi 50) hapo dereva anaongeza mwendo bila kujua mbele  kama kilometa 1.5 unakutana na kona kali kisha mteremko mkali, huu ni uzembe, na Tanroads. Baada ya kugundua hilo, huku ajali ikiwa imeshatokea wamekimbia kuweka alama katika eneo hilo,” amesema mtoa taarifa wetu.
Amesema kutokana na dereva kuongeza mwendo na kukutana na kona kali, gari lilimshinda na kuanza kuhangaika nalo na baada ya kufanikiwa kukata kona ndiyo ghafla akakutana na korongo hivyo kushindwa kulimudu gari na kutumbukia korongoni.
“Kitaalamu pia tunaita uzembe wa dereva, maana pamoja na uzoefu dereva anatakiwa kutumia akili wakati akiwa barabarani, lakini yeye ni kama alijikuta anapaniki kutokana na hali aliyokutana nayo. Hakuweza kutuliza akili yake ukizingatia pia alikuwa anakutana na changamoto ya hali ya hewa kutokana na kuwepo kwa ukungu katika eneo hilo hivyo kusababisha kutokuona vizuri,” amesema mtoa taarifa wetu.


Chanzo chetu kimesema, wanafunzi wote walikuwa wamekaa kwenye viti huku baadhi yao wakiwa wamefunga mikanda hivyo wakati wa uokozi baadhi ya mikanda ilikatwa na visu au panga kuwaondoa majeruhi na waliofariki katika eneo hilo la ajali.
Amesema baada ya kulifanyia ukaguzi gari lilisababisha ajali, hawakubaini ubovu wowote lilikuwa katika hali nzuri na dereva wake alikuwa anakidhi viwango kwa maana ya kupitia mafunzo yote ya udereva wa abiria.
Shule ya St. Lucky Vincent ilinunua kutoka gari hilo kutoka kwa mtu, ila baada ya kulinunua na kubadili kadi gari, ambao ndiyo huonesha umiliki, bima iliendelea kubaki katika umiliki wa muuzaji, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.
“Jalada tayari limeshapelekwa kwa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi ambazo ni kufikisha suala hili mahakamani, lakini sio suala kubwa hata kidogo haya ni mambo ya trafick kesi,” amsema.
JAMHURI limemhoji Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Nuru Selemani  aliyesema: “Jeshi letu lina utaratibu wake. Msemaji ni RPC hivyo wasiliana naye atajibu maswali yako yote kwani ndiye kiongozi wangu,” amesema SSP Selemani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishina Mwandamizi Msaidi wa Jeshi la Polisi, SACP Ilembo ameliambia kuwa JAMHURI jeshi hilo linamshikilia mmiliki wa shule ya Lucky Vincent. Hata hivyo,  taarifa zilizopo ni kwamba mmiliki huyo ameshafikishwa Mahakamani, tangu Ijumaa wa wiki iliyopita.
“Bado sijafikishiwa taarifa hivyo hapo siwezi kukujibu zaidi. Na huyo mmiliki wa shule yuko kituo cha Polisi Wilaya. Hao labda wana la kukwambia mimi sina,” amesema SACP Ilembo.
OCD wa Wilaya ya Arusha hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye si Msemaji.

Hospitali ya Mount Meru
JAMHURI limefika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru na kufanya mahojiano na Mganga Mfawidhi, Jacqueline Uriyo, aliyesema hospitali hiyo ilipokea majeruhi wanafunzi watatu, maiti za wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja.
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa kwamba kuna maiti tatu za wanafunzi ambazo hazijachukuliwa, amesema kwamba maiti wote walitambuliwa na ndugu zao na kwamba pia waliletewa nguo za kubadilisha kisha taratibu za kuwachukua zilifanyika kama ilivyokuwa imepangwa.
“Hizi taarifa kwamba kuna wanafunzi mzazi wao alifariki na wameshindwa kuchukuliwa si kweli, kwani wanafuzni wote ndugu zao walijitokeza, walileta nguo za kuwabadilishia na hakuna wanafunzi waliokuwa na majina ya ubini yaliyokuwa yakifanana, huu ni uongo unaoenezwa huko mtaani, lakini hapa kwetu tumebaki na hawa watoto wanaosubiri kwenda kupata matibabu zaidi nje ya nchi,” amesema Uriyo.


