Mwishoni mwa 2010 na mwanzoni mwa 2011, dunia ilishuhudi mfululizo wa maandamano na kuanguka kwa tawala kongwe katika ulimwengu wa Kiarabu. Maandamano hayo yanaitwa “Arabian Spring.”

 Yalianza kwa Mapinduzi ya Tunisia ambayo yalifanyika kwa hisia binafsi ya Mohamad Bouazizi Desemba 18, 2010 katika maandamano ya rushwa kwa polisi na matibabu kwa wagonjwa.

Kwa hakika “Arabian Spring imetikisa watawala waliokuwa wamejisahau katika ulimwengu wa Kiarabu katika nchi za Tusinia, Misri, Libya, Yemen, Bahrain pamoja na Syria bado kunafukuta.

Sababu kadhaa zinatajwa kuchangia hali hiyo, kama vile uongozi wa kibabe, rushwa, ukosefu wa ajira, watu kutokuwa na haki na uhuru wa kujiamulia wanavyotaka watawaliwe katika nchi hizo.

Tunaona katika Ulimwengu wa Kiarabu vijana katika nchi hizo wakilalamikia umaskini, na kupanda kwa bei za vyakula, mfumuko wa bei, lakini pia ukiukaji wa haki, na uhaba mkubwa wa ajira kama nilivyosema awali ni sehemu tu ya sababu za “Arabian Spring”. 

Mwandishi Hisham Sharabi katika kitabu chake cha mfumo dume anaeleza kwamba; “Wakati mataifa mengi katika dunia yakiwa na kiwango cha juu sana cha haki za demokrasia na siasa, ulimwengu wa Kiarabu bado unakabiliwa na mifumo mbaya ya kisiasa ya msingi ya rushwa, hali ya sheria ya dharura, ukosefu wa uchaguzi huru na uhuru wa kujieleza na imani kali za kidini.” 

Heka heka za uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki zimeanza, tofauti na miaka ya nyuma. Uchaguzi wa mwaka huu utakabiliwa na upinzani mkali kutoka katika kundi la Chama cha Mapinduzi. 

Makundi ya vijana tayari yamejipanga kukabili kundi la wazee katika uchaguzi huo na tayari vijana kadhaa wameshachukua fomu katika Afisi Kuu ya Makao Makuu ya CCM Zanzibar, wakisubiri hatua nyingine kabla ya siku ya kuchaguliwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mkakati maalum umeandaliwa ambao unaratibiwa na kundi kubwa la vijana walioko Umoja wa Vijana wa CCM, vijana wa CCM waliomo ndani ya Bunge pamoja na wanasiasa wengine vijana wa Zanzibar wakishirikiana na wenzao wa Tanzania Bara.

 Chini ya mkakati huo, kundi hilo la vijana limefanikiwa hadi sasa kuwaunganisha karibu vijana wote waliomo katika Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na kilichosalia sasa ni kampeni ambayo kauli mbiu yake ni “Vijana Kwanza, Wazee Watupishe.” 

Kwa hali ya mambo yanavyokwenda, wimbi la vijana linaweza kuwaweka kando wanasiasa wazee ambao hawataweza kuhimili mahitaji ya siasa za zama hizi hasa ikizingatiwa kuwa ndani ya Bunge la Tanzania kwa sasa kuna vijana wengi ambao kama wataamua kuwaunga mkono vijana wenzao, nafasi ya wanasiasa wakongwe inaweza kuwekwa katika kaburi la sahau. 

Suala la kuwapa nafasi vijana za uongozi katika ulingo wa kisiasa ni jambo lisiloweza kuepukwa kwa sasa na zaidi tukitazama mahitaji mapya ya jamii na hata ya uendeshaji wa mabunge na vyama vya siasa kwa ujumla. 

Jamii ya leo ni jamii huru kabisa iliyojikomboa katika nyanja zote za maisha. Leo vijana wanautazama ulimwengu kwenye kiganja cha mkono. Hapo wanapata kila aina ya taarifa, wataona vijana wenzao katika mataifa mengine wakisakata kabumbu kwenye timu  za Ulaya wakilipwa mamilioni ya fedha, wengine wakiwa katika nafasi za uongozi wa kisiasa. 

Nchi zao ziliwaandaa vijana katika soko la ajira. Vijana wameonesha ujuzi, maarifa na uwezo wa uongozi katika nchi hizo na zimepata maendeleo ya haraka kwa sababu ya nguvu ya ujana katika kuchapa kazi. 

