DIWANI WA CHADEMA AUWAWA KWA MAPANGA NA WATU WASIOJULIKANA MOROGORO

Diwani wa CHADEMA, Godfrey Lwena ameuawa usiku wa Alhamisi nyumbani kwake.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha kuuawa kwa diwani huyo wa Kata ya Namwawala, Jimbo la Mlimba.

Hata hivyo kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Matei amesema kwa sasa hawezi kufahamu mauaji hayo yanatokana na nini.

Akizungumza kwa simu Kamanda Matei pia amesema kwa sasa ni mapema mno kuwajua watu waliohusika na mauaji hayo na hivyo amewataka wananchi kuwa wavumivu wakati polisi wakiendelea na uchunguzi wa mauaji hayo.

“Mauaji yametokea usiku huu na polisi wameshafika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu, sasa hivi tuko kwenye uchunguzi na tunaomba wananchi watusaidie kutoa taarifa za watu wanaodhani kuwa wanahusika kwenye tukio hili na tutahakikisha tunawapata,” amesema Kamanda Matei.

Awali mbunge wa Jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali alithibitisha mauaji hayo na kudai kuwa yatakuwa yamepangwa.

Amesema kuwa mauaji hayo yametokea saa moja na nusu usiku wakati diwani huyo akiwa  nyumbani kwake.

“Akiwa nyumbani kwake ghafla umeme ulikatika, Lwena alitoka nje na kuzunguka nyuma ya nyumba yake kuangalia kama kulikuwa na hitilafu na ndio ghafla lilitokea kundi la watu na kuanza kumshambulia kwa mapanga, ” amesema Lijualikali.

Lijualikali amesema kuwa pamoja na watu hao kumshambulia diwani huyo kwa mapanga hadi kufariki lakini pia familia ya diwani huyo imepigwa mawe wakati wakijaribu kupambana na kundi hilo la watu.