Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, inaendelea na mchakato wa kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Uelimishaji na uhamasishaji unatekelezwa kupitia warsha mbalimbali za kikanda zinazoendelea kufanyika hapa nchini.

Lengo ni kuhakikisha wadau wote kupitia wizara, wakala na idara zake, halmashauri na Serikali za Mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia ikiunganisha taasisi za kidini, vikundi vya kijamii, na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) wanaelimishwa na kuhamasishwa.

Mbali na kuelimisha na kuhamasisha, warsha zinalenga kuwajengea uwezo maafisa mipango na maendeleo ya jamii kwenye halmashauri zote nchini ili kushuka kwa wananchi vijijini, kuona kero zao na kuziingiza kwenye mipango ya maendeleo kimkakati kwa lengo la kuleta matokeo chanya kwa wote.

Awamu ya pili ya mpango huo imeanza 2016/17 na itakwisha 2020/21. Mpango huo umeandaliwa kwa kuangalia maendeleo ya kisekta na kikanda, na moja ya maeneo yaliyozingatiwa wakati wa uandaaji wa mpango ni Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. 

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imebainisha malengo matatu ya kipaumbele ambayo ni kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri; kudumisha uongozi na utawala bora, na mwisho kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na umaskini.  

Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo inajitokeza katika Mpango wa miaka 15 ambao umegawanywa katika awamu tatu ya miaka mitano mitano. Mpango umelenga mambo makuu manne ambayo ni; kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu kwa kujenga msingi wa uchumi na viwanda utakaoleta mapinduzi ya kilimo. 

Kilimo kinachozungumziwa katika viwanda ni kilimo cha kibiashara kinachoweza kubadilisha dhana ya bidhaa kuuzwa ghafi kama ilivyo hapa nchini na kuelekea kwenye bidhaa zilizosindikwa na kuongezwa thamani.

Kilimo cha namna hiyo kitachangia zaidi fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo na biashara, hivyo kwenda sambamba na lengo la nane la Malengo ya Maendeleo Endelevu, linalotaka kuboresha na kukuza uchumi endelevu wenye kutoa ajira na kazi zenye staha kwa wote. 

Katika mpango wa pili wa maendeleo ni utekelezaji wa lengo namba moja la Malengo ya Maendeleo Endelevu la kutokomeza umaskini. Kilimo na viwanda ni sekta inayoweza kutoa ajira kwa watu wengi, si lazima viwe viwanda vikubwa bali hata vile vya kati vyenye uwezo wa kutoa ajira kwa watu wengi zaidi na vile vidogo vidogo kama vile vinavyoratibiwa na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).

Awamu ya pili ya maendeleo imeeleza aina ya viwanda vinavyoweza kuleta tija katika suala zima la kupambana na umaskini. Moja ni viwanda ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake inapatikana nchini, hususani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili. 

Viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi kama vile nguo, viatu na mafuta ya kupikia; na mwisho ni viwanda vinavyotumia teknolojia na kuajiri watu wengi. Uanzishaji wa viwanda vyenye sifa tajwa hapo juu, unaenda sambamba na lengo la tisa la Malengo ya Maendeleo Endelevu linalosisitiza kuanzisha viwanda endelevu. 

Mpango umelenga kufungamanisha maendeleo ya uchumi na watu, ili uchumi ukue ushiriki wa watu wa makundi yote ni muhimu sana, maendeleo ya watu yanahusisha pia kupanua fursa za upatikanaji wa elimu bora kwa watu wote itakayowezesha wananchi kujiajiri au kuajiriwa; na hivyo kupanua wigo wa ushiriki wao katika sekta ya viwanda. 

Maendeleo ya watu yanaenda sambamba na kupata elimu, na kuimarisha afya za wananchi ikijumuisha huduma za matibabu, usalama wa chakula, upatikanaji wa viinilishe, maji safi na salama, na hifadhi ya jamii. Malengo ya Maendeleo Endelevu kwenye lengo la tatu na nne yanasisitiza pia afya bora na ustawi kwa rika zote na elimu bora inayotolewa kwa usawa na kutoa fursa kwa wote kujiendeleza. 

Mtu mwenye elimu na afya bora ni rasilimali muhimu katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Umaskini, ujinga na maradhi ni kikwazo namba moja kwa maendeleo yoyote yale – yawe ya uchumi au viwanda. 

Mpango wa Maendeleo na Malengo ya Maendeleo Endelevu yanaweka wazi kwamba ili tuweze kutokomeza umaskini uliokithiri katika nyanja zote na kila mahali kuwekeza katika elimu na afya bora, ni masuala ya msingi na ya kutiliwa mkazo.

Kwenye suala la afya, malengo yanasisitiza kuzuia vifo vya watoto hasa walio chini ya umri wa miaka mitano, kuzuia vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, na kuzuia maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha ukimwi.

Malengo yamejikita pia katika kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuongeza upatikanaji wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ambazo kwa sasa zinapatikana kwa wingi zaidi.  

Aidha, Serikali, kupitia Wizara ya Afya, imetoa tamko kuwaomba wale wote watakaobainika kuwa wameambukizwa virusi vya ukimwi, kuanza mara moja kutumia dawa zinazofubaza virusi hivyo bila kujali kiwango cha chembe chembe za CD4 zilizoko mwilini.

Hili ni jambo bora kwa ustawi wa maisha ya watu, lenye kukusudia kurefusha maisha ya rasilimali watu inayohitajika sana katika sekta ya kilimo na viwanda. Taarifa kutoka Wizara ya Afya zinatia matumaini kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wajawazito wenye VVU wanapata dawa za kukinga watoto wao. 

Hii inaashiria kwamba nguvukazi itakayopatikana hapo baadaye kama watapewa elimu bora na kuwa na afya bora, ni mtaji mzuri wa baadaye katika sekta ya kilimo na viwanda, na maendeleo ya nchi kwa ujumla. 

Katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Fatma Mrisho, alikaririwa na chombo kimoja cha habari akieleza kwamba dhamira ya shirika hilo ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 tunakuwa na Tanzania isiyo na maambukizi, unyanyapaa, wala vifo vitokanavyo na ukimwi. 

Dk. Mrisho anaeleza kwamba kwa sasa Tume yake inatekeleza mkakati ujulikanao kama sifuri tatu, ikiwa na maana ya kumaliza maambukizi mapya ya ukimwi, kukomesha unyanyapaa, na mwisho kukomesha  maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto  kwa asilimia sifuri. 

Hii ni njia mojawapo muhimu ya kufungamanisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu. Bila kuwa na jamii yenye afya bora ni dhahiri kwamba dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda yaweza kuwa ngumu kutekelezeka. 

Taarifa za kutia matumaini kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, ni kwamba dawa za ARV zinafanyiwa marekebisho ili kumwezesha mtumiaji asizitumie kila siku – ikiwezekana zitumike mara moja kwa mwezi.

Urahisi wa utekelezaji wa malengo husika kisekta, umejikita katika utekelezaji wa Mpango wa awamu ya pili wa Maendeleo. Katika kuwianisha viwanda na maendeleo ya binadamu, Mpango wa Maendeleo unahamasisha uendelezaji wa mipango miji, nyumba na maendeleo ya makazi mijini.

By Jamhuri