Mtunga Zaburi, Mfalme Daudi aonya hivi: “…Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, jeuri huwavika kama nguo, macho yao hutokeza kwa kunenepa, wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. Hudhihaki, husimulia mabaya.  Husimulia udhalimu, kana kwamba wako juu.” Zaburi 73:6-8; Mhubiri 8:11, Biblia Takatifu.

Wadau ‘wanajamii’ wenzangu; ‘maono’ yaliyonitokea kwa miezi kadhaa yanazidi kunikereketa; niendelee ‘Kusema yaliyo ya kweli na Amani na Upendo; kwa uweza wa Roho Mtakatifu’.

Kiburi na udhalimu pia dharau ni kosa na dhambi kwa Mwenyezi Mungu na wanajamii wenzako; wapo baadhi ya wanajamii wanaofanikiwa kupata nafasi za uongozi au utajiri na kulewa mafanikio hayo kupita kiasi; hata wakijiona wana makosa.

Bilionea Bill Gates wa Marekani, mwanzilishi wa Microsoft, alisema: “…Ni vizuri kufurahia mafanikio, lakini ni muhimu kuyachukua makosa kama funzo.”

Naye, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili; Ali Hassan Mwinyi, alisema: “…Kushinda ni moja ya mafanikio katika maisha iwapo utaamua kufanyia kazi makosa yako.”  Mwisho wa kunukuu.

Yote hayo ni kielelezo dhahiri kwamba kiongozi au mwanajamii ukoseapo jambo lolote, au kama hauna uhakika nalo; usifanye ajizi, likubali kosa lako na kufanya masahihisho stahiki badala ya kulitolea kejeli; dharau au kulifanyia kiburi.  Kosa ni funzo. Hakuna mtu mkamilifu kwa asilimia mia moja.

Tuchunge ‘vinywa’ vyetu au ndimi zetu kwa kutoa uamuzi wenye busara, hekima, upole na kuwaridhisha ipasavyo tunaowaongoza na kututegemea.

Hata kama unampenda kiasi gani kiongozi yeyote yule, kwa madhambi anayofanya au udhalimu wa dhahiri; unatakiwa kumuonya papo kwa papo; ukimya kwake ni unafiki wa dhahiri na kujizolea dhambi pia kwa Mungu – YEHOVA.  Kuonya ama kukosoa si kosa.

Wapo baadhi ya wanajamii na viongozi hapa Afrika yetu ambao huona maovu ya mtu mwingine hayawahusu; na wakiegemea kwenye tamko la “Kila mtu ataubeba msalaba wake”; na wapo baadhi ya viongozi ambao huwapongeza na kuwatia ‘moyo’ – viongozi wenzao wanaotenda makosa; ati “…kwa kuwa wamewateua na kusimamia matakwa na utashi wao wa kiuongozi.”  Ni dhambi.

Biblia Takatifu yaonya hivi: “…Nimwambiapo mtu mbaya, hakika utakufa; we usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumuonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mikononi mwako.

Lakini ukimwonya mtu mbaya (hasa kiongozi), wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.

Tena mtu mwenye HAKI yake, na kutenda uovu, nami nitaweka KIKWAZO mbele yake…” Ezekiel 3:18-20.

Hivyo basi, twastahili kuchunga ‘ndimi’ zetu hasa viongozi wetu wa Afrika ya sasa; kwani matamko yao huchukuliwa kama ni ‘amri’ na hata kama yanakiuka katiba, sheria na haki za wanajamii.  Ni dhambi na dhuluma.

‘Ndimi’ zetu, ni chombo au kiungo cha mwili kinachoweza kujenga au kuibomoa jamii mara moja na kusababisha mfarakano usio na tija.  Ni dhambi.

Neno la Mungu laonya: “…Aonywaye mara nyingi akishupaa shingo; atavunjika ghafla, wala hapati dawa.  Wenye HAKI wakiwa na amri watu hufurahi; bali muovu atawalapo, watu huugua.”  Mithali 29:1-2 (Biblia).

Mirathi ya siasa

Tumezoea kusikia juu ya ‘mirathi’ iwahusuyo wana -ndugu wa mwanajamii mwenzetu anapoaga dunia.  Lakini leo, ‘…maono’ yamenijia niusemee ukweli kuhusu mirathi ya kisiasa.  Si jambo la ajabu.

Hivi karibuni tumemsikia Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally akisema baadhi ya viongozi vijana wanahitaji ‘kufundwa’. Upo ukweli, pia sintofahamu juu ya kauli yake.

Wapo pia baadhi ya viongozi wakubwa kitaifa ambao nao kwa nyakati tofauti wamezama kwenye wimbi la ‘mapoyoyo’; tena kwa utashi binafsi wa kutisha na kushangaza.

