Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Sukari Tanzania (NSI) kilichopo Morogoro, umelalamikiwa kwa kukiendesha chuo kama taasisi binafsi.

JAMHURI imepata taarifa kuwa chuo hicho hadi sasa kimeendeshwa kwa kipindi cha miaka tisa bila kuwa na Baraza la Uongozi.

NSI inaongozwa na Kaimu Mkuu wa Chuo, Julius Raphael Deteba, na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Salumu Mwanalelo, ambao wamekuwa ndiyo wenye mamlaka ya uongozi na utendaji wa chuo hicho tangu mwaka 2007 mpaka sasa.

“Wanakiongoza chuo namna wanavyotaka bila hata ya kufuata taratibu za kisheria, huku wakiendelea kulea uozo ndani ya taasisi hii ya Serikali,” anasema mtoa taarifa.

Imeelezwa kwamba Serikali imekitelekeza chuo hicho na mali zake ambazo mapato yake hayajulikani yanakopelekwa.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Juni 30, 2015 imebainisha uwepo wa ubadhirifu katika mikataba ya upangishaji wa nyumba zinazomilikiwa na chuo ambayo mpaka sasa haijatolewa ufafanuzi.

Ripoti hiyo inasema chuo kinamiliki nyumba 138, ambapo kati ya hizo nyumba 39 zinatumiwa na wafanyakazi wa chuo na nyingine 99 zilizobaki zimepangishwa kwa watu binafsi kwa mikataba isiyojulikana.

Ripoti ilibainisha kutokuwapo kwa uongozi mzuri wa chuo hadi chuo kinakosa dira na mwelekeo wa kitaaluma, zaidi ya kukiendeshwa kimazoea kama taasisi binafsi.

Yapo malalamiko juu ya matumizi ya karakana ya chuo ambayo hutumika kuchonga vipuri vya magari na mashine mbalimbali.

“Karakana hutumika kutengeneza vipuri kutoka viwanda vingine vya sukari pamoja na vipuri mbalimbali vya magari ya kampuni na watu binafsi, lakini hatujui fedha zinazopatikana zinaenda wapi,” anasema mtoa taarifa mwingine.

Pamoja na karakana kufanya kazi siku zote na kuingiza fedha, malipo yanayotolewa hayafuati mfumo wa Serikali.

Katibu Mtendaji wa TSPA, Deo Lyatto, ameiambia JAMHURI kuwa kisheria chuo hicho bado kipo chini ya Serikali japo zipo juhudi zinazofanyika kukiondoa.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Sukari cha Taifa, Julius Raphael Deteba, alipoulizwa na JAMHURI juu ya malalamiko hayo ya wafanyakazi, amesema malalamko hayo ni majungu yanayoenezwa na wabaya wake ndani ya chuo hicho.

“Nimekuwa kiongozi ndani ya chuo hiki kwa miaka mingi na sijawahi kupatwa na kashfa yoyote ndani ya utumishi wangu, kama kuna watu wamekuletea majungu kama hayo kwangu hawana hoja,” anasema Deteba.

Anasema ndani ya utumishi wake katika taasisi hiyo, anajielewa kuwa yeye ni msafi kuanzia duniani hadi mbinguni na hata viongozi wake wanalijua hilo.

Deteba anasema majungu hayo hayawezi kumnyima ujasiri wa kuendelea kufanya kazi na kuhakikisha anaisaidia Serikali ya Awamu ya Tano kutimiza ahadi zake kwa wananchi.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Salum Zuberi Mwanilelo, anasema suala hilo hawezi kulizungumzia kutokana na unyeti wake, hivyo linahitaji maandalizi ya kutosha. “Hapa nilipo kuna kelele nyingi, sidhani kama tunaweza kuelewana,” anasema Mwaninelo.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Yongolo Mweshemi, amekiri uwepo wa matatizo ndani ya chuo hicho na kusema kuwa Serikali ipo katika mipango madhubuti ya kukabiliana na matatizo hayo.

Alipoulizwa kuhusiana na ripoti ya CAG iliyobaini upungufu ndani ya chuo hicho, amesema yeye kama mkurugenzi hana taarifa ya ripoti hiyo.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, amesema Wizara inayo taarifa juu matatizo yanayoendelea ndani ya chuo hicho na Serikali inayafanyia kazi.

“Kwa mfano, suala la chuo kuongozwa bila ya kuwa na Bodi si la kuweza kufanyiwa kazi kwa ghafla… linahitaji muda wa kuliangalia kwa jicho pevu,” anasema Dk. Tizeba.

Anathibitisha uwepo wa ripoti ya CAG ya Juni 30, 2015 iliyobaini uwepo wa matatizo ndani ya chuo ambayo wizara inayafanyia kazi.

Chuo cha Sukari cha Taifa (NSI) kilianzishwa mwaka 1975 na kuanza rasmi kutoa mafunzo kwa wafanyakazi katika mashamba ya miwa na mafundi kuendesha na kutengeneza mitambo, mwaka 1981 baada ya kufunguliwa rasmi Agosti 8, 1981 na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

By Jamhuri