Wizara imekurupuka kuanzisha Wiki ya Elimu

Hii ni Wiki ya Elimu Tanzania. Tanzania inaadhimisha Wiki ya Elimu kwa mara ya kwanza.

Lengo la Wiki ya Elimu tunaambiwa kwamba ni kusherehekea mafanikio na kujituma, pia kuwapatia motisha watu mbalimbali waliosaidia juhudi za kuboresha elimu nchini wakiwamo wanafunzi, walimu na shule.

Kaulimbiu ya Wiki ya Elimu ni, “Elimu bora kwa wote inawezekana. Timiza wajibu wako.”

Kwa jumla, uamuzi wa kuwa na Wiki ya Elimu Tanzania ni mzuri. Lakini tukitaka kusema kweli (na lazima tuseme kweli), Wizara imekurupuka kuanzisha Wiki ya Elimu.

Kwa upande mmoja, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haikutoa taarifa yoyote mapema kwa walimu na wanafunzi wao kwamba watakuwa na siku yao. Wiki ya Elimu ni wiki ya walimu na wanafunzi wa shule. Kwa hivyo, ushiriki wao katika wiki yao hii umekuwa mdogo sana!

Ajabu ni kwamba Waziri wa Elimu alikuwa na maofisa wote wa elimu mjini Morogoro miezi michache iliyopita. Mbona hakuwashirikisha jambo hili zito? Ushirikishwaji unakosekana!

Lakini kwa upande mwingine, Wizara haina chochote cha kusherehekea kipindi hiki.  Hakuna mafanikio yoyote yaliyopatikana katika sekta ya elimu kiasi cha kufanya sherehe. Juu ya yote, Wizara haikujituma.

Kwa upande wa kaulimbiu ya Wiki ya Elimu, “Elimu bora kwa wote inawezekana. Timiza wajibu wako.”

Hapa haijulikani nani anatakiwa atimize wajibu wake. Maana wanafunzi, walimu na wazazi wanatimiza wajibu wao. Tatizo ni wizara yenyewe. Haitimizi wajibu wake, wala haijitumi!

Kwa kuwa matatizo ya elimu (ambayo yanaitwa changamoto) ni makubwa mno, tulitazamia kwamba Wizara ingeshughulikia kwanza mambo mbalimbali yanayopigiwa kelele. Baada ya hapo ingeanzisha Wiki ya Elimu kutafuta kuungwa mkono baada ya Wizara yenyewe kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Katika mazingira hayo, umma wa Tanzania unashangaa Wizara inasherehekea mafanikio yapi na kujituma kupi!

Bado watoto wetu wanamaliza shule wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Sababu iko wazi. Leo watoto wadogo, yaani wanafunzi  wa darasa la kwanza na la pili wanafundishwa masomo tisa! Wanafundishwa Hisabati, Kiswahili, English, Sayansi, Tehama, Stadi za kazi, Haiba na Michezo, Kifaransa na Dini!

Hawafundishwi kusoma na kuandika. Ni kweli Kenya wanafunzi wa madarasa hayo wanafundishwa masomo11, Burundi masomo 11, Rwanda masomo 10 na Uganda masomo tisa.

Lakini hatuwezi kulinganisha maendeleo ya elimu katika nchi hizo na yetu. Kule kwa wenzetu Wizara ya Elimu inasimamia elimu kwa ufanisi na umakini. Haisambazi vitabu vibovu shuleni, lakini pia kule wana vifaa bora vya kufundishia kusoma na kuandika. Sisi huku masomo ya kusoma na kuandika tumefuta kabisa!

Kwa hiyo, haishangazi kusikia kuwa upimaji wa wanafunzi wa darasa la pili uliofanyika katika halmashauri 20, umeonesha kwamba katika kila wanafunzi 100 waliopimwa, wanafunzi 92 hawakuweza kusoma na kuelewa!

Katika mazingira hayo, tunasherehekea nini? Wizara ifanye kazi kwanza ili katika wanafunzi 100 watakaopimwa 92 waweze kusoma na kuandika. Ndipo ianzishe upya Wiki ya Elimu ya kusherehekea mafanikio na kujituma.

