Hali zinabadilika, mabadiliko ni muhimu

Desemba 13, mwaka huu itatimia miaka 27 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliposema: “Hali zinabadilika. Tuendelee na chama kimoja cha siasa ama tuwe na vyama vingi vya siasa.”

Maelezo haya aliyatamka Desemba 13, mwaka 1991 alipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, alipotoa maoni na msimamo wake wa kutaka tubadilike kufuatana na hali, tuwe na vyama vya siasa nchini. 

Alisema kuwa huko nyuma kuanzia mwaka 1965 hatukuwa na vyama vingi vya siasa kwa sababu ya hali ilivyokuwa. Kuwa na vyama vya siasa ilikuwa ni kuipinga TANU na kuipinga ASP.  Ilionekana kama usaliti, usaliti kwa vyama hivyo, ambavyo vimeleta uhuru na ukombozi wa Watanzania.

Mwalimu Nyerere alisema kuwa ilikuwa vigumu pia kuwako na vyama vingi kutokana na sheria. Sheria ya nchi iliruhusu chama kimoja, haikuruhusu vyama vya siasa. Lakini ifahamike wakati huo walikuwapo watu waliopenda vyama vingi vya siasa. Ingawa watu hao hawakuwa wengi nchini. 

Nakumbuka Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Mimi naamini watu wanaipenda CCM. Kuna kundi linawapenda wanaodai mabadiliko. Viongozi wako serious. Ni wazalendo tu. Upande wa opposition ni minority. Watu wa kutosha, wanao viongozi.”

Mwalimu Nyerere aliendelea kusema: “Ya kwanza kubadili ni sheria. Si kufanya upinzani wa kijinga kijinga. Acha hawa wala pesa. Sisi tunaweza kuongoza mabadiliko yetu wenyewe, tukapata vyama si vya uhasama. Si vyama vingi.”

Vilevile alisema: “Chama na Serikali wanataka mabadiliko. Mabadiliko yoyote yanataka kiongozi.” Nimekariri baadhi ya dondoo za mazungumzo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kukumbushana kuepuka chuki, faraka na mapigano miongoni mwetu. 

Ikumbukwe hatimaye Serikali, CCM na wananchi walifuta fikra ya usaliti na kuweka mawazo kuhusu mabadiliko ya hali na mabadiliko ya sheria kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Mfumo ambao ulianza rasmi mwaka 1992, na vyama vingi vya siasa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa taifa wa kwanza mwaka 1995. 

Hakika hali inabadilika jinsi mambo yalivyo. Nazungumzia vizazi na mawazo yao, watu na mazingira yao. Rejea shabaha ya Wana TANU na Wana ASP ilikuwa kupata uhuru kutoka kwa wakoloni. Leo shabaha ya Wana CCM ni kujenga taifa, kuondoa ufisadi na kujenga uchumi imara. 

Aidha, wapo wasio Wana CCM wanayo shabaha hiyohiyo. Kadhalika wapo Wana CCM na wasio wana CCM wanaopenda ufisadi, kuvunja umoja wa kitaifa na kuharibu mbinu za ujenzi wa uchumi imara. Hizi ni kambi mbili zinazokinzana chini ya kigingi cha demokrasi, haki na utawala wa sheria. 

Kuwako vyama vingi vya siasa ni kuwapa nafasi wananchi kutoa, kupokea na kupanua mawazo na fikra juu ya demokrasia ya kweli, inayozingatia haki na utawala wa sheria kwa wananchi. Si kuwa chanzo cha usaliti wa vyama vya siasa, kupinga kijinga kijinga, kutotii sheria za nchi au kufifisha juhudi za maendeleo ya nchi.  

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, anasema: “Sisi tunaweza kuongoza mabadiliko yetu wenyewe. Tukapata vyama si vya uhasama.”  Je, katika kauli hii, tunajifunza nini na hali za mabadiliko kupitia vyama vyetu vya siasa nchini?  

Mimi naamini kama asemavyo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Hii ina maana kwamba Watanzania tunaweza kuongoza mabadiliko yetu wenyewe, tukitumia uzalendo wetu kuonyesha uaminifu, unyenyekevu, moyo wa upendo na ujasiri. Tunaweza. 

Ndani ya miaka 27 (1991 – 2018) tumeona na tumesikia baadhi ya watu kutenda yasiyo mema na kukwamisha mabadiliko. Mwaka ujao wa 28 (2019) na kuendelea tugange kufungua sura mpya ya kuleta mabadiliko ya kweli, kwani Tanzania mpya itajengwa na wananchi wazalendo.