Mpita Njia (MN) hukutana na mambo mengi ambayo wakati mwingine
anashindwa kuyanyamazia, na hivyo kuwafanya baadhi ya watu wamwone
kama mtu ‘mfukunyuku’.
Februari 12, 2018, MN alikuwa miongoni mwa wasafiri wa ndege ya
Fastjet yenye namba FN-144 kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam. Akawa
amepata ndege ya saa 6:10 mchana na kutua saa 7:45 mchana JNIA.
Punde, ndege ikiwa inaelekea kwenye njia ya kupaa, akamsikia abiria
jirani yake akimwita mhudumu wa ndege na kumwomba ampatie parnadol
akisema alikuwa hajisikii vizuri.
MN akapanua sikio. Akamsikia yule mhudumu mwanaume akisema angetoa
dawa baada ya ndege kupaa na kutulia. Dakika 30 baadaye, yule abiria
akawa amebonyeza kengele kumwita mhudumu. Baada ya dakika 5 hivi
mhudumu akarejea. Yule abiria akakumbushia dawa. Mhudumu akamjibu kuwa
hawatoi parnadol kwa sababu wamempa abiria mwingine siku kadhaa
zilizopita na hizo dawa zikamsababishia mzio (allergy)! Yule abiria
akiwa anaweweseka, akasisitiza kuwa hana mzio wa hiyo dawa kwa hiyo
anaomba apewe tu.
MN akiwa amekodoa macho, yule mhudumu akagoma. Abiria akasimama na
kulalama, “Hivi angekuwa mzungu mngemnyima dawa?” Kusikia hivyo, wale
wahudumu wakaanza kumbembeleza. Mhudumu mmoja akamweleza yule abiria,
“Kama ‘kweli’ unaumwa turuhusu tutangaze endapo kuna daktari humu
akusaidie.” Yule abiria akachachamaa kwa kuhoji iweje asingizie kuugua
na kuomba dawa ambazo hata duka la dawa zinaweza kutolewa bila cheti
cha daktari?
Kuona mambo yanaelekea pabaya, mmoja wa wahudumu akatangaza kuomba
daktari kama yumo ndani ajitokeze. Bahati nzuri akajitokeza mama mmoja
aliyetambuliwa kwa jina la Bhoke. Huyu alikuwa na mama yake
anayesumbuliwa na shinikizo la damu. Yaelekea alikuwa akimpeleka
hospitali ‘kubwa’.
Akawa na kipimo cha shinikizo la damu. Akamfuata yule mgonjwa (abiria)
na kumpima. Akabaini shinikizo la damu lilikuwa juu. Akamwuliza dawa
anazotumia, akamjibu “coated aspirin” au parnadol zinamsaidia
kutuliza. Basi, yule mgonjwa akapewa coated aspirin. Baada ya dakika 5
hivi jasho likamtoka kweli kweli. Akawa amepata nafuu.
Tukio hili likamfanya MN ajiulize maswali mengi. Fastjet huu ni
ubahili (maana kila kitu wanauza) au ni roho mbaya kwa abiria weusi?
Je, ni kweli hawakutoka parnadol kwa sababu ya kuhofu mzio kwa mgonjwa
au hawana kabisa “Kisanduku cha Huduma ya Kwanza”? MN anadhani kuna
sababu kwa mamlaka kulichunguza tukio hili maana kama mambo ndiyo
haya, basi abiria wa Fastjet wawe tayari kukabiliana na kifo bila
msaada ndani ya ndege za shirika hili. Kama kuna mamlaka inataka
maelezo, basi iwasiliane na MN kupitia kwa mhariri maana hili ni
janga.

By Jamhuri