HATUPANGI KUSHINDWA, TUNASHINDWA KUPANGA (2)

Weka pamba masikioni usisikilize maneno yanayoua mawazo mapya

Mawazo ni muhimu katika kupanga. “Kupata wazo jipya lazima kuwe kama kukalia pini; lazima likufanye uruke na kufanya kitu fulani,” alisema E. L. Simpson. Jambo kubwa linaanza likiwa wazo dogo.

Jogoo wanaowika kuna wakati yalikuwa mayai. Jambo baya ni kuvunja mayai. Mawazo yanazaliwa, yanakua. Ukibeba mimba ya mawazo chunga watu wasiitoe kwa maneno yanayoua mawazo.

Kuna aliyesema: “Kupokea mawazo mapya epuka maneno haya yanayoua mawazo. Halipo kwenye bajeti. Nani amefikiria hilo? Tulijaribu hilo tukashindwa. Hatuko tayari. Si wakati muafaka. Ni vigumu sana  kulitawala. Ni la kufikirika sana. Haliendani na sera yetu. Litachukua muda mrefu. Linahitaji kufanyiwa kazi sana. Tusubiri tuone. Tuunde kamati. Kuna ambaye amelijaribu?” “Mawazo yanaanza yakiwa madogo. Haijalishi watu wanachokuambia, maneno na mawazo vinaweza kubadilisha dunia,” alisema Robin Williams.

“Litachukua muda mrefu,” ni maneno yanayoua wazo jipya. Acha lichukue muda mrefu. Roma haikujengwa siku moja. Mfaransa Marshal Louis Lyauley alipomwambia mtunza bustani wake kuwa anatamani kupanda aina fulani ya mti, mtunza bustani huyo alisema: “Mti huo ili ukomae na kuvunwa unachukua miaka mia moja.” Marshal Louis Lyauley alisema: “Kama ni hivyo hatuna muda wa kupoteza, tuanze kupanda mchana huu.” “Muda mzuri sana wa kupanda mti ulikuwa ni miaka 20 iliyopita. Muda wa pili mzuri sana ni sasa.” (Methali ya China).

“Ni vigumu sana kulitawala.” Ni maneno yanayoua wazo jipya. Washindi wanaona majibu katika kila jambo gumu. Watu wanaoshindwa wanaona jambo gumu katika kila jibu.

Washindi husema: “Linaweza kuwa wazo gumu, lakini linawezekana.” Watu wanaoshindwa wanasema: “Linawezekana lakini ni jambo gumu.” Washindi wanaona fursa katika kila jambo gumu. Watu wanaoshindwa wanaona jambo gumu katika kila fursa.

“Linahitaji kufanyiwa kazi sana,” ni maneno yanayoua wazo jipya. Usikubali maneno hayo yakuvunje moyo. “Kunguru mkaa bure hufa njaa.” (Methali ya Iceland). Usipolifanyia kazi wazo lako utakufa njaa.

Neno ‘kazi’ katika Kamusi ya Kiswahili linatangulia neno ‘mafanikio.’ Mafanikio hayaletwi kwenye sahani ya dhahabu bali yanafanyiwa kazi.

“Tusubiri tuone,” ni maneno yanayoua wazo jipya. Ngoja ngoja huumiza tumbo. Chuma hupata kutu kutokana na kutotumika. Maji hupoteza usafi wake sababu ya kutuama. Kutofanya lolote kunaua mawazo.

“Usisubiri: muda hautakuwa kamwe, ‘muda sahihi.’ Anzia ulipo, na tumia vifaa ulivyonavyo vifaa vizuri zaidi vitakukuta njiani,” alisema  Napoleon Hill.

“Haiwezekani,” ni neno linaloua wazo jipya. “Mtu anayesema haiwezekani asimwingilie ambaye analitenda.” (Methali ya China).  “Haiwezekani” si ukweli wa mambo bali maoni. Lisilowezekana linawezekana.

“Giza linakuja. Katikati ya utekelezaji, wakati ujao unaonekana patupu. Kishawishi cha kuacha ni kikubwa. Usiache. Uliye naye ni mwema. Utajiambia hakuna njia ya kutoka. Lakini pamoja na Mungu hakuna lisilowezekana. Ana kamba nyingi na daraja na njia za ardhini za kukutoa kwenye shimo zaidi ya unavyoweza kufikiria, sali daima. Tumaini,” alisema  John Piper.

“Hatuko tayari,” “hatujaandaliwa kisaikolojia.” Ni maneno yanayoua wazo jipya. “Hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika kama mtu atangoja alifanye vizuri sana kiasi cha mtu yeyote kutoona kasoro.” (John Henry Newman). Kusitasita ni ugonjwa, dawa yake tenda, anza.

“Watu watasema nini?” Ni maneno yanayoua mawazo mapya. Ukingoja watu wakukubali ndipo utende utakuwa mfungwa wa watu. Kama wanakujadili wamekukubali. Kama una wazo zuri, halali, usisikilize maneno ya watu. Maneno hayo ni daraja, halizuii maji kutiririka. Weka pamba masikioni usisikilize maneno ya watu yanayoua mawazo mapya.