Eti Lembeli naye anamsema Magufuli!

Wahenga waliwahi kusema kuwa nyani haoni kundule. Suala la vyeti feki na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Rais John Pombe Magufuli ndio ‘habari ya mjini’ sasa hivi. Uthubutu huu unastahili pongezi za dhati kutoka kwa watu makini na wapenda haki wote.
Kwa bahati mbaya sana, juhudi na hatua hizi za Mheshimiwa Rais zinabezwa na wasioitakia mema nchi yetu. Wabezaji na wakosoaji wa juhudi hizi wamekuwa wakijivika joho la ucha-Mungu na uzalendo wakati jamii inawajua kinyume.
Mmoja wa wabezaji wakubwa wa juhudi za Mheshimiwa Rais ni James Daudi Lembeli, aliyekuwa Mbunge wa Kahama (CCM), ambaye baada ya kushindwa kurejea bungeni kupitia CCM aliamua kukimbilia CHADEMA na sasa hivi amejikita kuichafua na kuibeza Serikali ya Mheshimiwa Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Tweeter.
Pamoja na mambo mengine, Lembeli amehoji kuwa kwa nini uhakiki wa vyeti uwabague baadhi ya watu huku wanasiasa wakiachwa. Sipingani na hoja hii na wala siwatetei waliogushi vyeti na taaluma. Hata hivyo, ninachokikataa ni nia yake katika hoja hii. Je, Lembeli anamaanisha kweli anachokisema? Nimelezamika kuandika makala hii kwani James Lembeli ninamjua vema.
Katika miaka iliyopita kuliibuliwa tuhuma kadhaa dhidi ya Lembeli, na alikwenda mahakamani kuyashitaki baadhi ya magazeti huku akidai kuvunjiwa heshma yake aliyoijenga kwenye jamii kwa muda mrefu. Hata hivyo, aliufyata baada ya kuumbuliwa pale ushahidi ulipowekwa hadharani na gazeti moja ambako alishiriki katika mchezo mchafu wa kuuza baadhi ya mbuga zetu za wanyamapori kwa kampuni binafsi ya Afrika Kusini.
Lembeli alifanikiwa kuuhadaa umma kiasi cha kuonekana kama msomi, mcha Mungu, mwadilifu, mkweli, mtetezi wa wanyonge, mzalendo na ‘mtambo’ wa kupambana na ufisadi! Ni kutokana na sifa hizi zilizotajwa na baadhi ya watu kwamba ni za kutunga, Lembeli aliwahi kushika nyadhifa za juu katika taasisi kadhaa ikiwa ni pamoja na Msemaji wa TANAPA na Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Kuna vyombo vya habari viliwahi kuhoji utata wa elimu ya Lembeli kama ambavyo ameweka mwenyewe kwenye taarifa zake, lakini hakuthubutu kukanusha au kutoa ufafanuzi.
Utata wa elimu ya Lembeli unaonekana kwenye taarifa zake alizotoa mwenyewe kwa vyombo viwili alivyokuwa anahusiana navyo. Vyombo hivyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako yeye alikuwa Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; na asasi ya Afrika Kusini inayoitwa African Parks Network (APN) ambako alikuwa Mjumbe wa Bodi; nafasi inayoaminika kuwa alipewa ili aweze kutumika kufikia malengo ya APN ya kununua na kumiliki hifadhi zinazozalisha hapa nchini.
Wasifu (CV) wa Lembeli kwenye tovuti ya Bunge ilikuwa inaonesha kuwa alisoma na kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Njombe. Aidha, alihitimu Diploma ya Uandishi wa Habari huko Kitwe, Zambia. Maelezo (profile) yake kwenye tovuti ya APN yalionesha kuwa alisoma na kuhitimu Diploma ya Uandishi wa Habari hapa Tanzania; na kwamba alikuwa anachukua Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza.
Lembeli hakuwahi kukanusha wala kusahihisha maelezo haya yanayokinzana ambayo aliyatoa yeye mwenyewe. Kwa hiyo hakuna chembe ya shaka kuwa hata yeye hajui kuwa alisoma wapi. Aidha, hicho Chuo cha Uandishi wa Habari cha Kitwe alichodai kusoma hakikuwahi kuwepo katika miaka hiyo.
Kutokana na maelezo yaliyo kwenye tovuti ya Bunge na ile ya APN, ni wazi kuwa historia ya elimu ya Lembeli inatia shaka. Mlolongo wa elimu yetu unaonesha kuwa stashahada (diploma) inapatikana baada ya kumaliza kidato cha sita au kusoma astashahada (certificate). CV ya Lembeli inaonesha kuwa kapata diploma yake moja kwa moja baada ya kuhitimu kidato cha nne. Hasemi kuwa alisoma wapi kidato cha sita au astashahada!
Lakini pia, kwa nini Lembeli asiwe wazi juu ya nchi alikosoma diploma? Ni Zambia au Tanzania? Je, mtu akisema anadhani kuwa diploma ya Lembeli ni ya ‘kuchonga’ atakuwa amekosea nini?
