MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuonya Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko, kwa kushindwa kuwasiliana na mdhamini wake. Onyo hilo limetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, katika kesi ya kufanya maandamano yasiyo halali inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo mwenyekiti wake,  Freeman Mbowe.

Kabla ya kutolewa onyo hilo, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi, ameeleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (Ph) lakini mawakili wa utetezi hawakufika mahakamani.

Imeelezwa kuwa mshtakiwa wa tano, Esther Matiko,  hakufika mahakamani ambapo shahidi wake alieleza kuwa amepata dharura, na kwa vile mhusika alikuwepo, angeweza kueleza. Amedai kuwa alipigiwa simu ya dharura ili aende shuleni anaposoma mwanaye Agosti 1, mwaka huu,  na akaondoka saa 4 usiku.

 

Baada ya kueleza hayo Hakimu Mashauri alimhoji Matiko kuwa mbona mdhamini wake alishindwa kuieleza mahakama kwamba alikwenda kufanya nini Kenya. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 13, mwaka huu.

 

Mbali na Mbowe, washitakiwa wengine ni Katibu mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini Msigwa;  Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu Bara ambaye ni  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika;  Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche;  Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

By Jamhuri