DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel imesema changamoto kubwa kwake kibiashara mwaka huu imekuwa zoezi la kusajili laini kwa njia ya alama za vidole ambalo mpaka sasa hivi limeigharimu kampuni hiyo zaidi ya Sh bilioni 2.
Zoezi hilo limekuwa mtihani kwa Halotel na kampuni nyingine za simu za mikononi kwani agizo lake lilikuja ghafla katikati ya mwaka wakati bajeti za matumizi na mipango ya kutekelezwa kwa mwaka 2019 vilikwisha kupangwa.
Mwezi Mei mwaka huu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliziamrisha kampuni zote ze simu za mikononi
kusajili upya wateja wao wote kwa kutumia alama za vidole.
Kwa mujibu wa agizo hilo, zoezi la uandikishaji linapaswa kukamilishwa Desemba 31, mwaka huu.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Halotel, Nguyen Anh Son, amesema hivi karibuni kuwa sababu za kibiashara zimewafanya
kugharamia usajili wa wateja wao ambao wanakaribia kufika milioni tano.
Kufikia katikati ya mwezi huu, kampuni hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam ilikuwa imefanikiwa kuwasajili wateja
wake milioni 1.5 tu, wakati TCRA imezidi kusisitiza kuwa mwisho wa usajili ni Desemba 31, ambayo ni Jumanne wiki
ijayo.
“Ili kuendesha zoezi la usajili kwa ufanisi ilitubidi tuingie gharama ya kununua vifaa vya alama za vidole 10,000 kwa
gharama ya Sh bilioni 2. Kufanikisha usajili wa mteja mmoja inatugharimu Sh 400,” Son aliliambia JAMHURI katika
mahojiano maalumu ofisini kwake.
Kimahesabu, usajili wa wateja milioni 1.5 umeigharimu Halotel Sh milioni 600. Na kwa kuwa sasa hivi kampuni hiyo ina jumla ya wateja milioni 4.5, usajili wao wote utagharimu Sh bilioni 1.8 na kufanya gharama ya zoezi zima kuwa Sh bilioni 3.8.
Son anasema hizi ni fedha nyingi ambazo hazikuwa kwenye mipango yao ya matumizi ya mwaka huu lakini inabidi
zitumike kwani gharama ya kuwapoteza wateja ambao hawatasajiliwa ni kubwa zaidi.
TCRA inasema kufikia mwanzoni mwa mwezi uliopita, laini zilizokuwa zimesajiliwa zilifikia karibu milioni 17, sawa na
takriban asilimia 40 ya laini zote zilizokuwa sokoni katikati ya mwaka.
“Kibiashara mwaka huu ulikuwa mzuri zaidi ya mwaka 2018 kutokana na mabadiliko chanya sokoni lakini ulikuwa na
changamoto kubwa ya usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole,” Son anasema kwenye mahojiano na
JAMHURI na kuomgeza:
“Ni zoezi muhimu sana lakini limetugharimu fedha nyingi ambazo hazikuwa kwenye bajeti ya mwaka huu lakini kwa
sababu ya ustawi wa biashara yetu inabidi zitumike.”
Anasema mwaka 2020 utakuwa mwaka wa kuboresha huduma na bidhaa mbalimbali ili kujizatiti na kushindana
kwa mafanikio sokoni.

By Jamhuri