Gwiji wa soka barani Afrika na duniani, ametangazwa kuwa Rais wa Liberia na kuchukua mikoba ya Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika Ellen Johnson Sirleaf aliyemaliza muda wake.

Ushindi wa Weah umetokea wakati kumbukumbu zikionesha kuwa mwaka 2005, aliwania kiti hicho na kushindwa katika raundi ya pili na Sirleaf.

Mwaka 2011, Weah akashiriki tena Uchaguzi Mkuu nchini humo, akiwa mgombea mwenza wa Winston Tubman. Ulipofika mwaka 2014 mwanasoka huyo bora wa dunia alishinda kiti cha useneta kupitia chama cha Congress for Democratic kwenye kaunti ya Mountserrado, wadhifa aliokuwa nao hadi anachaguliwa kuwa Rais wa Liberia.

Ushindi huo ameupata baada ya kumshinda mpinzani wake, Joseph Boakai aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo kwa kaunti 12 kati ya 13 za nchi hiyo.

Weah kabla ya kushinda nafasi hiyo, amekuwa Seneta wa Bunge la Liberia tangu mwaka 2015.

Pia amewahi kuwania  kiti hicho mara mbili yaani 2005 na 2011 akiwa mgombea mwenza.

Pamoja na changamoto za kisiasa, Weah hakukata tamaa zaidi ya kuendelea kujiongezea umaarufu na kuwa mtu mwenye ushawishi kwa watu wa nchi yake.

Katika muda wote huo, alikuwa akiendelea kuwa balozi kuhamasisha elimu kwa watoto waliopoteza matumaini, chini ya mradi uliokuwa na udhamini wa Shirikisho la Sokan Duniani ( FIFA).

Mwaka 2012, Weah aliwatangazia wananchi wa Liberia kwamba amekubali kuwa balozi wa amani katika uongozi wa Rais aliyemaliza muda wake.

Mwaka 1997, UNICEF walimtambua kama balozi wa kujitolea katika masuala ya utoaji wa elimu ya kupambana na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na ukimwi.

Pia aliwasaidia watoto walioathiriwa na mafunzo ya kijeshi kwa kuwapa mafunzo ya kuwajenga kisaikolojia.

Weah alizaliwa Oktoba Mosi, 1966 katika kitongoji cha Slum, mji ulioko Kusini Mashariki mwa Monrovia nchini humo.

HISTORIA YAKE KATIKA SOKA

Mwanasoka  huyu mahiri ameweka historia katika soka Afrika na duniani kwa kuwa mchezaji bora wa dunia wa kwanza kuwa Rais wa nchi.

Akiwa mchezaji mpira, Weah alianza safari ya kusaka mafanikio ya soka katika vilabu mbalimbali nchini mwake, kabla kwenda Ulaya kutafuta maisha bora.

Akiwa Ulaya, alitumia zaidi ya miaka 14 kucheza soka katika timu za nchi mbalimbali kama Ufaransa, Italia na England.

Kwa mara ya kwanza aliingia barani Ulaya mwaka 1988 na kujiunga na klabu ya Monaco ya Ufaransa, wakati huo kocha wa timu hiyo akiwa ni Arsene Wenger.

Akiwa katika klabu hiyo alikuwa ni sehemu ya timu iliyoshinda (French cup) mwaka 1991 na kuisaidia klabu kufikia hatua ya fainali kwenye mashindano ya Europeans cup winner mwaka 1992 kwa kufunga magoli manne katika michezo tisa aliyocheza.

Hakukaa sana na klabu hiyo na ilipofika mwaka 1992, alijiunga na klabu ya Paris Saint Germain ya nchini humo.

Akiwa klabuni hapo pia aliwezesha kushinda ubingwa wa ligi (liguer 1) na 1994 akawa mfungaji bora wa mashindano ya ngazi ya Vilabu Bingwa Ulaya (UEFA champion leaguer) mwaka 1994-95.

Mwishoni mwa 1995 alihama na kwenda kujiunga na klabu ya AC Milan ya nchini Italia.

Alikaa ndani ya  klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne na kufunga magoli muhimu katika mashindano mengi aliyocheza, kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Serie A mara mbili, 1996 na 1999 .

Mafanikio yaliyoiwezesha klabu hiyo ya ACMilan kutinga hatua ya fainali mwaka  1998 na kutwaa  kombe (Coppa Italia).