Kwa kutumia ujanja huo ambao nalazimika kuamini kuwa aligushi diploma yake, Lembeli alikuja na hekaya nyingine kwamba alikuwa anafanya Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano ya Umma huko Uingereza! Hakutaka kusema aliposoma shahada ya kwanza. Je, shahada ya kwanza kwake haikuwa ulazima na umuhimu? Inaeleweka kuwa siku hizi kuna shahada (degree) za kununua sokoni kama nyanya. Wachambuzi wa mambo ya kitaaluma walimtaka Lembeli awatoe Watanzania wasiwasi kuwa yeye hakuwa mmoja wa wanunuzi wa shahada hizi, hasa ikitiliwa maanani kwamba historia kuhusu taaluma yake tayari ilikuwa imeingia doa, jambo ambalo hakuwahi kulifanya.
Lembeli amewahi kuwa Afisa Uhusiano kwenye vyama vya ushirika na ‘Chief Manager’ wa Uhusiano wa Umma TANAPA. Bila shaka nafasi hizi alizipata kutokana na diploma ambayo kuna uwezekano wa asilimia 99 kuwa ilikuwa ya kugushi kutokana na yeye kushindwa kuwekwa wazi kuwa aliipata wapi na ilikuwaje akaipata kwa kuruka baadhi ya hatua kama elimu ya kidato cha sita au astashahada.
Ni wazi kwamba diploma hii ndiyo iliyomfanya Lembeli akaajiriwa TANAPA. Hata hivyo, inasemekana kuwa baadaye Lembeli aliingia kwenye mgogoro na mwajiri wake na moja ya masuala yaliyojitokeza ni utata kuhusu elimu yake. Baada ya mambo kuwa mazito alitimkia kwenye siasa na hivyo mjadala kuhusu elimu yake ukafa kifo cha kawaida.
Ni ajira ya TANAPA iliyotokana na diploma yenye utata iliyomfanya Lembeli aaminike kama mtaalamu wa uhifadhi wa wanyamapori na hatimaye kupata Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Ni uenyekiti huu uliomfanya awanyanyase na awajengee ‘fitna’ na ‘mizengwe’ watendaji waadilifu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, walioonekana kuwa kikwazo kwake katika kufikia malengo yake ya kiuchumi.
Ni uenyekiti huu wa Kamati uliozaliwa na diploma ‘isiyoeleweka’ ambao aliutumia kulazimisha aogopwe na kupewa safari za nje ya nchi na Wizara ya Maliasili ili kumziba mdomo. Ni uenyekiti huu ambao alikuwa akiutumia kama fimbo ili apewe Uenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori (TWPF) na kumnyanyasa yule aliyeshauri kuwa kumpa Uenyekiti wa Bodi kutazua mgongano wa maslahi kiutendaji.
Ni uenyekiti wa Kamati uliozaliwa na diploma hii uliomsaidia Lembeli kupewa zawadi ya ujumbe wa Bodi ya APN ili afanikishe mchakato wa kukabidhi mbuga zetu kwa makaburu wa Afrika Kusini. Nasema ni zawadi yenye lengo maalum kwa kuwa Lembeli hakuwa na taaluma ya uhifadhi hata chembe. Na Tanzania haina ukame wa wataalamu waliobobea katika fani ya uhifadhi. Kuwa Afisa Uhusiano TANAPA hakumfanyi mtu kuwa mtaalamu wa uhifadhi kama ambavyo huwezi kujiita wakili kwa kuwa eti umewahi kuwa dereva wa jaji.
Diploma hii isiyoeleweka ya Lembeli ndiyo iliyompa imani kuwa angeweza kuwa waziri siku moja. Na hii ndiyo sababu ya kuwasimamia kooni kwa hila mbaya mawaziri kadhaa akiamini kuwa siku moja angepewa uwaziri ili anyamaze.
Kama ambavyo alifanikiwa kutumia hila na kuhadaa watu na mamlaka kadhaa kuwa ni msomi wa diploma, Lembeli pia alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuuhadaa umma na kuthubutu hata kujifananisha na Mwalimu Nyerere, jambo ambalo lilikera watu na hata baadhi ya waandishi kulieleza kama kufuru na kutahadharisha kwamba kumfananisha Lembeli na Nyerere ni sawa na kufananisha giza na mwanga.
Leo hii Lembeli anapojifanya kusimama hadharani eti anabeza uthubutu wa Rais Magufuli kutumbua wale wenye vyeti feki namshangaa sana. Mtu aliyetumia ‘diploma isiyoeleweka’ kupora madaraka na nyadhifa ambazo alizitumia vibaya kuumiza watu binafsi na Taifa zima anapata wapi ujasiri wa kuhoji (moral authority)?
Kama Lembeli ana hakika na anayosema kumshambulia Mheshimiwa Rais Magufuli, basi aweke vyeti vyake hadharani tuvione!

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji wa JAMHURI mwenye makazi yake mkoani Simiyu

1286 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons