Maisha bila malengo ni kama meli bila usukani

Watu wanaongozwa na malengo. Ni lengo gani linalokuongoza maishani? Watu waliofanikiwa wana malengo, ambao hawakufanikiwa wana matakwa au matamanio tu. Atakalo mtu hapati, hupata ajaliwalo. “Mtu asiye na lengo ni kama meli bila usukani – mtu aliyepotea, mtu bure, kabwela,” alisema Thomas Carlyle. 

Kuna ambaye amesema: “Kuishi bila mpango wa Mungu kwa maisha yetu ni kama kushona bila sindano, bila uzi, au kuandika hadithi ya maisha yako kwa kalamu ambayo haina wino.” Tunaweza kusema maisha bila malengo ni kama kalamu bila wino, ni kama sindano bila uzi. Kuwa na malengo kunaleta amani. 

“Wewe, Bwana, unawapa amani wale wanaotunza malengo yao kwa uthabiti na kuweka tumaini lao kwako.” (Isaya 26:3). Tunza malengo yako kwa uthabiti. Weka tumaini lako kwa Mungu.

Victor Frankl katika kitabu chake ‘Man’s Search for Meaning’ alijenga hoja kuwa mtu anapokuwa hana lengo la kuishi, hana wakati ujao wa kutegemea, anajikunja kwenye kona na kufariki dunia. Kutokana na matokeo ya utafiti wake katika kambi za kutesea za Wanazi, aliandika: “Jaribio lolote la kumrudishia mtu nguvu ya ndani katika kambi kwanza ilikuwa katika kumwonyesha malengo ya wakati ujao.”

Kuwa na malengo makubwa. Kaa na watu watakaokusaidia kuwa na malengo makubwa. Ukizungukwa na “mwewe,” utaruka juu sana kama mwewe. 

Kuwa na orodha ya malengo. Lengo la kwanza ni vizuri lihusu uhusiano wako na Mungu. Jonathan Edwards alizungumzia lengo la kumpa Mungu utukufu. “Azimio: watu wote kuishi kwa ajili ya Mungu. Azimio la pili: kama watu wengine wanaishi kwa ajili ya utukufu wa Mungu au la, mimi naazimia.” Kila unachokifanya kinaweza kuwa na lengo la kumtukuza Mungu. 

Lengo la pili ni vizuri likakuhusu wewe, kujiendeleza, kujitakatifuza na kuwa wewe zaidi. Lengo la tatu ni vizuri uwe ngazi ya kuwainua wengine. Hapa wanaingia wanafamilia, watu waliokuzunguka na nchi yako. Lengo hili  linahusu uhusiano wako na watu wengine. Usijiulize, watu wengine wanakufanyia nini? Bali wewe unawafanyia nini? Usijiulize, taifa linakufanyia nini? Bali, unalifanyia nini taifa? “Lengo la maisha ya binadamu ni kutumikia na kuonyesha huruma na nia ya kuwasaidia wengine,” alisema Albert Schweitzer.

Kuishi kwa malengo kuna faida nyingi sana. Kwanza ni kuvumilia. Mwanafalsafa wa Kijerumani alisema: “Yeye ambaye ana kwa nini ya kuishi anaweza kuvumilia namna yoyote.” Kwa nini unaishi? Upande wa kwa nini ukikosa maishani, kukata tamaa kunaingia na mtu anaweza kuaga dunia. 

Victor Frankl aligundua kuwa kwenye kambi za Wanazi za kutesea waliokuwa na malengo waliendelea kuishi. Malengo yao yalikuwa ya aina mbalimbali. Mfungwa mmoja alikuwa na mtoto mwenye ulemavu wa akili, alikuwa na tamaa kubwa ya kwenda nyumbani kumtunza. Mmoja alikuwa na msichana anamchumbia, alitegemea kufunga ndoa baada ya vita kumalizika. 

Victor Frankl mwenyewe alikuwa anamalizia kuandika kitabu, alikuwa na matumaini ya kuendelea kuishi na kumalizia kuandika kitabu chake na kukichapisha.

Pili, ni kuwa na furaha. “Vipengele vikubwa vya furaha ni: kuwa na jambo la kufanya, kuwa na jambo la kupenda na kuwa na jambo la kutumaini,” alisema Thomas Chalmers. Kuwa na jambo la kutumaini hilo ni lengo. George Bernard Shaw aliandika: “Hii ndiyo furaha ya kweli ya maisha: kutumiwa kwa ajili ya lengo unalolifahamu kuwa ni kubwa; ikiwa ni nguvu ya asili badala ya pupa za maumivu madogo madogo na manung’uniko, ukilalamika kuwa ulimwengu hauwezi kujitoa na kukupa furaha.” 

By Jamhuri