Watanzania tunakinyanyasa, kukibeua Kiswahili


“Lugha yetu ya Kiswahili imepata misukosuko mingi kwa kunyanyaswa na kubeuliwa kwa karne nyingi zilizopita. Unyonge wetu ulitokana na kutawaliwa na kudharauliwa uliotufikisha mahali ambapo hata sisi wenyewe tulianza kukinyanyasa na kukibeua Kiswahili.”

Kauli hiyo ilitolewa na Saadan Abdu Kandoro (STAHAKI) katika kifunguzi cha kitabu chake kiitwacho ‘Ushahidi wa Mashairi ya Kiswahili na Lugha Yake’ (Uk xvii).

 

Aya hiyo imenifanya nitie nanga katika safari yangu ya kuabiri ndani ya kitabu chake, ili nipate kusanifu maana na tafsiri ya maneno aliyosema. Ingawa sitakuwa sahihi moja kwa moja, basi angalau niseme na kujadili ili nikate kiu yangu juu ya maneno hayo.


Maneno hayo yananipa taswira ya kuwa ni indhari kwa mtu yeyote atakayepitia kitabu hicho. Na mtumiaji au mkereketwa wa lugha ya Kiswahili kutambua lugha hiyo ni chombo muhimu katika mawasiliano ndani ya jamii yetu.


Nilipokuwa nasanifu kauli ya Saadan Abdu nilizingirwa na kauli nyingine tatu tofauti, kutoka kwa magwiji wawili wa lugha ya Kiswahili na mwingine wa mambo ya siasa nchini. Magwiji hao ni Profesa Mugyabuso Mlinzi Mulokozi na Joshua S. Madumula, na Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru.


Profesa Mulokozi wa Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam (TATAKI) anasema, “Ipo hali ya kufifia na kulegalega kwa maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika miaka ya hivi karibuni.”


Naye Profesa Madumula wa Chuo Kikuu cha Eckernforde Tanga, anasema, “Lugha ya Kiswahili ni chombo muhimu katika kuwaunganisha wananchi kabla na baada ya Uhuru nchini. Lakini umuhimu huo unapungua na badala yake unapewa lugha ya kigeni.”

 

Mzee Ngombale-Mwiru wa CCM anasema, “Hali ya lugha yetu ya Kiswahili hivi sasa si nzuri sana. Kuna makosa mengi katika matumizi. Vipi Kiswahili kiwe tatizo wakati ni lugha ya msingi ya Taifa letu?”


Kauli hizo za magwiji wa lugha ya Kiswahili na siasa, zilitamkwa katika sherehe za uzinduzi wa kitabu cha historia ya hayati Sheikh Kaluta Amri Abeid (1924-1964), kilichoandikwa na hayati Mathias Eugen Mnyampala, kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, March 12, 2013.


Mtumiaji na mkereketwa yeyote wa lugha ya Kiswahili atashituka na kuguswa na kauli hizo, kwani zinaonesha  wazi Kiswahili hakipewi hadhi stahiki kimatumizi, isipokuwa kinapewa hadhi na utukufu kwa kuvikwa kilemba cha ukoka.


Hivi leo magwiji wa lugha ya Kiswahili, wanazuoni na wanangezi wa lugha, wakereketwa na Waswahili wanadai wanataka na wanapenda lugha yao itumike kifasaha katika kuandika na kuzungumza; na pia kipewe nafasi katika kufundisha masomo kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu.


Tamu na hamasa hiyo bado kupatikana kutoka kwenye vyombo vya uamuzi. Busara ya vyombo hivyo bado doro na mikono ya kutoa ni mifupi kufikia watumiaji Kiswahili. Nzumari inahitajika kuamsha busara na uhunzi unahitajika kurefusha mikono hiyo.


Mpiga nzumari na mhunzi wakipatikana na kufanya matilaba katika usanii wao, hapana shaka kibali kitapatikana kwa sababu lele za kutukuza, kuenzi na kuendeleza lugha ya Kiswahili zimeanza muda mrefu kusikika.


Kabla ya kusanifu kauli za magwiji hao wanne, Saadan Kandoro, Profes Mulokozi, Profesa Madumula na mzee Ngombale-Mwiru na magwiji wengine wa lugha ya Kiswahili watakaojitokeza katika makala haya, nitangulize pia fasihi na ushauri wa baadhi ya Waswahili.

 

Sheikh Shaaban Robart anasema, “Titi la mama litamu hata kama ni la mbwa.” Hayati Mathias Mnyampala anasema, “Lugha kama Kiingereza, Kiarabu na Kifaransa watu wanaweza kujifunza ili kupanua maarifa yao”.


Kutokana na maelezo hayo, nasema lugha ya Kiswahili ni yetu, hatuna budi kuikuza na kuithamini na wala si kuinyanyasa na kuibeua. Kila mdharau chake hufa maskini.

 

Mshairi na msanii mmoja wa nyimbo, Ali Mtoto Seif (kwa sasa ni marehemu), alipokuwa katika kikundi cha JKT Taarab, Mgulani, Dar es Salaam, alitunga wimbo uitwao ‘Moyo’. Baadhi ya maneno yanasema:


‘Ingawaje nina changu, kindani nyumbani kwangu, tena chaota ukungu, mithili ya nungunungu, sikithamini wenzangu, tena naona kichungu. Hata kwenye njozi zangu, huviota vya wenzangu, vinang’ara kama mbingu, na vitamu kama dengu, nikizinduka wenzangu, hunikithiri uchungu’.

Kutokana na shairi hilo, nakuuliza wewe Mswahili mwenzangu: Je, Kiswahili ni kichungu?


1455 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!