Alipopata tuzo ya Afrika kwa mara ya kwanza 1989,  ilikuwa kubwa katika soka na  jarida moja la nchini Ufaransa, lilikariwa likisema kuwa ilimfungulia njia ya kusonga mbele katika maisha ya  soka.

Aliendelea kuiteka soka la Ulaya na ilipofikia 1995, alichaguliwa kuwa mshindi wa tuzo ya ballon d’or na kutajwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa FIFA.

Safari yake katika soka iliendelea barani Ulaya na ilipofika mwaka 1996 alikuwa ni alichaguliwa mchezaji wa pili wa FIFA.

Hata hivyo alijikuta akifungiwa kucheza mechi sita za klabu bingwa Ulaya baada ya kumpiga kichwa beki wa kireno, Jorge Costa.

Hiyo ilikuwa Novemba 20, 1996 katika pambano kati ya AC Milan na FC Porto.

Ilipofika Januari 20, aliamua kuhamia nchini Uingereza na kujiunga na klabu ya Chelsea na kufanikiwa kushinda taji la F.A cup mwaka 200 na baadaye akahamia klabu ya Manchester City na kisha kurudi nchini Ufaransa katika klabu ya Olypique Marseille.

Baada ya kutoka nchini Ufaransa Mei, 2001, Weah alienda kumalizia soka lake katika nchi ya Falme ya Kiarabu katika klabu ya Al Jazira kabla ya kustaafu soka mwaka 2003.

Pamoja na mafanikio aliyopata mpaka anastaafu mpira katika ngazi ya vilabu, upande wa timu ya taifa hakuwa na mafanikio ya kujivunia.

Alifanikiwa kucheza mechi 60 na kufunga magoli 13 tu, japokuwa mpaka anastaafu soka bila ya kushiriki katika dunia, lakini mchango wake ndani ya timu ya taifa ulikuwa ni mkubwa.

Kuna wakati alikuwa mfadhili na mwalimu, akiwajibika mpaka kuwalipa posho wachezaji wa benchi la ufundi.

Mafanikio mengine katika ngazi ya timu ya taifa yalikuwa ni kushiriki katika mashindano ya mataifa huru ya Afrika 1996 na 2002 na kuishia katika hatua za awali.

Baada ya kuachana na maswala ya soka, Weah aliamua kujiingiza katika masuala ya kisiasa na kuwania urais mwaka 2005.

Kwa kutambua nguvu ya soka katika kuleta amani ya Liberia, Weah aliwekeza dola za kimarekani milion mbili kama mishahara na gharama za usafiri  na vifaa kwa timu ya taifa ya Liberia (The Lone Stars.)

Akiwa kama meneja wa timu  ya Taifa, aliwaongoza vyema hadi kufika kwenye mashindano ya kombe la dunia mwaka 2002 na kushinda katika nafasi ya makundi na kutolewa katika kinyang’anyiro hicho katika hatua za mwisho.

ELIMU.

Weah ana Shahada ya Kwanza ya Uendeshaji Michezo kutoka Chuo Kikuu cha Parkwood kilichopo Uingereza. Hata hivyo baadhi ya watu wanatilia shaka shahada hii kwa kuwa chuo hicho kinajulikana kwa kutoka shahada bila kusoma hapo.

Baadaye alipata Shahada ya Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kikuu cha DeVry kilichopo nchini Marekani.

Mwaka 1999 alipata Shahada ya Udaktari ya Heshima kutoka Chuo Kikuu cha A.M.E Zion nchini Liberia.

Inasemekana kuwa kwa mara ya kwanza Rais huyu mteule alipogombea urais wa Liberia, hakuwa na elimu ya kutosha na wanadai kuwa ilichangia kwa kiwango kikubwa kushindwa kwake katika kuwania kiti hicho.

Familia na Kabila

Weah anatoka kabila la Kru lililoko upande wa kusini-mashariki mwa Liberia kwenye Kaunti ya Grund Kru ambayo ni moja ya maeneo yaliyokubuhu kwa  umasikini wa hali ya juu nchini humo.

Wazazi wake ni William T. Weah, Sr. na Anna Quayeweah. Alilelewa zaidi na bibi yake upande wa baba, Emma Klonjlaleh Brown.

Alihudhuria shule ya msingi katika shule ya Muslim Congress na sekondari katika shule ya Wells Hairston High School.

By Jamhuri