Bado wakaguzi wa shule hawatimizi wajibu wao wa kuendesha semina za masomo wanayoyakagua. Badala yake wanakwenda shuleni kukaripia na kukemea walimu kwa kufundisha vibaya masomo ambayo hawakuelekezwa namna ya kufundisha vizuri!

Ni jukumu la wakaguzi wote kuendesha semina za masomo yote. Lakini kuna walimu wanakiri kuwa hawajahudhuria semina yoyote katika miaka kumi iliyopita. Wanaletewa masomo mapya shuleni bila kufanyiwa semina.

Na sasa umezuka mtindo mbovu sana. Walimu wanatakiwa wajiitishie semina kwenye kata waziendeshe na waelekezane wenyewe! Hii haijatokea katika nchi yoyote isipokuwa Tanzania. Tuseme wakaguzi wa shule hawana uwezo na ujuzi wa kuendeshea semina za masomo wanayokagua? Kwa kweli sijaona tunachosherehekea.

Bado silabasi zinazotumika kufundishia masomo mbalimbali hazikutungwa kwa ufanisi na zinavuruga walimu.

Chukua kwa mfano, silabasi ya Historia darasa la tano. Mwalimu anatakiwa afundishe utawala wa Wajerumani Tanganyika, Tanganyika chini ya utawala wa Waingereza, utawala wa kisultani Zanzibar, mapambano ya Watanganyika dhidi ya Wajerumani, na kadhalika. Silabasi hazikutungwa kwa mfululizo unaomsaidia mwanafunzi kuelewa somo.

Huwezi kufundisha utawala wa Waingereza Tanganyika kabla hujafundisha mapambano ya Watanganyika dhidi ya Wajerumani. Pia huwezi kufundisha ukoloni wa Wajerumani na Waingereza kabla ya utawala wa kisultani Zanzibar.

Kana kwamba ubovu huo haujatosha, bado kuna tatizo kubwa la vitabu wanavyotumia walimu kufundishia masomo mbalimbali. Pamoja na Wizara kutahadharishwa isisambaze vitabu shuleni bila kuanza kutafuta maoni ya walimu walivyovitumia, Wizara imetumia vibaya fedha ya rada kwa kusambaza vitabu vibovu shuleni.

Tatizo jingine ni hili: Walimu wanatumia vitabu vitatu au vinne katika darasa moja kwa somo moja, vyenye maelezo tofauti.

Chukua, kwa mfano, mazao ya biashara yaliyomo katika Nembo ya Taifa. Oxford University Press wanasema ni pamba na karafuu. Educational Books Publishers wanasema ni pamba na kahawa.

Halafu bado kuna tatizo la madawati. Inaonekana fedha ya rada iliyotengwa kwa ajili ya kununua madawati imeyeyuka. Hatusikii madawati hayo yamesambazwa wapi.

Kisha bado kuna masomo ya Stadi za Kazi na Tehama ambayo yanawapotezea wakati walimu na wanafunzi wao. Hakuna  walimu waliopewa mafunzo ya kufundisha  masomo hayo na hayana vifaa vya kufundishia! Kwa hivyo, lengo la masomo hayo kuwasaidia wanafunzi wanaorudi nyumbani kujiajiri limepotea kabisa!

Vile vile, bado masomo ya Historia na Uraia yaliyokusudiwa kuwajengea  wanafunzi uzalendo yameendelea kupuuzwa na Wizara! Kwanza, masomo hayo yalifutwa kabisa! Yaliporejeshwa masomo hayo si tu yana vipindi vichache zaidi shuleni bali katika Mtihani wa Taifa huulizwa maswali 14 wakati masomo mengine huulizwa maswali 50.

Juu ya yote, bado walimu wana madai yasiyo na idadi ambayo hayashughulikiwi! Ni katika mazingira hayo tunaulizana Wizara inasherehekea mafanikio yapi na kujituma kupi?

Sasa basi, kwa kuwa katika Wiki hii ya Elimu, Wizara ya Elimu inasherehekea kujituma tunaitazamia kwamba itaendelea kujituma kwa kuboresha maandalizi ya Wiki ya Elimu ya mwaka 2015.