Wiki iliyopita makala hii iliishia pale ilipokuwa inasema baadhi ya waandishi wameamua kuisifia serikali tu. Hapana, hii si Tanzania tunayotakiwa kuijenga. Nchi ya waoga wa kuthubutu, nchi ya wanafiki, nchi ya kujipendekeza kwa watawala.

Mungu alipompa malaika Lucifer cheo cha uwaziri mkuu mbinguni, Lucifer alijisahau. Alidhani kwamba Mungu hatamtoa tena kutoka kwenye nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba; kuna wakati shetani alikuwa malaika mbinguni, kabla hajaondolewa mbinguni alikuwa malaika mkuu. Kwa kifupi ni kwamba yeye ndiye aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya Mungu.

 Akalewa madaraka ya uwaziri mkuu, akajiona anaweza kuiongoza dunia na mbingu. Akatamani kuabudiwa kama Mungu Mwenyezi anavyoabudiwa, akajiona anaweza kuumba.

Akajawa kiburi na majivuno, Mwenyezi Mungu akachukizwa na nyendo za shetani, akamuondoa kutoka kwenye ufalme wake wa milele. Kisa cha shetani kuondolewa mbinguni ni ‘majivuno’.

Nabii Isaya anatufunulia siri hiyo, “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa ewe uliyewaangusha mataifa, nawe ulisema moyoni, ‘Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu: Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye aliye juu’.” [Isaya 14:12-14]. Tuogope kulewa madaraka tuwapo madarakani.

Siasa si uadui, ni hoja. Siasa ni sehemu ya maisha ya binadamu. Mwanafalsafa Hegel anasema: “Binadamu ni mnyama wa kisiasa.” Hizi siasa za kushambuliana kwa mapanga ni siasa zinazopandikiza chuki ya kudumu kwa kizazi hiki na kinachokuja.

Ni hatari kwa taifa kuwasikiliza watu fulani na kuwapuuza wengine. Ni hatari kwa taifa kuyaamini mawazo fulani na kuyapuuza mengine, ni hatari kwa taifa kuwachukia wasema ‘ukweli’.

Ni hatari katika taifa kuwa na watu wanaojulikana na wasiojulikana, kuna matukio ya Watanzania wenzetu kutekwa, kuteswa na wengine wanauawa, nyumba tunayoijenga ni moja, tunyang’anyane fito?

Nihitimishe makala yangu kwa kuwaomba wasomi wa Kitanzania wazitoe akili zao likizo na kuzileta kwenye taifa lao. Taifa letu linahitaji mgongano wa kifikra.

Mgongano huo wa kifikra utaliingiza taifa katika mijadala itakayoleta mawazo mbadala. Binafsi huwa ninatofautiana sana na mitazamo ya baadhi ya viongozi wetu. Mfano, unakuta kiongozi ameishia darasa la saba, au kidato cha nne au kidato cha sita.

Huyu kiongozi yeye atapendelea sana umwite ‘Mheshimiwa.’ Ukimwita jina tofauti na hilo, ni kosa la kinidhamu. Yaani ni taabu kweli kweli, lakini ukiingia ndani ya kichwa cha kiongozi huyu utakuta ana mawazo mabaya.

Kiongozi mwenye mawazo kama hayo atatoa wapi mawazo jengefu ya kifikra? Niwaombe sasa wanazuoni na wasomi mbalimbali tuanzishe mijadala ya mawazo jengefu katika midahalo ya kitaifa, kwenye vyombo mbalimbali vya habari kama magazeti, redio na televisheni.

Lengo kuu ni kuijenga Tanzania yenye ushindani wa kifikra. Tusiwaachie wenye mawazo dhaifu kuichafua Tanzania yetu kwa mawazo yao dhaifu. Asante sana kwa kutumia muda wako kuyasoma maoni haya. Mungu akubariki sana.

337 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!