Neno ‘mapoyoyo’ si tusi wala kashfa, bali linashabihiana na neno-kuu ‘…yoyoma’; yaani ‘enda ovyo, enda bila mpango; enda popote lakini pasipo kuaga, totoma, tokomea; ea, eka, esha’.  Kamusi ya Kiswahili Sanifu ukurasa 320.

Hivyo basi, mwanajamii au kiongozi yeyote Afrika yetu afanyae mambo au uamuzi ulio ndivyo-sivyo; yenye utata na migongano isiyoleta tija stahiki; huyo dhahiri ni kati ya viongozi mapoyoyo. Tunao wengi na wanajidhihirisha wenyewe kwa kukurupukia kauli zao tata na nyingine zikiwa hazina staha.

Tatizo hilo linazushwa na tabia za uongozi uliogubikwa na woga, kutojiamini, chuki, malipizi na hata kujipendekeza kwa baadhi ya wakubwa zao na wanajamii wanaowazunguka. Ni dhambi.

Mirathi ya siasa zetu Afrika haiko katika tabia hizo kwani waasisi wa siasa za Bara letu la Afrika; na hasa Tanzania; hawakuwa na mwenendo huo wa ‘kipoyoyo’.  Rejea waasisi wa Umoja wa Afrika (OAU); wengi wao walikuwa viongozi makini na waadilifu.

Waasisi wa siasa za Afrika yetu…ilee, waliepuka kabisa kuwachanganya wanajamii waliowaongoza kwenye migogoro na migonganisho, na walichunga vema ‘ndimi – vinywa’ vyao; kwa kujenga ushirikiano pevu wakati wote.

Waasisi hao walifanya majadiliano na baadhi ya viongozi na wanajamii kwa njia za kistaarabu zaidi, hata kukosoana bila ya kupayukapayuka kupitia vyombo vya habari. Ustaarabu wa Kiafrika na kiuongozi mustarehe. Hawakushabikia lugha za vijembe vya mitaani.

Waasisi wa siasa za Afrika yetu walisimamia ‘Utu, Ukweli, Amani na Upendo’ kwa wanajamii wote wakikazia juu ya maendeleo stahiki.

Hayati Malcolm X, mwanaharakati wa haki za weusi Marekani; alisema: “Nitafuata ukweli bila ya kujali nani anausema.  Nitafuata haki bila ya kujali inampendelea nani au ipo dhidi ya nani.”

Yamkini, baadhi ya waitwao wanasiasa wetu Afrika ya sasa; mirathi hiyo makini ya siasa haimo katika harakati zao za kiuongozi; ijapokuwa hudiriki kuimba kuwa wanawaenzi waasisi wa siasa za Afrika yetu ileeee.

Naamini, kwa ‘maono’ yaliyonijia mara kadhaa; yanielekeza kwamba viongozi wetu wa siasa Afrika; ni wana wa watangulizi wa hao viongozi waliokuwa makini, wenye weledi kwa waliyoyatenda kwa faida ya wananchi wao.

Mithali 17:25-27 Biblia Takatifu yaonya hivi: “…Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye; Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa; Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si-kwema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao.  Azuiaye – maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara.”

Msisitizo uko pia kwenye Mithali 24:1-2 ukituonya “…Usiwahusudu watu waovu, Wala usitamani kuwa pamoja nao; Kwa maana moyo wao hufikiri dhuluma.  Na midomo (ndimi-vinywa vyao) yao huongea madhara.”

NENO la Mungu lasema: “…Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa (ndimi) cha kujipendekeza hutenda uharibifu.”  Mithali 26:28.

 Baadhi ya viongozi wetu Afrika yetu, na hasa mabunge ya sasa badilikeni, vinginevyo hamkidhi mirathi ya siasa za kweli za waasisi wa Afrika yetu ilee.

Baadhi ya viongozi wa mabunge ya Afrika yetu ya sasa wanatumika kiuovu dhidi ya wanajamii wenzao.  Ni dhambi.

Usomapo kitabu cha Kura’an Tukufu, Suratut Tawba, sura ya 9, aya 107 yaonya hivi: “Na bila shaka wataapa (waseme) ‘Hatukukusudia ila wema’.  Lakini Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao ni waongo.”

Naye, hayati Reginald Mengi, amewaasa viongozi wetu miezi kadhaa iliyopita akisema: “Chungeni ndimi zenu” kwa faida ya taifa letu.

Rai yangu “Mungu usikie sauti yangu katika malalamiko yangu; Unilinde uhai wangu na hofu ya adui.” Zaburi 64:1.  Chungeni ndimi zenu.  Amina.

Mungu Ibariki Afrika yetu na viongozi wake.

Simu: 0655305588

281 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!