ELIMU YA KULIPA KODI YAENDELEA KUTOLEWA KWA WATANZANIA

 Afisa Muelimishaji Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rose Mahendeka akiwaelimisha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017/18 katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
 Msaidizi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Chama Siriwa akiwasilisha mada mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi ya Majengo, katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Valentine Baltazar akiwasilisha mada mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Taratibu za Kiforodha, katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari,
 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepongezwa kwa kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa ofisi za Serikali na Asasi za Kiraia kwa ajili ya kuongeza ufahamu na kuwa mabalozi wa masuala yanayohusu kodi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya kodi kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) yaliyofanyika leo ofisini hapo,  Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Bw. Edwin Rutageruka amesema TRA inastahili kupongezwa kwa kazi inayoifanya ambayo imepelekea kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
“Ni dhahiri kwamba, sasa hivi  TRA inafanya kazi kubwa ya ukusanyaji wa mapato na kutoa elimu ya kodi kwa vikundi na taasisi mbalimbali, hivyo, fursa hii tuliyoipata tuitumie vizuri ili kuongeza uelewa wa kutosha kuhusu kodi ili tuwe  mabalozi wazuri kwa wengine”, amesema Rutageruka.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania  Bi. Rose Mahendeka, akiwasilisha mada ya Kodi na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 amesema,  kila mwananchi anajukumu la kudai risiti kila anaponunua bidhaa na kila mfanyabiashara anatakiwa kutoa risti kila anapofanya mauzo.
“Suala la kulipa kodi lipo kwa mujibu wa sheria hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kudai risiti wakati wote anaponunua bidhaa na vivyo hivyo kwa upande wa wafanyabiashara wanapaswa kutoa risiti kila wanapofanya mauzo”, amesisitiza Mahendeka.
Muelimishaji mwingine kutoka TRA aliyewasilisha mada kuhusu Kodi ya Majengo Bw. Chama Siriwa amewahimiza wafanyakazi hao wa TANTRADE kuwahi kulipa kodi ya majengo ya mwaka huu wa fedha 2017/18 ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na msongamano wa watu ambao mara nyingi hujitokeza kulipa mwishoni.
“Watu wengi wana tabia ya kusubiri tarehe za mwisho kulipia kodi ya majengo suala ambalo linasababisha msongamano usio wa lazima na hivyo kuchelewa kupata huduma kwa wakati”, amefafanua Bw. Siriwa.
Siriwa ameongeza kuwa, Kodi ya Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai Mosi ya mwaka wa fedha husika hadi Juni 30 ya mwaka unaofuatia na kusisitiza kuwa muda huu ni muafaka kabisa wa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.
Mamlaka ya Mapato Tanzania, katika kipindi cha miezi 6 iliyopita imefanya jumla ya semina 137 kwa wafanyakazi wa Serikali, Asasi za Kiraia, wafanyabiashara na vikundi mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na kuongeza uhiari katika ulipaji wa kodi.