Kama ilivyoshindwa nadharia ya Ujamaa katika nchi nyingi, mwenendo wa kuwapuuza vijana hautaendelea kuwa na nafasi tena katika uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki kwani inavyoonekana wanasiasa wazee hawataweza tena kuhimili vishindo vya mabadiliko ya kisiasa katika dunia ya sasa.

 Kama tunavyofahamu kuwa mabadiliko yaliyotokea katika ulimwengu wa Kiarabu katikati ya mwaka 2011 kwa wanasiasa wakongwe kupoteza nafasi zao za uongozi na hata umaarufu katika uwanja wa kisiasa.

 Hali hiyo inaweza kuleta changamoto mpya kwa vijana hapa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama walivyojitokeza katika kuchukua fomu za kuwania kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

 Ingawa mabadiliko ya kisiasa hapa kwetu hayatakuwa kama yale yaliyotokea katika Ulimwengu wa Kiarabu, lakini nguvu ya ujana itatumika kuwasukuma vijana kuingia katika Bunge la Afrika Mashariki.

 Haiba ya ujana inaweza kuwa turufu tosha ya kuwaacha nyuma wagombea wazee waliojitokeza kuwania nafasi hiyo. Ikiwa kuna mtu bado ana mashaka na msimamo wa vijana wa Zanzibar kuhusu nafasi za uongozi katika Bunge la Afrika Mashariki, basi jibu lake litapatikana kupitia kura katika Bunge hapo baadaye watakapochagua wabunge wa Afrika Mashariki.

 Ukipima mambo kwa sasa katika kisiasa ni wazi kuwa vijana tayari wamejitambua umuhimu wao, wamefahamu nguvu na uwezo wao katika kuleta mabadiliko si tu ya kisiasa, bali ya kiuchumi na kijamii.

 Ni vijana wachache katika zama za sasa ambao hawajitambui, wala hawajielewi  na kwa maana hiyo aina hii ya vijana ni rahisi kutumiwa na wanasiasa wenye kujali maslahi yao zaidi kwa kuwa vijana hao hawafahamu maisha yao yanakwendaje.

 Wapo vijana wengi hivi leo wameamka katika usingizi mzito, wameshawaelewa wanasiasa wababaishaji, wazugaji na wanauelewa wa kutosha juu ya masuala ya siasa, uchumi, uongozi na masuala mengine ya kijamii.

 Mwishoni mwa miaka ya 1990 tulishuhudua Ujamaa ukianguka kwa kasi kubwa na ile kambi ya Mashariki ikilazimika kubadili mwelekeo wa chombo chake, lakini licha ya salaam za wakati kuanza kutumwa miongoni mwa wanasiasa wakongwe, bado kuna wengine wanasubiri iwakute aibu ya kushindwa katika ulingo wa kisiasa.

 Pamoja na mabadiliko hayo, wapo wanasiasa wazee au wakongwe wasiokubali mabadiliko ya jambo katika jamii, hawa watashindwa wenyewe katika uchaguzi wa mwaka huu kwa wapigakura vijana waliomo ndani ya Bunge la Tanzania kuwanyima kura zao.

 Vijana wengi wanaonekana kuanza kuzitupia kisogo siasa zisizowahakikishia maisha bora. Si vyama vya upinzani au vyama tawala; vyote vitakuwa katika wakati mgumu kipindi hiki.

 Lazima tukubali kwamba matumaini ya vijana yanajengwa kwa uhalisia wa mambo na kwamba masuala ya kuboresha  huduma za jamii kama elimu, makazi bora, afya, maji safi na salama, demokrasia na utawala bora ni mambo ambayo vijana wanayatizama kwa jicho pana.

 Vijana nao katika kufikia kutimiza  haja za kisiasa wanahitaji kufikiria zaidi namna watakavyoweza kutoa ushindani stahiki kwa wanasiasa wazee kwani si kila kijana anaweza kuwa kiongozi mzuri, la hasha.

 Kamwe vijana wenye sifa za mashaka na ubabaishaji hawataweza kuushinda ‘mfumo wa uanasiasa wa uzee’ bali ni vijana makini, weledi, wenye adabu na staha na wenye kujituma ndio watakaoweza kuleta changamoto ya kweli katika siasa.

 Jambo hili si la kufikirika, ni suala lililo wazi kwamba vijana hawatakubali tena kutumika katika kuwabeba wanasiasa wazee bali watatumika kama nguvu kubwa ya mageuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi katika kuwafikisha mbele vijana wenzao kufanikiwa.

1273 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!