Alipoulizwa hali za watoto hao amesema wote wanaendelea vizuri na wanaweza kuongea na kuelezea tukio, lakini hospitali hiyo imeweka utaratibu wa kuwaona kutokana na kuhitaji muda mwingi wa kupumzika.
Mmoja wa Madaktari wa hospitali hiyo (Jina linahifadhiwa ) ameliambia JAMHURI katika uchunguzi uliofanywa kwa wanafunzi waliofariki umebaini kuwa wanafunzi hao walivunjika mifupa mingi mwilini.
“Kulifanyika Postmoterm lakini inasikitisha sababu ya vifo ilikuwa ni kuvunjika kwa mifupa mwilini, kila mmoja alivunjika si chini ya mara tano. Wapo wengine wakati wa kujiokoa walijikinga na mikono, lakini sababu ni impact iliyotokea.  Wapo ambao mpaka wanafikishwa hapa walikuwa bado wanachuruzika damu.
“Wapo waliopata majeraha ya ndani, lakini pia walivunjika vunjika, wengine vichwa viligongwa vibaya, wengine moyo. Ila wote 32 walikuwa wamevunjika mifupa kama nilivyokufahamisha hapo awali,” amesema mtoa taarifa.
Kuhusu majeruhi amesema Doreen amevunjika taya na kwamba ndiye aliyeumia zaidi kuliko Wilson na Saidia, lakini amekuwa imara na mwenye kumbukumbu nzuri ya tukio zima.
“Doreen ametueleza kwamba ajali hii aliiota kabla ya kutokea, na kwamba hata wakati wa kupanda magari alimkatalia rafiki yake kupanda basi moja, na hata alipoletwa hapa hospitali wote tulijua amekufa na hata vipimo vilionyesha hivyo, lakini ghafla alishtuka na madaktari wakaanza juhudi za kumuokoa. Doreen is fighter, huyu mtoto ana maajabu,” amesema.
Majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo ni Doreen, Saidia na Wilson.

 Mganga Mkuu wa Mkoa
Akizungumza na JAMHURI Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Vivian Wonanji amesema  Mkoa umeandaa utaratibu wa kukutana na waathirika wa tukio hilo la ajali kuwapatia matibabu stahiki yatakayotolewa kwa wiki moja.
Dk. Wonanji amesema tayari ofisi yake imewasiliana na wataalamu wa saikolojia 20 ambao wamejitolea kufanya kazi hiyo, 17 kati yao wanatoka Arusha, watatu wanatoka Dar es Salaam. Pia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) limetoa wanasaikolojia watatu hivyo idadi hiyo kuongezeaka na kuwa 23.
“Utaratibu wote wa zoezi zima utakuwa chini ya Mkoa ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kujitokeza. Tumeshajipanga jinsi ya kuanza kutoa matibabu. Kwanza tutaanza kuwatambua waathirika ambapo tunaangalia kwa wanafunzi (shule husika), shule jirani, walimu wao pia na wazazi. Hivyo zoezi hili linaanza wiki hii kwa timu nzima kukutana.
“Jitihada zilizopo sasa ni kutafuta uwezeshwaji katika kufanikisha matibabu haya ambapo ni kuandaa vipeperushi madodoso, kugharamia watu wanaotoka nje ya mkoa wetu jambo ambalo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Zoezi zima litafanyika kwa awamu mbili, tutafanya sasa na wataendelea kuwa chini ya uangalizi, baada ya miezi miwili tutaendelea na kuhakikisha kila mmoja anakuwa katika hali nzuri ya afya ya akili jambo ambalo linawezekana,” amesema Dk. Wonanji.

Walezi wa wanafunzi waliofariki wazungumza
Peniel Ndemno (66) na Emmy Sitayo (59) ni walezi wa Ruth Ndemno (14) ambao wanamiliki kituo cha kulea watoto yatima kijulikanacho kwa jina la Matonyok Parents Trust kilichopo Kata ya Olasiti, Mtaa wa Kimindorosi.
Sitayo ambaye kitaaluma ni muuguzi ndiye mwanzilishi wa kituo hiki miaka 12 iliyopita ambacho kina watoto 40.
Amesema walimpokea Ruth katika kituo hicho akiwa na umri wa miaka mitatu ambapo alipelekwa kituoni hapo na kiongozi wa Kanisa la KKKT usharika wa Sombetini.
Akiwa kituoni hapo alipata mfadhili wa kumsomesha kutoka nchini Uholanzi, Petra Pontangel, ambaye amekuwa akimfadhili tangu chekechea mpaka darasa la tano, akiwa darasa la tano alipata mfadhili mwingine raia wa Marekani ambaye amekuwa akimlipia ada mpaka mauti yalipomkuta.
“Waliokuwa wanamsomesha kwa kipindi hiki ni familia ya Remer Bringson, ambao ni raia wa Marekani. Kwa mwaka huu walikuwa wamelipa ada ya muhura wa kwanza mwezi ujao wamalizie muhula wa pili. Pia walikuwa na malengo naye kwani walipanga akimaliza kidato cha nne wamchuke akasome huko huko kwao Marekani, lakini ndiyo hivyo tena,” amesema Sitayo.


