Katika mambo mengi mazuri ambayo Serikali imeyafanya, hapana shaka ni kujenga uzio au kuta kuzunguka maeneo ya shule.

Miaka hii shule nyingi za Serikali hasa za mjini, zina uzio unaozunguka shule. Hili ni jambo zuri sana.

Tukiangalia Manispaa ya Kinondoni iliyopo mkoani Dar es Salaam, tutaona kwamba karibu shule zote za eneo la Kinondoni na Mwananyamala zina uzio isipokuwa shule mbili.

Shule hizo ni Shule ya Msingi Mwongozo iliyopo eneo la Mkwajuni na Shule ya Msingi Msisiri “B” iliyoko eneo la Mwananyamala.

Umuhimu wa kila shule kuzungukwa na uzio hauwezi kusisitizwa kwa sababu uko wazi. Kwanza uzio wa shule ni mpaka wa wazi unaodhibiti wanafunzi wasitoke eneo la shuke ovyo ovyo.

Bila uzio wa shule unakuta mwanafunzi anaadhibiwa isivyo halali kwa kuvuka mpaka wa shule ambao haupo wazi.

Pili, uzio wa shule ni mpaka wa wazi kati ya eneo la shule na eneo lisilo la shule. Kwa hivyo, ni rahisi kudhibiti vijana wahuni wanaogeuza eneo la shule kuwa kijiwe chao.

Shule haihitaji kutumia nguvu kuwafukuza vijana wahuni kama hao. Wanajua waziwazi kwamba hilo ni eneo la shule.

Tatu, uzio wa shule ni chombo madhubuti kinachozuia watu wenye tabia ya kuvamia maeneo ya wazi au ya umma wasivamie.

Ni katika ukweli huu wote kuhusu umuhimu wa shule kuwa  na uzio, Serikali ina sababu ya kupongezwa kwa kuona hilo hata imefanya juhudi kubwa kuzizungushia shule uzio. Kama tujuavyo, miaka hii kuna migogoro mingi ya ardhi na ya maeneo mbalimbali inayozushwa na watu wanaopanua shughuli zao za biashara.

Wakati mwingine maofisa wa halmashauri wasio waadilifu, wametokea kuelewana na wafanyabiashara hata wamewaruhusu kumega maeneo ya shule.

Jambo kama hilo linapotokea unakuta wanaolaumiwa na kusumbuliwa ni walimu wakuu.

Nakumbuka wakati mmoja maelewano kama hayo yalifanyika kati ya ofisa au maaofisa wa

 

Manispaa ya Ilala. Wakamruhusu mfanyabiashara mmoja kumega eneo la Shule ya Msingi Mnazi Mmoja kando ya Mtaa wa Lumumba karibu na Mahakama.

Mwekezaji alijenga hoteli, lakini kilichotokea ni kusumbuliwa na kudhalilishwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, hata ilidaiwa alipoteza maisha yake kwa shinikizo la damu katikati ya kadhia hiyo.

Nahofia hali kama hiyo kutokea Shule hii ya Msingi Mwongozo iliyopo Mkwajuni eneo la Kinondoni Manispaa ya Kinondoni.

Kwa kuanzia kampuni moja ya simu imeruhusiwa kujenga mnara wa simu eneo la shule, kando ya nyumba ya Mwalimu upande wa kaskazini mashariki kwa shule.

Karibu kabisa na mnara huo wa shule kuna baa ambayo upanuzi wake unaendelea. Kwa kuwa hakuna uzio au mpaka wa wazi kati ya shule na baa, unaweza kufika wakati ambao mwenye baa akaweza kumega sehemu fulani ya eneo la shule hiyo lililo kaskazini mashariki mwa shule.

Hilo likitokea litaleta athari mbili. Kwanza, utazuka mgogoro wa ardhi kati ya shule na mwenye baa. Mgogoro huu unaweza kuzuiwa sasa ama kwa manispaa kuweka mpaka wa shule wa wazi eneo hilo, au kwa manispaa kuanza kujenga sasa uzio wa Shule hii ya Mwongozo ukianzia eneo hilo la kaskazini mashariki mwa shule ambalo liko katika hatari ya kumegwa.

Pili, mbali na mgogoro wa ardhi unaoweza kuzuka kati ya shule na mwenye baa, eneo hilo likiruhusiwa kuwa sehemu ya baa litaathiri sana shughuli za shule na tabia ya wanafunzi. Wahenga wamesema, “usipoziba ufa utajenga ukuta”.

Kwa hivyo, manispaa isipochukua hatua sasa kuhakikisha kwamba eneo hilo la shule halimegwi, itajikuta iko kwenye mgogoro wa ardhi unaoweza kuathiri elimu katika Shule ya Msingi ya Mwogozo.

Tumeshuhudia mara nyingi mtu anavamia eneo la umma. Halafu anaachwa ajenge eneo hilo. Mwishoni mtu anatakiwa abomoe jengo alilojenga kama kwamba watendaji wa Serikali walikuwa wamelala mpaka mhusika alipomaliza kujenga.   Hatutaki hali hiyo itokee Shule ya Msingi Mwongozo.

Wala hatutaki kusikia kesho anasumbuliwa Mwalimu Mkuu wa Mwongozo, kutokana na kumegwa eneo la shule wakati Manispaa ya Kinondoni, Idara ya Ardhi imetakiwa mapema ichukue tahadhari.

Wakati huo huo, Manispaa ya Kinondoni haina sababu ya kubakiza mkia baada ya kufanya kazi kubwa nzuri. Tazama! Shule za msingi za Hananasifu, Mkunguni, Kumbukumbu, Kinondoni, Msisiri “A”, Mwananyamala Kisiwani, Mchangani, Mwananyamala “B” na Minazini zote zina uzio wa shule.

Hii ni kazi nzuri iliyofanywa na Manispaa ya Kinondoni eneo la Kinondoni na Mwananyamala. Katika hali hiyo, umma unaitazamia Manispaa ya Kinondoni kukamilisha kazi hii nzuri kwa kuzijengea uzio shule za Mwongozo na Msisiri “B”. Hapana shaka Manispaa ya Kinondoni itafanya kazi hiyo.


1789 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!