Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), imelalamikiwa kwa vitendo vya rushwa kwa kufanya uamuzi unaoonesha kuwapendelea matajiri wanaolalamikiwa na wafanyakazi wao kwa kutowalipa haki zao na kuwafukuza kazi bila utaratibu.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wananchi wapatao saba waliofungua mashauri yao CMA wakilalamikia kufukuzwa kazi bila kulipwa haki zao, wanasema kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa madai yao wamekuwa wakielezwa na walalamikiwa hao kwamba hawawezi kushinda ndani ya tume hiyo.
‘‘Madai yetu yako wazi kabisa lakini uamuzi unaotolewa unatia shaka kwani hata kabla ya kusikilizwa kwa malalamiko yetu tunaelezwa na waajiri wetu kwamba hatuwezi kupata haki zetu, na hawa wanaonesha wazi kuna vitendo vya rushwa ambavyo vimekithiri ndani ya tume hii.”
“Tunaamini kwamba tume hii haiko kwa ajili ya kuwapatia haki zao wanyonge bali iko kwa ajili ya kuwatumikia matajiri tu, hivyo Serikali iifute na kuunda chombo kipya ambacho hakitaegemea upande mmoja na kutoa haki kwa watumishi wanaofungua malalamiko yao bila upendeleo,’’ amesema Yusufu Salum ambaye amefungua mgogoro katika tume hiyo dhidi ya mwajiri wake Lake Oil Limited.
Salum alikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Lake Oil Limited iliyoko eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa kipindi cha miaka mitatu akiwa na kazi mbili tofauti ikiwemo utunzaji wa bustani kuanzia Machi 1, 2013.
Amesema kutokana na kazi hiyo ya utunzaji wa bustani ambayo inahusisha kusafisa eneo, kung’oa visiki, kupanda miti ya michungwa na mipera alikuwa akilipwa mshahara wa Sh 2,500,000 kwa mwezi.
Amesema pamoja na kazi hiyo, mwajiri wake amekuwa akimlipa fedha pungufu tofauti na makubaliano ya kiasi hicho cha mshahara na kusababisha afanye kazi kwa usumbufu mkubwa na kwamba alipodai haki yake ndipo alipojikuta akifukuzwa kazi.
Amesema Septemba 16, 2013 alitanguliziwa malipo ya Sh 500,000, Septemba 30, 2013 akalipwa Sh milioni 1, kati ya Oktoba 17 na 21 mwaka 2013 alilipwa Sh milioni 4, Novemba 1 na 12 alilipwa Sh milioni 2 na kwamba kiasi cha fedha anachodai kwa mwajiri wake huyo kutokana na kazi ya utunzaji wa bustani ni Sh milioni 12 ambazo ni malimbikizo ya mshahara.
Amesema madai yake mengine ni likizo, fidia ya mishahara ya miezi 12, kiinua mgongo, NSSF, mkono wa kwaheri, mishahara yake hadi anaachishwa kazi na hati safi ya utumishi.
‘‘Nilifungua shauri la mgogoro na mwajiri wangu katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Kanda ya Dar es Salaam, lililopewa namba CMA/DSM/ILA/R.883/16 na mwajiri wangu akanieleza kwamba siwezi kupata ushindi wowote ndani ya tume hii.
Kutokana na uamuzi wa CMA ambao umejaa mashaka nimepewa nakala mbili tofauti za hukumu ya kwanza kulikuwa na madai kwamba nilikuwa katika mkutano wa kiroho jambo ambalo halina ukweli wowote na nilipohoji kuhusu hoja hiyo ikaandikwa nakala nyingine ya hukumu yenye marekebisho,’’ amesema.
Katika nakala hiyo ya hukumu iliyotolewa Januari 9, mwaka huu iliyotolewa na Msuhishi, Alfred Amos kuna maneno yanaeleza, ‘‘Nianze na kipindi ambacho mlalamikaji alikuwa katika mkutano wa kiroho (worship seminar) Juni 2015 hadi Julai mwaka jana, saa 8 mchana hadi saa 9 alasiri.
Muda wa tume (business hours) CMA ni kuanzia saa 1:30 hadi saa 9:30 alasiri ambapo mlalamikaji angeweza kutumia asubuhi hadi saa 7 mchana kufungua mgogoro.
Lakini kwa kuhofia kwamba endapo shauri lingefunguliwa, lingefutwa, ‘‘For Want of Prosecution’’ hivyo tume inakubaliana na ruhusa ya mlalamikaji kipindi cha semina hadi kwisha. Pili tume imetazama tangu ameachishwa kazi hadi kabla ya semina, yaani Aprili hadi Mei Mwaka juzi (siku 32), ambapo mlalamikaji alieleza kuwa alikuwa na makubaliano na mkurugenzi kusubiri makusanyo ya fedha ili apate kumlipa kwa kuwa alipoachishwa kampuni ilikuwa haina fedha.’’
Amesema madai ya kuwa alikuwa kwenye semina ya kiroho kama yalivyotolewa na tume hiyo katika uamuzi wake mdogo yametungwa kwa sababu wanazozifahamu wao kwani yeye imani yake sio Mkristo na wala hakuwa kwenye semina.
Pamoja na uamuzi huo mdogo kujaa kasoro ambazo zinaonesha wazi kwamba zilitungwa ili kumnyima haki zake kama alivyoelezwa awali na mwajiri wake, alipolalamika kwa Mkurugenzi Msaidizi wa CMA, Emilyo Mwidunda na kuamuriwa kufanyiwa marekebisho, Januari 20, mwaka huu akapewa nakala nyingine ya uamuzi mdogo ambayo iliondolewa kipengele hicho kinacholalamikiwa.
Mwidunda alipohojiwa na JAMHURI, kuhusu kukithiri kwa vitendo vya rushwa na uamuzi unaopendelea upande mmoja ndani ya tume hiyo amesema mwenye mamlaka ya kuzungumza ni Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Nungu.
Nungu amelieleza JAMHURI kwamba angekutana na walalamikaji hao ili asikilize madai yao ndipo achukue hatua dhidi ya wahusika. Hata hivyo baada ya walalamikaji kufahamishwa na gazeti hili kuhusu kauli hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo walionana nae kwa ajili ya ufumbuzi wa madai yao.
Mkuu wa Ulinzi wa kampuni ya Lake Oil, Adolf Kachira amesema kutokana na madai ya Salum kuchukua muda mrefu alifikiri madai yake alilipwa na kwamba Wizara ya Kazi ndio inawaangusha, na malalamiko yao dhidi ya manyanyaso wanayokutana nayo hayashughulikiwi.
Meneja Mwajiri wa Kampuni ya Lake Oil Limited, Fahim Saad amesema walikuwa na mkataba na Salum na kazi walizokuwa wanakubaliana na ikikamilika walikuwa wanatoa kazi nyingine.
‘‘Tumempa fedha nyingi sana huyu jamaa kwa ajili ya malipo ya kazi ambazo alikuwa anazifanya ikiwemo kutunza bustani. Yeye ni mtunzaji wa bustani tu na tulimalizana nae muda mrefu,’’ amesema Saad.
Alipohojiwa kuhusu kiasi cha fedha alizolipwa kwa kazi hiyo ikiwemo mishahara yake na haki zake zote anazostahili akidai kuwa ni nyingi, hakutaka kuelezea hilo.
Hata hivyo Salum amesema hakuna fedha alizolipwa baada ya mkataba wake kuvunjwa na ndio sababu ya yeye kwenda Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kufungua mgogoro na mwajiri wake.

By Jamhuri