Amesema kwamba Ruth alikuwa na ndoto za kuwa daktari bingwa na alikuwa na juhudi darasani jambo ambalo lilikuwa likiwapa matumaini ya kutimiza ndoto zake.
Ruth anaelezwa kuwa mkimya na mwenye hekima ambaye muda mwingi aliutumia kujisomea hasa kipindi cha mapumziko.
“Ni kama alijua kilichokuwa mbele yake. Baada ya likizo ya Pasaka kumalizika, akiwa nyumbani alipotaka kuondoka, alimwambia dada yake hapa nyumbani ambaye ni mtoto wetu wa mwisho Naramat kuwa kwa mara ya kwanza hajisikii kwenda shule kwani moyo wake ni mzito. Akamwambia ninakwenda, lakini naomba uniombee,” amesema Sitayo.


Sitayo amesema kifo cha Ruth kimekuwa ni pigo kwa wanafamilia wote, huku akisisitiza watoto wengine wamekuwa wanyonge hivyo wanaendelea kuongea nao kuwajenga kisaikolojia.
Mzazi wa Greyson Rabson (13), Rabson Massawe (40) mkazi wa Morombo ameliambia JAMHURI kwamba mwanaye, Greyson, alikuwa ndiye mtoto wake wa kwanza na kwamba kifo hicho kimekuwa pigo kubwa kwa familia hiyo.
Amesema mtoto wake amesoma katika shule hiyo kwa miaka tisa kuanzia chekechea mpaka darasa la saba na kwamba alikuwa miongoni mwa watoto wanaoongoza darasani.
“Wakati ajali inatokea nilikuwa Manyara, hivyo sikuwa mbali. Niliposikia nilikimbilia eneo la ajali, lakini nikakuta watoto wameondolewa nikaenda mbio mpaka shule ya Tumaini. Nilizuiliwa kuingia, lakini niliwazidi nguvu nikapita mpaka ndani nikaanza kuita jina la mwanangu hakuitika.  Nikakimbia mpaka hospitali ya Karatu nikaenda chumba cha kuhifadhia maiti nako nikazuiwa kuingia, nikaenda kuangalia majeruhi mwanangu sikumuona.


“Baada ya muda kidogo tukaruhusiwa kuingia chumba cha kuhifadhi maiti kuwatambua ndipo nilipomuona mwanangu amelala pale. Niliumia sana, lakini sikuwa na jinsi,” amesema Massawe.
Amesema kabla ya ajali iliyogharimu maisha ya mtoto wake, alikuwa ameshafanya mawasiliano na shule hiyo ili kumpeleka mtoto wake Sara kuanza masomo mwezi Juni mwaka huu, lakini bado anatafakari kama anaweza kuendelea na mpango huo.
“Bado nina mambo mengi ya kutafakari kwa sasa, ni kama maisha yanaanza upya. Ila pia nasubiri kujua hatua za kiserikali baada ya hapa ikiwa ni pamoja na masuala mbalimbali ya usafiri na usafirishaji,” amesema Masawe.

Majeruhi wapelekwa Marekani
Majeruhi watatu wa ajali iliyotokea wiki iliyopita, Jumapili wamesafirishwa kwenda nchini Marekani kwa matibabu zaidi.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu wiki iliyopita alisema amefanikiwa kupata ndege aina ya DC 8 kutoka Shirika la Samaritan Purse linaongozwa na mtoto wa Billy Grahm, aitwaye Franklin Grahm kwa ajili ya kuwasafirisha watoto Doreen, Sadia, na Wilson pamoja na wazazi wao watatu (Mama zao), ikiwa ni pamoja na Muuguzi Simphorosa Silalye, na Daktari Elias Mashalla wa hospitali ya Mt. Meru. Ndege iliyobeba wagonjwa hao inatarajiwa kutua Mjini Charlotte, jijini New York na wagonjwa pamoja na waliowasindikiza wataingia katika ndege nyingine maalumu ya kubeba wagonjwa (Air Ambulance) hadi mji wa Sioux, Iowa ambako watapokelewa na Uongozi wa Hospitali na Mercy na Shirika la STEMM.

Majina ya watoto waliofariki
Mteage Amos, Justine Alex, Irine Kishari, Gladness Godluck, Praise Roland, Shedrack Biketh, Junior Mwashuya, Aisha Saidi,  Oumhqh Heri Rashid, Gema Gerald, Rebecca Daudi, Hagai Lucas, Sada Ally, Ruth Ndemna, Musa Kassim, Neema Eliwahi, Neema Martin, Greyson Robson Massawe, Witness Mosses, Hevenight Enock, Iar Tarimo, Anorld Alex, Naomi Hosea, Rukia Altani, Paulo Thomas, Eliapendo Eliudi, Marion Mrema, Rehema Msuya, Sabrina Said, Prisa Charles

By Jamhuri